Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

KASAMBULA Fundi cherehani aliyenusurika na adhabu ya kunyongwa hadi kufa

10597 Fundi+pic TanzaniaWeb

Tue, 3 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Geita. “Mkuu wa gereza aliposoma majina na mimi kutajwa  miongoni mwa waliosamehewa nililia sana, si kwa sababu ya uchungu bali nilijikuta machozi yanatoka kama yamefunguliwa.”

“Nilipiga magoti nikamshukuru Mungu huku nalia toka niliposamehewa kunyongwa na kufungwa maisha nilikua naamini kuna siku nitatoka gerezani lakini siku naambiwa nimesamehewa sikuamini, nilijikuta nalia.”

Ni maelezo ya Julius Joshua maarufu kama Joachim Kasambula, aliyekua mfungwa kwa zaidi ya miaka 32 ambaye aliachiwa kwa msamaha wa Rais John Magufuli, Desemba 9, 2017.

Joachim Kasambula ni mtoto wa nne kati ya 11 wa Mzee Peter Kasambua, mkazi wa Nyankumbu mjini Geita na alifanikiwa kusoma hadi darasa la saba Shule ya Msingi Nyankumbu na kuhitimu mwaka 1977.

Kabla ya kufungwa Kasambula alikua anajishughulisha na kilimo na alibarikiwa kuwa na mke na watoto wanne.

Anasema mwaka 1984, historia ya maisha yake ilibadilika baada ya kutokea matatizo kati ya sungusungu (askari jamii) na familia yao.

Wakati huo wazazi wake walikua wakiishi Nyankumbu na wadogo zake na yeye, pacha wake na kaka zake wawili walikua wakijitegema na kuishi Msalala mjini Geita.

Katika hali ya kushangaza mama yake alituhumiwa kuwa mchawi huku baba na ndugu zake saba wa kiume kwa wizi na wazazi wao kutakiwa kuondoka eneo hilo.

Anasema wazazi na baadhi ya ndugu walitawanyika, wazazi walienda kuanza maisha mapya Tabora huku yeye na pacha wake Rock Kasambula au Samson Maige walisafiri hadi Singida.

Kasambula anasema mwaka 1984 walijikuta wakiingia katika kundi la biashara ya meno ya tembo na ngozi za chui kutoka Singida na kwenda kuuza Dar es Salaam.

Bila kujua kama kundi lile pia linajishughulisha na ujambazi, mwaka 1985 walikamatwa wakihusishwa kwenye kesi ya mauaji, walidaiwa kuiba benki mjini Singida, kwanza walimuua mlinzi kabla ya kufanya uhalifu huo.

“Kwa wakati huo lile lilikua tukio kubwa nchini, kwenye kundi letu la watu 12 kuna waliotambulika kwenye gwaride na mimi na ndugu yangu licha ya kutotambuliwa lakini tulihusishwa kwa kuwa ni kundi moja,” anasema na kuongeza kwamba wenzao 10 walitoka na wao walibaki ndani na kuhukumiwa adhabu ya kifo kwa kunyongwa kwa ushahidi wa kimazingira. Hiyo ilikuwa Agosti 11, 1989 na kupelekwa Gereza la Isanga mkoani Dodoma na kusubiri kunyong’wa.

 

Maisha gerezani Isanga

Tofauti na watu wanavyoamini kuwa gerezani ni sehemu ya mateso lakini kwa anayesubiri kunyongwa gerezani ni sehemu ya kupumzika, anachokosa ni uhuru wa kutoka nje.

Anasema mfungwa wa kunyongwa akiwa gerezani hafanyi kazi yoyote na hasumbuliwi, kazi yake kubwa ni kula na kulala huku akiandaliwa chakula kizuri na huletewa alipo kwa wakati.

Anafafanua kuwa mfungwa huyo hupewa maziwa, mkate, nyama licha ya kwamba kuna wakati havipatikani vyote lakini huwezi kulinganisha maisha ya mfungwa wa kunyongwa na mfungwa wa maisha.

Mwaka 2001 alihamishiwa Gereza la Ukonga baada ya kuugua na hivyo kuhitaji matibabu Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Anasema maisha aliyoishi Isanga ni tofauti na Ukonga kwani huduma za Ukonga zilikua bora zaidi na aliendelea kumuomba Mungu akiamini ipo siku atatoka.

