Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

KAKAKUONA : Viwanda 4,700 sawa, tunawalindaje wawekezaji?

48954 PIC+Viwanda

Wed, 27 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Siku chache zilizopita, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo alisema hadi kufikia Desemba 2018, zaidi ya viwanda 4,700 vilikuwa vimejengwa ndani ya miaka mitatu.

Viwanda hivi ni vile ambavyo vilitokana na agizo la Serikali kuwa katika kila mkoa ujenge viwanda si chini ya 100, ili kufikia malengo ya kuifanya Tanzania iwe na uchumi wa kati ifikapo 2020. Hivi ni sawa na asilimia 183.73 ya lengo la kujenga viwanda 2,600 vilijengwa nchini.

Kwa mujibu wa Jafo, viwanda vikubwa vilikuwa 108, viwanda vya kati 236, vidogo 2,422 na vidogo kabisa 2,010, ambavyo kwa ujumla wake vimetoa ajira 36,796 kwa Watanzania.

Nimeona baadhi ya Watanzania kwenye mitandao ya kijamii wakibeza takwimu hizo, lakini hizi ndizo takwimu rasmi za idadi ya viwanda. Mimi sitaki kuingia kwa undani aina ya viwanda vilivyojengwa, ila kwa mafanikio hayo Serikali inastahili pongezi.

Lakini pamoja na pongezi hizo, iko swali la msingi hapa, Je, tunawalindaje wawekezaji wa ndani na nje ya nchi? tunawajengea mazingira gani mazuri ya kuwafanya waione Tanzania kama sehemu salama?

Hoja yangu ni kuwa tunavilindaje viwanda hivi na vilivyokuwepo awali kwa sababu ipo mifano ya wawekezaji kuanza kukata tamaa, kutokana na kutendewa isivyo na mamlaka za Serikali.

Nitatolea mfano wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), ambayo imejenga kiwanda kikubwa mjini Moshi, na ni moja ya viwanda vikubwa vitatu vya walipa kodi wakubwa.

Licha ya kupewa eneo la Pasua Block JJJ na Serikali yenyewe la kujenga kiwanda hicho, umejitokeza mgogoro mkubwa kati yake na Shirika la Reli Tanzania (TRC), ikidai eneo kilipo kiwanda ni lake.

Kwa uhalisia wa mgogoro huu, wala haukupaswa kuwa kati ya TRC na SBL bali TRC na Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, ambayo ndiyo mamlaka halali ya ugawaji ardhi kwa mujibu wa sheria.

Hebu tujiulize, mathalani Halmashauri ya Manispaa ya Moshi ingekuwa imegawa eneo hilo mara mbili, tunamvunjia nyumba mtu ambaye tayari amejenga au tunamtafutia eneo lingine?

Bahati nzuri Kamati ya Bunge ilitembelea eneo hilo wiki mbili zilizopita na kupewa taarifa kamili kwamba SBL wanamiliki eneo hilo kwa mujibu wa sheria, wanalipa kodi na wana nyaraka zote.

Nimpongeze Waziri wa Ardhi, William Lukuvi, Mkuu wa mkoa Kilimanjaro, Anna Mghwira na Mkuu wa wilaya ya Moshi, Kippi Warioba kwa namna wanavyoutafutia suluhu mgogoro huu. Nimeambiwa, na sina sababu ya kutoamini, kwamba hata Mkurugenzi mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa naye anatamani mgogoro huu umalizike, na ikumbukwe unahusisha pia wananchi 800.

Kamati ya Bunge imeamua kuuchukua mgogoro huu, na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Stella Manyanya, ameahidi kuwa Serikali itatumia busara kubwa kumaliza mgogoro huo kwa njia ya amani.

Ni kweli, hiyo ndio njia itarejesha imani ya wawekezaji wa ndani na wa Uingereza, ambao hawaelewi wamekosea wapi wakati ardhi wamepewa na Serikali, halafu leo wanatakiwa kubomoa bila fidia.



Columnist: mwananchi.co.tz