Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

KALAMU HURU: Ya Chalamila na ‘Magufuli Ruling Party’

56253 Elius+Msuya

Wed, 8 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amesikika akieleza matamanio yake ya kuwapo kwa chama kimoja kinachoitwa Magufuli Ruling Party wakati wa ziara ya Rais John Magufuli mkoani humo.

Akifafanua kauli yake, Chalamila alisema kila mwezi Rais Magufuli amekuwa akiwasaidia kulipa malipo ya watumishi wilayani Kyela.

Hata hivyo, akijibu kauli hiyo, Rais Magufuli alisema licha ya matamanio hayo ya Chalamila, yeye angetamani kuwe na vyama vingi sana vitakavyoleta ushindani kwa sababu ni kwa mujibu wa katiba, lakini siku zote CCM ndiyo iwe inashinda.

Inawezekana Chalamila alitoa kauli hiyo kama mzaha, lakini kwa cheo chake inaweza kuwa imebeba ujumbe mzito nyuma yake. Kwamba Rais Magufuli anafanya kazi kubwa ambayo inampandisha daraja si tu la kuwa mwenyekiti wa CCM, bali pia awe na chama (au mwenyewe awe ndio chama)

Kauli kama hizi zimekuwa zikitolewa na baadhi ya viongozi na makada wa CCM, huku wengine wakitamani Rais Magufuli aongezewe muda wa kuwepo madarakani na wengine wakitamani hata uchaguzi wa mwaka 2020 usiwepo ili aendelee kutawala.

Ni dalili kwamba ama viongozi na makada hawa hawaisomi Katiba ya Jamhuri ya Muungano au wameamua kuipuuza makusudi. Katiba inasema Tanzania ni nchi inayofuata mfumo wa demokrasia ya vyama vingi.

Wakati kauli kama hii ikitolewa, tayari kuna vitendo vya kukandamiza upinzani, ikiwa pamoja na kuvinyima vyama fursa za kufanya mikutano na maandamano, mambo ambayo ni moja ya haki za kiraia na kikatiba za kukusanyika na kutoa maoni hadharani bila kuingiliwa.

Pamoja na kauli za Serikali kuwa mikutano inatakiwa ifanywe na wabunge na madiwani kwenye maeneo yao, lakini bado kuna maswali mengi, ikiwa pamoja na vyama visivyo na wabunge na madiwani na viongozi wa Serikali za mitaa vifanyeje mikutano ya hadhara?

Wanajiuliza, mbona viongozi wa CCM wanafanya mikutano hadi ya hadhara bila bughudha yoyote?

Kauli kama hizi haziishii tu kuathiri mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, bali pia vinaweza hata kuiathiri CCM yenyewe. Hivi Chalamila ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa CCM wa mkoa, anawezaje kuwaza kuwa na chama kingine pembeni zaidi ya chama chake?

Maana yake sasa Chalamila haoni umuhimu wa CCM. Anatamani kuwa chama kingine pembeni kitakachotimiza matamanio yake. Je, ni kwamba CCM haiwezi kutimiza ahadi zilizotolewa hadi kuwe na chama kingine?

Ni wakati sasa viongozi wa Serikali kutafakari wanapotoa kauli zao, wazilinganishe na matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayoongoza nchi.



Columnist: mwananchi.co.tz