Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

KALAMU HURU : Viongozi fuateni misingi ya utawala bora

38016 MUSA+JUMA KALAMU HURU : Viongozi fuateni misingi ya utawala bora

Wed, 23 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mataifa mengi barani Afrika yanakabiliwa na tatizo na ukosefu wa utawala bora hali ambayo imesababisha baadhi ya nchi kuingia katika migogoro ya kikatiba, vita vya wenyewe kwa wenyewe na migogoro ya aina mbalimbali.

Utawala bora ni matumizi ya mamlaka ambayo yanakuwa na uwazi, uwajibikaji, ushirikishaji wa watu, ufanisi, tija, uadilifu, usawa na kufuata utawala wa sheria.

Hivyo katika utekelezaji dhana ya utawala bora kuna mambo muhimu lazima yafuatwe ambayo ni matumizi mazuri ya madaraka, vyombo vya dola na rasilimali kwa faida ya wananchi walio wengi.

Mambo mengine muhimu katika dhana ya utawala bora ni viongozi kujua na kutambua madaraka waliyonayo, matumizi yake na mipaka iliyowekwa na katiba na sheria katika matumizi ya madaraka hayo.

Ikiwa Taifa linafuata misingi ya utawala bora kuna faida kubwa ambazo zinapatikana ambazo ni pamoja na matumizi mazuri ya rasilimali za nchi, kuwa na maendeleo endelevu, kupungua kwa umasikini, kuondoa ujinga na maradhi na kutokomeza rushwa. Pia huduma za jamii huwa bora na hali ya amani na utulivu hujitokeza na migogoro kutatuliwa kwa mujibu wa sheria.

Pia kama kuna utawala bora wananchi hupata taarifa za utekelezaji wa mipango na bajeti pia hupewa taarifa za mapato na matumizi katika maeneo yao.

Hivyo misingi hii ya utawala bora inawalazimu, viongozi katika kada na nafasi mbalimbali kujua uwajibikaji na kuwa tayari kujibu, kubeba dhamana na kutoa maelezo kwa wananchi juu ya maamuzi katika kutekeleza dhamana aliyopewa.

Ndio sababu Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 inaeleza wazi kuwa Kwa mujibu wa Ibara ya 8 (1) (c), Serikali itawajibika kwa wananchi.

Katika siku za karibuni, kumeanza kuibuka matukio ya baadhi ya viongozi au watendaji wa taasisi za umma na binafsi kutoheshimu misingi ya utawala bora katika sehemu wanazoongoza.

Bado tuna viongozi ambao hawaamini kuwa wanapaswa kutumikia wananchi badala ya maslahi yao. Wengine hawataki kuwajibika pale taasisi wanazoziongoza zinapokuwa na matatizo.

Hivi sasa migogoro inaongezeka katika mihimili ya utawala, nikimaanisha Bunge, Mahakama na Serikali. Tumesikia mgogoro baina ya Bunge na chombo muhimu kama ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Vilevile tumeanza kusikia migogoro baina ya mahakama na serikali, hasa pale ambapo mahakama inatoa maamuzi lakini serikali haitekelezi, hivyo kuonekana kuna muhimili mmoja unaufanya mwingine dhaifu, hii si misingi ya utawala bora.

Hivyo, kila kiongozi akiheshimu katiba ya nchi licha ya mapungufu yaliyopo, watu wengi watabaki salama na kuishi maisha bora. Kuheshimu sheria na taratibu mlizojiwekea ni jambo muhimu, hata katika ngazi ya familia, baba akiwa aheshimu haki za watoto na mama yao, ni wazi nyuma hiyo haitakuwa salama.

Kufuata misingi ya utawala bora ni jambo ambalo halikwepeki na kwa viongozi wa umma, ni muhimu zaidi kwa kuwa wao wamepewa dhamana kubwa ya kuongoza wananchi.

Mussa Juma ni mwandishi wa Mwananchi mkoa wa Arusha.



Columnist: mwananchi.co.tz