Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Jasusi CIA atinga Zanzibar kama ofisa ubalozi -5

52206 Pic+jasusi

Mon, 15 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katika toleo lililopita tuliona jinsi CIA ilivyomuona mwanasiasa machachari wa Zanzibar, Abdulrahman Mohamed Babu, kama tishio la usalama wa maslahi yao visiwani Zanzibar na hivyo wakatafuta mbinu za kumuangamiza. Leo tunaona jinsi hofu dhidi ya ukomunisti ilivyoifanya Marekani ifikirie mkakati mpya wa Zanzibar na kumtuma jasusi wake kama ofisa ubalozi ili kusukuma mambo. Sasa endelea...

Katika ujumbe ambao Balozi wa Marekani nchini Tanganyika, William Leonhart alimtumia Waziri wa Mambo ya Nje, Dean Rusk alieleza kuhusu kutowezekana kwa Zanzibar na Tanganyika kuungana.

“Si sisi wala Waingereza ambao wanaamini kwamba Muungano wa Tanganyika-Zanzibar unawezekana,” alisema katika ujumbe huo.

Hiyo inaonyesha hata Wamarekani na Waingereza hawakuamini kwamba muungano ungewezekana, lakini walisukumwa kuuchochea uwezekane kutokana na ile hofu ya ukomunisti kukomaa visiwa vya Zanzibar na kuathiri maslahi ya nchi za Magharibi.

Wakati huo, ubalozi wa Marekani mjini Nairobi ukiwa chini ya William Attwood ambaye ni mwandishi wa kitabu cha The Reds and the Blacks ulikuwa ukiandaa mipango mingine kwa Zanzibar endapo muungano ungeshindikana.

Attwood, jasusi mwingine wa Marekani chini ya mwavuli wa ubalozi aliandika katika kitabu chake The Reds and the Blacks: A Personal Adventure, kuwa “nchi za Magharibi ndizo zilizowasukuma marais wa Afrika Mashariki kufanya kila waliloweza kuivuta Zanzibar katika familia (ya Afrika Mashariki)”.

Lakini “kwa sababu za kihistoria na za kitamaduni, Tanganyika ilipendekezwa kuwa mteule halali wa kuungana na Zanzibar”.

Kwa mujibu wa jarida la Africa Now, Waingereza na hasa Wamarekani walikuwa wametengeneza mpango waliouita Zanzibar Action Plan (ZAP), ambao ungehusisha uvamizi wa kijeshi katika visiwa hivyo kama muungano ungeshindikana. Kabla mpango huo haujamalizika, Attwood aliomba kuonana na Rais Jomo Kenyatta na alipokubaliwa, aliendesha gari mwenyewe hadi Ikulu. Mazungumzo baina yao hayakuripotiwa na vyombo vya habari, lakini baadaye jioni siku hiyo, Attwood alituma ujumbe wa telegram.

“Kenyatta ameonyesha ishara ya kukubali mpango wa uvamizi wa kijeshi wa Uingereza (ambao ungefanywa Zanzibar). Yamkini Nyerere na Obote watakubali pia. (Kenyatta) Amethibitisha uamuzi wake wa kukutana na Nyerere, Obote na Karume ndani ya siku chache zijazo kuijadili Zanzibar,” unaeleza ujumbe huo.

Kwa mujibu wa kitabu Foreign Relations of the United States 1964-1968: Congo, 1960-1968, Attwood ndiye aliyempa Kenyatta wazo la kuitisha mkutano wa Shirikisho la Afrika Mashariki, na katika mkutano huo Karume alialikwa pia.

Wakati wote huo ubalozi wa Marekani visiwani Zanzibar ulikuwa chini ya Mmarekani Frank Charles Carlucci III, ambaye alikuwa akitazama kila hatua ya kisiasa ilivyokuwa ikienda na waliokuwa wakiendesha—hasa Abdulrahman Babu.

Huyu alikuwa jasusi makini, pengine kuliko Leonhart wa Dar es Salaam na Attwood wa Nairobi.

Carlucci alitakiwa kuhakikisha kuwa wakomunisti wote wanakosa nguvu kisiasa au wanaondolewa kabisa Zanzibar. Aliingia Zanzibar akitokea Zaire (sasa Congo) ambako hali yake ya kisiasa ilikuwa imechafuka.

Aliingia Zanzibar wakati kukiwa na tuhuma kuwa Marekani, Ubelgiji na Uingereza zilihusika katika mauaji ya waziri mkuu wa kwanza wa Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo), Patrice Lumumba.

Katikati ya tuhuma hizo, Carlucci alikuwa ameingia Zanzibar kutimiza kile alichotumwa na Marekani na akawa ofisa wa ubalozi, lakini inasadikiwa kuwa alikuwa akifanya kazi ya kijasusi.

Akiwa Zanzibar, Carlucci alijenga na kuimarisha njia nyingi za mawasiliano—hiyo ikiwa ni pamoja na kuwa na watu wengi aliokuwa akiwahoji kupata taarifa. Inaelezwa kuwa mara kwa mara alikuwa akitazamana kwa jicho baya na baadhi ya viongozi wa Serikali ya Mapinduzi.

Siku moja, akijibu kauli za katibu wa Jumuiya ya Madola wa wakati huo, Duncan Sandys, ambaye alizuru Afrika Mashariki kwa muda mfupi, Frank Carlucci alisema:

“Inakubalika kwamba Serikali ya Zanzibar haina nguvu, hasa inapopimwa kwa viwango vyetu (Wamarekani). Hata hivyo, kama ilivyo kwa Sandys, huenda nimevutiwa na GOZ kuliko nilivyotazamiwa na ilivyotazamiwa na wengine … watu wenye siasa za wastani na wale wenye siasa kali wameelimika vizuri na wamefunzwa kuliko Waafrika wengine niliofanya nao kazi.”

Jumamosi, Machi 14, 1964, Rusk alituma ujumbe mwingine wa telegram uliosisitizia wazo la awali la kuwatumia Kenyatta na Obote, lakini pia ukasisitiza kwamba Marekani iepuke kuwasiliana moja kwa moja na Nyerere kuhusu Zanzibar, badala yake wamwachie Kenyatta. Walijaribu kumtumia Kenyatta kuwasiliana na Nyerere kumweleza utashi wao.

“Idara (pengine akimaanisha CIA) ingetaka kupata maoni ya Balozi Leonhart ikiwa (Oscar) Kambona anaweza kufanya kazi hii muhimu na kama anaweza kuanzisha mazungumzo naye (Nyerere).”

Frank Charles Carlucci, ambaye alikuwa ofisa wa ubalozi wa Marekani visiwani Zanzibar, alitimuliwa Januari 1965 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kutangazwa kuwa ni mhamiaji asiyetakiwa (persona non grata).

Hata hivyo, katika miaka ya sabini, Rais Jimmy Carter alimteua Carlucci kuwa naibu wa mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), na katika utawala wa Ronald Reagan akapewa cheo cha kuongoza Idara ya Ulinzi ya Marekani.

Itaendelea kesho



Columnist: mwananchi.co.tz