Ana bahati. Ndiyo ni sahihi kusema hivyo kuhusu Jokate Mwegelo. Kitu ambacho anajitofautisha na wengine ni kupanga nyumba. Jojo hajawahi kujitegemea kimaisha kama wenzake mpaka utu uzima wake huu.
Mengine yote yamefanywa zaidi yake na wengine ambao wangeweza kupata nafasi aliyonayo hivi sasa. Elimu, umaarufu, kujuana na watu na kukipenda chama. Ana bahati sana Jojo ndo ukweli.
Pamoja na bahati lakini anastahili. Vyovyote iwavyo ana tofauti kubwa na wasanii wengi. Hata kama samaki mmoja akioza wote wameoza kuna mmoja atakuwa na nafuu kwa kitoweo. Jokate anastahili na Mungu ampe nguvu.
Somo kwa wasanii wasio angalia kesho yao. Wanaogeuza ngozi zao kama kuta za gereza kwa maandishi (tattoo). Wanaobeba ya vyumbani na guest na kutundika mitandaoni. Mtaongoza watu ‘lokesheni’ siyo Kisarawe. Nani awateue?
Ifike wakati wasanii waishi maisha halisi badala ya ‘kufeki’ sana. Matokeo yake wanaanza kuonyesha uhalisi wanapokwama kwa magonjwa au misiba.
Hiki ndicho kiliwaponza mpaka kwenye soko lao la filamu.
Kuuaminisha umma kuwa wao ni matawi ya juu. Wao wanapata pesa nyingi na kumiliki mali na magari ya kifahari wakati ndivyo sivyo. Hili ni kosa kubwa kwa sanaa yao ingawa wengi hawajui na hawajui kuwa hawajui kama ni kosa.
Unaweza kujikweza kama kuna ukweli ndani yake. Lakini unajikweza wakati siyo kweli au unaruhusu watu wakupandishe juu bila kukushikilia lazima uanguke. Ugonjwa wa kujikweza umejenga undugu na wasanii.
Kwa mfano mfumo wa kodi za TRA ni chanzo cha mauti ya soko lenyewe. Hii ni kwa sababu soko la filamu halikuwa kubwa kihivyo kama ambavyo ilionekana kwa watu kutokana na majigambo ya wasanii wenyewe.
Msanii anajitapa kuwa ana nyumba ya Sh400 milioni. Na akiaminisha umma kuwa chanzo chake cha kipato ni filamu. Unategemea watu walionaje soko la filamu? Hapa huwezi kuwalaumu TRA kwa mfumo huo wa kodi. Hawakupata taarifa sahihi juu ya biashara husika, hata hao wasanii wenyewe hawana hizo taarifa. Walikwenda tu na upepo unavyokwenda.
Taarifa sahihi zilikuwa kwa msambazaji na familia yake. Wao ndio wamiliki wa filamu zote, wasanii na watengezaji walikuwa waajiriwa kama waajiriwa wengine. Kwenye hili hawakuwa wazi wasanii wote.
Ndio maana hakuna msanii anayemiliki filamu yake. Hadi leo hii mifupa yake ikiwa imelala pale Kinondoni, Kanumba hakuwa na filamu anayoimiliki amekwenda na kila kitu chake na kubaki jina tu.
Ukweli biashara ya filamu ilikuwa ndio kwanza inachanua, kuitoza kodi kwa mfumo huu ilitosha kuifanya itoweke kama homa ya manjano au kifadulo. Hiki kilikuwa kirusi kikubwa sana.
Mbali na hilo ni wasanii wachache sana kuliko ndevu za AY, waliolipwa vizuri na msambazaji, Sh20 milioni kwa
filamu (part 1 & 2 = Sh40 milioni). Wengine waliambulia kama milioni kumi kwa kila filamu (part 1& 2 ).
Wengine walilipwa hadi Sh3.5 milioni kwa kila filamu. Ukichanganya gharama za kutengeneza, faida zao zilikuwa kati ya Sh 1 hadi Sh10 milioni tu. Lakini mitaani walikuwa na sura za milioni 200 kwenda juu.
Mfumo wenyewe ni utozaji kodi kwa stika, mfanyabiashara analipia kodi kwa nakala elfu tano siyo chini ya hapo kabla hajaiingiza kazi sokoni, bila kujua soko likoje. Kama ana wateja elfu mbili au elfu moja tu. Atajua mwenyewe.
Mfumo ukafanya wasambazaji wasite kuingiza filamu nyingi sokoni, kwa sababu hawakujua mwenendo wa biashara utakuwaje. Na malipo kwa wasanii yakaporomoka ghafla ‘automatikale’.