Anasema mwaka 2002 akiwa Ukonga alipata taarifa ya kubadilishiwa kifungo kutoka cha kunyongwa na kuwa kifungo cha maisha wakati huo Ukonga kulikuwa na wafungwa zaidi ya 80 wanaosubiri kunyongwa, wawili akiwemo yeye ndio walipata msamaha wa Rais.

Anasema licha ya kufurahi lakini alikua anamuwazia pacha mwenzake ambaye walikua wote Isanga na kuhamishiwa Gereza la Maweni mkoani Tanga kama amebahatika au ataendelea kusubiri kunyongwa.

Anasema kwa msaada wa mkuu wa gereza alipata taarifa za pacha wake naye kubadilishiwa kifungo na baada ya muda alihamishiwa Ukonga hadi alipofariki akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari.

 

Kifungo cha maisha

Kasambula anasema ni kama alipelekwa kwenye ulimwengu mwingine na kukuta maisha mapya tofauti na alivyokua kwenye kifungo cha kunyongwa.

Alisema kwenye kifungo cha maisha kila kitu kinaenda kwa muda, kuna wakati maalum wa kuamka, kula na kazi, aliishi kama mgeni kwa siku nne na baadaye kupelekwa kiwandani kufanya kazi, alichagua kazi ya ufundi wa kushona nguo.

“Gerezani ni chuo cha mafunzo kuna kila aina ya ufundi wapo mafundi seremala, wafumaji, utengenezaji sabuni, ushonaji, ufundi magari na ufundi mwingine, mfungwa anachagua anachotaka kujifunza,” anasema Kasambula.

Anasema maisha ya kunyongwa mfungwa hafundishwi chochote, ni kama tayari amepotea na anasubiri saa tu lakini yule wa maisha anafundishwa kujitegemea wakiamini iwapo atabahatika kutoka basi ataweza kubadilika.

Anasema nguo nyingi za viongozi, samani za ndani ya Bunge na kwenye taasisi za Serikali hushonwa na wafungwa.

 

Changamoto za mfungwa wa maisha

Anasema tofauti na mfungwa wa kunyongwa kifungo cha maisha ndio kifungo au unaweza sema hiyo ndio jela kwani  mfungwa wa kunyongwa husumbuliwi na mfungwa mwenzako au askari magereza, mara nyingi wafungwa wa aina hiyo hubadilika wenyewe na kuwa wapole wenye nidhamu ya hali ya juu, maisha yao huyakabidhi kwa Mungu wakisubiri siku ya kunyongwa.

Anasema tofauti na alivyokua amezoea kwa miaka mingi, alipoanza maisha ya kifungo cha maisha alikutana na suluba nyingi, hakuna wa kukuonea huruma.

Anasema pia wafungwa wao kwa wao hawana upendo ni wababe lakini pia wanakutana na kipigo kutoka kwa askari au wanyapara (viongozi wa wafungwa) .

Changamoto nyingine iliyompa muda kuzoea ni aina ya chakula ambacho kilikua ugali maharage kila siku tofauti na alipokuwa kwenye kifungo cha kunyongwa, huko walikua wakiletewa chakula kizuri, wanafuliwa nguo na kuoshewa vyombo.

Kwa uzoefu wake Kasambula anasema ipo haja kwa Serikali kuboresha maisha ya mfungwa wa maisha kwa kuwa anaishi muda mrefu gerezani hivyo ni vema akala na kupata matibabu mazuri kama haki ya msingi kwa mfungwa.

Anasema uamuzi wa Rais Magufuli kushauri wafungwa wafanye kazi ni mzuri na usiishie tu kwa wafungwa wa maisha bali hata wale wa kunyongwa kwa kuwa siku mfungwa wa kunyongwa anapobadilishiwa kifungo inakuwa ni mateso makubwa kumudu majukumu mapya.

“Anakuwa kama ameshalemaa unakuta mtu ana miaka 30 anaishi kula na kulala, leo akiambiwa alime hawezi tena kwa kuwa ameshalemaa ni vema wafanye kazi na si kula bure na kuingizia serikali hasara,”anasema.

Kasambula ambaye amekaa gerezani kwa zaidi ya mika 30 anasema vifungo vya muda mrefu havimfundishi mfungwa bali vinaisababishia Serikali hasara kwa kulisha watu bure.

