Tangu aingie madarakani, Rais John Magufuli amekuwa kwa namna moja au nyingine akionyesha ukali dhidi ya ufisadi. Watu wengi wametumbuliwa kwenye nafasi zako, wengine wamefikishwa mahakamani na hatua nyingine mbalimbali zimechukuliwa lakini ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), imeendelea kuonyesha uwepo wa mchwa.
Rais ameteua na kutengua teuzi za watendaji mbalimbali pale aliponusa harufu ya ufisadi na pengine hata kupata uthibitisho, lakini hakusita na hasiti kuwajibisha mtu anayejihusisha na ufisadi.
Watumishi kibao wa umma wako mahakamani hivi sasa wakipambana na kesi zao za ufisadi na wapo wafanyabiashara wakubwa kwa wadogo nao wako kortini kwa tuhuma za vitendo vya ufisadi.
Lakini ripoti ya CAG kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2018 bado imefichua ufisadi wa kutisha, ubadhirifu, ukiukwaji wa taratibu za fedha na utendaji mbovu umeendelea kutamalaki, kulikoni?
Kwa ripoti hii, inaonekana kama Rais anapigana vita mwenyewe. Mbona katika mikutano yake ya hadhara analalamika kana kwamba hana wasaidizi wa kumsaidia kupambana na ufisadi?
Ndio maana nimelazimika kuuliza, kwa ukali huu wa Rais Magufuli bado kuna watu hawajasoma alama za nyakati na wanaendelea kupiga dili? Kama hawamuogopi Rais watamuogopa nani, au kuna kitu kingine zaidi ya tunachokiona?
Related Content
- Kauli ya Bashiru inamulika haki ya kufanya siasa
- HOJA ZA KARUGENDO: Kumbuka, tanguliza ubinadamu-Somo kutoka nchini Rwanda
- Nani anafuata Afrika baada ya Mugabe, Bashir na Bouteflika?
- MAKALA YA MALOTO: Ripoti CAG: Wapo wanaotamani sheria za fedha zisiwepo
Kabla ya Magufuli hajashika madaraka, ufisadi ulitamalakini na ndiyo maana katika ilani ya uchaguzi ya CCM (2015-2020), chama hicho kilikuja na uanzishaji mahakama ya mafisadi.
Takwimu za Taasisi ya Global Financial Integrity (GFI), zilionyesha kuwa kati ya 2002 na 2011 kiasi cha Dola 4.5 bilioni za Marekani sawa na Sh7.3 trilioni zilitoroshwa hapa nchini kwenda nje. Katika ripoti hiyo mwaka 2010 pekee Sh2.1 trilioni zilitajwa kutoroshwa na mwaka 2011 Sh1.3 trilioni zilitoroshwa.
Ripoti nyingine kama ya Kar and Cartwright-Smith (2008), kuanzia mwaka 1970 hadi mwaka 2004 ilionyesha Sh10.4 trilioni zilitoroshwa kwenda nje ya nchi.
Ukwepaji wa kodi, misamaha ya kodi isiyo na tija na kashfa kubwa ziliendelea kutikisia nchi katika awamu ya tatu na nne. Tukajua alipoingia Rais Magufuli na Serikali yake haya yangekoma kama alivyokuwa anasema kila wakati.
Lakini ripoti ya CAG ambayo ndio jicho la Watanzania, imefichua madudu kama yaleyale ya awamu zilizopita, tena yakiwa na kiwango kikubwa zaidi. Rais analalamika, CAG analalamika, wananchi tunalalamika. Tunakosea wapi?
Kama ukali wa Rais haujasaidia, wasaidizi wake anaowateua hawamsaidii, mapendekezo ya CAG hayafanyiwi kazi, basi tuunde Tume ya Maridhiano ili kila aliye fisadi aje atubu na tumsamehe.
Baada ya hapo tuimarishe mifumo yetu ya utendaji badala ya kuacha liwe jeshi la mtu mmoja (Rais) katika mapambano dhidi ya ufisadi. Tukiendelea hivi haya ya CAG tutayasikia kila siku.
Badala ya kumwambia CAG Profesa Mussa Assad ajiuzulu kwa kutamka bunge ni dhaifu, tushirikiane naye kujua udhaifu ulipo na tuurekebishe na Bunge litimize wajibu wake wa kuisimamia Serikali badala ya kuendelea kuonyesha uimara wake kwa maneno.