Kuporomoka kwa malipo kukazalisha filamu mbovu za ujanja ujanja, wakikusanywa wasio na uwezo, na mastaa wakichezeshwa sehemu ndogo kwa malipo kidogo ili picha zao zitumike kwenye kasha tu na kuingiza sokoni.
Ndo mwanzo wa filamu laghai, walitumia akili nyingi kutengeneza makasha ya uongo ili wauze na kukwepa gharama kubwa. Watu nao utawadanganya mara moja siyo kila siku. Uhuni huu ukachokwa machoni kwa wateja wa filamu na kujikita kwa Wakorea.
Filamu zinapitia mabadiliko ya soko kuendana na wakati. Marekani walibadilika kitambo. Hawapo kwenye CD & DVD, wapo kwenye majumba ya sinema na mitandaoni (online).
Huku kwetu hawakujiandaa kwa mabadiliko yoyote ya kibiashara baada ya soko la CD & DVD kuporomoka, kwa kuwa tasnia ilikuwa bado changa. Mabadiliko ua wenzetu yalikuwa maili nyingi mbele yetu.
Badala ya maandamano ya kupinga uwepo sokoni kwa filamu za nje, ilipaswa kubadilika na mfumo wa kimauzo, kwenda kwenye majumba ya filamu na watu wafurike kutazama.
Hakuna wawekezaji wa kutosha, wenye mitaji mikubwa na ufahamu wa soko waliotaka kufanya mabadiliko na matokeo yake biashara ikadoda na filamu kuporomoka kabisa.
Leo hii filamu nyingi zinaoneshwa runingani. Hii imechangia pia kuporomoka kwa soko, wateja wanafuatwa majumbani na filamu hizo kupitia runinga.
Maumivu yamekuwa kwenye filamu za Kitanzania. Hakuna tofauti ya mwaka juzi na filamu ya mwaka huu. Visa na mikasa kufanana na wateja nao wanaona bora kutazama bure kabisa runingani.
Kichekesho ni kwamba malipo ya kuoneshwa runingani yanakwenda kwa wamiliki wa filamu na siyo wasanii, hapa msanii hanufaiki kwa lolote zaidi ya kuua soko lake.
Pia hawana jipya kwa filamu moja hadi
nyingine. Mbinu zilezile, maneno yaleyale na mikasa ni ileile. Makosa yanajirudia kwa kukosa muda wa kupitia makosa ya filamu zilizotangulia.
Watengenezaji hawana ujuzi na mpango wa kutoa mafunzo hakuna kabisa. Mashabiki wa kwenye majumba ya sinema wengi wana uzoefu wa filamu bora, hawana muda na filamu mbovu.
Mfumo huo mbovu wa kodi hawakupanga TRA peke yao. Wadau ambao ndo wasanii wenyewe walihusika. Ile hali ya kuonekana wao wana pesa nyingi walishindwa kuwa wakweli kwenye ugumu wa soko lao.
Wakawaaminisha mabosi wa TRA kuwa soko la filamu ni kubwa. Huku wao wasanii wakiamini uwepo wa stika kwenye makasha utasaidia kuua biashara haramu. Hili la idadi ya nakala za kulipia kodi kabla ya kuingiza sokoni wakilipuuza.
Ni kwa nini nakala elfu tano lazima zilipiwe kodi kabla ya filamu kuingia sokoni? Ni kwa sababu stika zinatengenezwa Uingereza kwa gharama kubwa. Chini ya nakala hizo haiwezekani ni gharama kubwa zaidi.
Na stika zinaagizwa baada ya msanii kutoa ‘oda’. Filamu zetu zilikuwa bado kuingia kwenye mfumo huo kwa sababu soko lao lilikuwa bado. Kjikweza mpaka kwenye vitu vya msingi kwa maisha yao kumewaponza.
Mfano halisi ni lundo la wasanii kukimbilia siasa. Mtazamo wa nje juu ya kipato chao mtu lazima ashangae furaha ya Jojo na wapambe wake. Anaachaje utajiri mkubwa kwenye sanaa na kwenda kujichosha na matatizo ya wana Kisarawe?
Soko la sanaa siyo kihivyo. Filamu mbili za mwisho za marehemu Kanumba ziliuzwa bila familia kupata senti. Yalikuwa malipo ya deni alilokuwa anadaiwa na wasambazaji wa filamu zake. Lakini amefariki akiaminika kama msanii tajiri sana.
Jojo pambana na hali yako na kumtanguliza Mungu. Huo ndo mtoko. Ukileta ‘swaga’ za Bongo Movie na mbwembwe za insta, utatukuta kitaa na kina Wema tunaulizia codes na location za kula bata.