Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

KALAMU HURU: Kiongozi mwenye digrii nne anakosolewa na nani?

85195 Elius+Msuya KALAMU HURU: Kiongozi mwenye digrii nne anakosolewa na nani?

Fri, 22 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katiba ya Tanzania ibara ya 8 (1) inaitambulisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii, na kuwa wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi.

Vifungu hivyo vinaonyesha kuwa Tanzania inafuata mfumo wa utawala (uongozi) ambao wananchi ndiyo chanzo cha mawazo ya viongozi. Inapofika mahali viongozi wakaonekana hawahitaji mawazo ya wananchi inatia shaka iwapo hiyo Katiba wanaifuata.

Mbaya zaidi, wasiwasi unakuwa pale unapokuta wananchi wenyewe hawai]jui nguvu walizopewa na Katiba.

Kauli karibuni ya Dk Harrison Mwakyembe, waziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo, kuhusu elimu yake imeibua mjadala mzito miongoni mwa Watanzania, hasa katika mitandao ya kijamii.

Dk Mwakyembe aliyekuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wake na wasanii jijini Dar es Salaam, aliwashangaa wasanii wanaoimba nyimbo za kisiasa akisema kuwa hazilipi.

Lakini kwa kauli yake hiyo alionyesha kulenga zaidi wasanii wanaoikosoa Serikali, akihoji kwamba mtu wenye elimu ya darasa la saba anawezaje kumkosoa yeye msomi mwenye shahada nne.

Mjadala umekuwa mkubwa kwa sababu watu waichukulia kauli hiyo kama kejeli kwa wananchi. Kwamba sasa wananchi hawawezi kumshauri mtu mwenye shahada nne, Au tuseme viongozi wetu sasa hawawezi kushauriwa na wananchi wenye elimu ya chini? Kwamba wao ndiyo wanaojua kila kitu?

Huyu si wa kwanza kutoa kauli kama hiyo na imeshakuwa kawaida sasa kuona viongozi na hasa mawaziri wakijitapa kutokana na elimu zao, wakijisifia kutokana na nafasi walizonazo. Wanasahau kuwa hata ubunge uliowapa uwaziri umetokana na wananchi.

Kuna kila dalili kwamba madaraka ya wananchi kwa mujibu wa Katiba yanakanyagwa na wananchi hawana jinsi ya kuyachukua.

Viongozi wanapora madaraka ya wananchi kwa kisingizio cha kulinda amani na watu wanaojaribu kuhoji wanatishwa kuwa wanataka kuvunja amani.

Imefika mahali sasa viongozi wanaona wananchi hawana haki ya kukosoa Serikali, maana hawana elimu kama ya viongozi.

Wanachokitaka wao ni kupongezwa tu. Hawataki kusikia mawazo mbadala.

Hii dalili ya ulevi wa madaraka na jeuri hii wanaipata kwa sababu ya kujilimbikizia madaraka. Wao ndiyo wameshikilia mifumo ya uchaguzi na vyombo vya ulinzi na usalama na vyombo vinavyosimamia uchaguzi.

Sina maana kwamba viongozi hawatakiwi kusoma hadi digrii nyingi au wananchi wanatakiwa kuwakosoa bila sababu, hapana. Bali ninachotaka kusema ni kuwa madaraka ya wananchi kwa mujibu wa Katiba lazima yaonekane na yaheshimiwe.

Columnist: mwananchi.co.tz