Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

KALAMU HURU: Kuna dalili ya kuhujumu ripoti ya CAG

54927 Elius+Msuya

Wed, 1 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ilianza mwishoni mwa mwaka jana Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai alipotangaza kumwita Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kujieleza kutokana na kauli alizotoa akiwa nchini Marekani ambazo zilidaiwa kulidhalilisha Bunge.

Profesa Assad akiwa Marekani alikaririwa akisema Bunge ni dhaifu kwa kushindwa kuisimamia Serikali, kauli ambayo ilichukuliwa kama dharau kwa mhimili huo.

Hata baada ya kuitwa kwenye kamati hiyo, Profesa Assad alisisitiza kuwa kauli hiyo ni ya kihasibu na hakukosea kuitoa. Kutokana na msimamo huo, Bunge lilipitisha azimio la kutofanya naye kazi. Hapo ndipo utata ulipoanzia.

Ndugai amekuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa Bunge halifanyi kazi na Profesa Assad lakini litanya kazi na ofisi ya CAG, kwa maana kwamba kosa ni la mtu, si ofisi.

Lakini, ripoti ya CAG iliyowasilishwa bungeni imeandaliwa na kutiwa saini na Profesa Assad, vipi Bunge litajiepusha naye?

Kama hiyo haitoshi, Ndugai ameonyesha kutofurahishwa na tabia ya wabunge kurejea ripoti hiyo kabla haijajadiliwa na kamati akimtaja mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe.

Ndugai alisema ripoti hiyo si mwisho, kwani kuna uchambuzi utakaofanywa kwenye kamati za Bunge (PAC na LAAC).

Tumemsikia pia Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola akisema bungeni hakuna mtu mwongo kama CAG. Lugola alikuwa akirejea utata wa ununuzi wa sare za polisi ambao ripoti hiyo inasema jeshi hilo limetumia Sh16.66 bilioni kuzinunua bila kuwa na ushahidi wowote.

Halafu waziri ana maana gani anaposema CAG ni mwongo? Je, ni Profesa Assad au ni ofisi yake? Hata hivyo, ni vigumu kumtenga Profesa Assad na ofisi yake maana hata ukaguzi wote unaratibiwa naye na yeye ndiye anaikabidhi ripoti kwa Rais kabla ya kupelekwa bungeni.

Kauli hizi za kutofanya kazi na CAG au kumwita mwongo au kuibeza ripoti yake zinaweza kuchukuliwa kama njia mojawapo za kuzorotesha kazi za ukaguzi zinazotambuliwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Katiba ndiyo inampa mamlaka CAG kufanya kazi zake na jinsi anavyopatikana na jinsi anavyoondolewa na jinsi ya kuchukua hatua za kisheria kupitia mahakama kama mtu hajaridhishwa na ukaguzi.

Maadamu Bunge limeshasema linafanya kazi na ofisi ya CAG, basi wabunge waachwe waitumie ripoti hiyo kwa uhuru na huko ndiko kuisimamia Serikali. Kama kuna jambo la uongo, maofisa masuhuli wa Serikali watakwenda kufafanua kwenye kamati.

Ripoti hiyo itumike kama nyenzo ya Bunge kuisimamia Serikali kuhakikisha fedha za umma zinatumika ipasavyo.



Columnist: mwananchi.co.tz