Anasema ni bora mtu anapohukumiwa kunyongwa, akanyongwa kwa wakati badala ya kumuacha gerezani kwa zaidi ya miaka 30 huku akila bure na kupata huduma zote muhimu ikiwemo matibabu.

Anasema kwa mfungwa wa kifungo cha miaka mingi walau iwe miaka saba kwani kwa mafunzo yanayotolewa gerezani mtu asipobadilika ndani ya miaka mitano hatabadilika tena .

“Mimi nimeingia gerezani nikiwa na mika 28 nimetoka nikiwa na miaka 60 tayari nimezeeka sina faida yoyote kwa jamii lakini kama ningetoka nikiwa hata na miaka 40 lazima ningefanya kitu kwa faida yangu na nchi yangu,” anasema.

 

Maisha ya uraiani

Kasambula anasema baada ya kutoka gerezani ni kama amezaliwa upya kwani kila kitu ni kipya katika maisha yake.

Anasema aliiacha Geita ikiwa msitu kila eneo na sehemu ndogo ndio ilikua vijiji lakini amerudi na kukuta maendelo makubwa na tayari imetoka kuwa kijiji na kuwa mkoa.

Anasema maisha kwake yamekuwa magumu licha ya kurudi akiwa na ujuzi lakini hana vifaa wala mtaji hivyo kubaki kuwa ombaomba na kuiomba Serikali na wadau kumsaidia kuwa na vitendea kazi ili atumie ujuzi aliopata kuendeshea maisha.

Licha ya wazazi wake na yeye kuwa na mashamba kabla ya safari ya Singida lakini cha kusikitisha wamerudi na kukuta mashamba yao yote yameporwa na kila wakitafuta haki hawaipati.

Anasema kwa kuwa ametoka kifungoni hana uwezo wa kuweka mwanasheria kusimamia kesi na hivyo anaiomba Serikali kuingilia kati ili warudishiwe haki zao.

 

Familia

Kasambula anasema kabla ya kwenda gerezani alikua na watoto wanne na mke mmoja na mkewe alifariki mwaka 2002 muda mfupi baada ya yeye kubadilishiwa kifungo.

Anasema wakati wote akiwa gerezani familia haikumtenga na walikua wakimtembelea mara kwa mara na hata alipoachiwa huru mmoja wa watoto wake ndiye aliyempokea na kumrudisha nyumbani.

Anasema kutokana na umri hana mpango wa kuoa au kuongeza familia na anamshukuru Mungu licha ya kutowalea watoto wake lakini bado wanamthamini kama baba.

 

Kufungwa ndugu wanne wa familia moja

Si jambo la kawaida familia kuwa na watoto wanne wanaotumikia vifungo vya muda mrefu na kama ipo basi ni chache.

Kasambula anasema licha ya yeye na pacha wake kufungwa na kuhukumiwa kunyongwa lakini kaka yake mkubwa David Kasambula  na mdogo wake Bernadino Kasambula walifungwa miaka 30 kwa makosa mawili tofauti.

Bernadino anasema amekuwa mtu wa kufungwa mara kwa mara na tayari ameshafungwa zaidi ya mara nne kwa makosa tofauti

Akifafanua anasema ameanza kuingia gerezani tangu mwaka 1992 hadi mwaka 2015 akiwa na makosa tofauti na ametumikia vifungo katika magereza ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Anasema kukaa kwake gerezani imekua funzo na chuo cha ujuzi na sasa anaendesha maisha kwa ujuzi alioupata akiwa gerezani, amekuwa fundi viatu na pia anatengeneza viatu, lengo ni kuhakikisha Watanzania wanavaa viatu vyake kwa wingi.

Kwa sasa Bernadino anatengeneza viatu zaidi ya 50 kwa mwezi na kila kiatu huuza kati ya Sh8,000 hadi 12,000 na changamoto kubwa anayokutana nayo ni mtaji mdogo hivyo kushindwa kufikia malengo yake ya kuzalisha viatu zaidi ya 30 milioni.

 

Bernadino anasema licha ya kuwa mfungwa wa muda mrefu lakini bado ana ndoto za kuwa kocha bora wa mpira wa miguu kwani akiwa gerezani aliendelea kutumia kipawa chake cha kucheza soka na kufundisha wenzake.

 

 

Columnist: mwananchi.co.tz