Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Jafo umesikika, ma-DC waache kutafuta kiki

13220 Daniel MjemaTanzaniaWeb

Thu, 23 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, tumeshuhudia baadhi ya wakuu wa wilaya (ma-DC), wakitoa amri za watu kuwekwa mahabusu kwa saa 48 hata katika mambo yasiyo ya jinai.

Lakini wiki iliyopita, nilifarijika sana nilipomsikia Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleiman Jafo, alipowapa somo na kuwarudisha katika msitari.

Japokuwa somo hili la Jafo limechelewa wakati matukio hayo yameshachochea chuki dhidi ya Serikali, angalau kwa kauli hiyo Serikali imejitenga na matendo ya viongozi hao wanaotumia vibaya sheria na madaraka yao.

Kabla sijaendelea na hoja yangu hii, ningependa niwarejeshe katika kile ambacho Waziri Jafo aliwaeleza wakuu wa wilaya walioteuliwa na Rais John Magufuli, Julai 28, 2018.

Nanukuu, “Kumetokea tabia. DC anaona kiki kubwa sana kuwaweka ndani watu saa 48. Kuwaweka watu ndani kunaisababisha watu waanze kuichukia Serikali kwa sababu ya kutia tia watu ndani bila sababu.

“Inatakiwa pale ambapo kuna jinai inatakiwa itendeke machoni mwa DC. Kwa kuzuia hilo jambo lisifanyike ndio mkuu wa wilaya atatumia sheria hii.

“Sasa wewe uko nyumbani umesikia jambo linatokea kwa mazingira tofauti anaagiza huyo tia ndani. Chuki nyingine zisizokuwa na maana tia ndani. Tunasababisha watu kuichukia Serikali yao…”.

Ni kutokana na kauli hii, ndio maana nimetangulia kumpongeza Waziri Jafo kwa kukemea tabia hii, japo inawezekana, wapo ma-DC vichwa ngumu wataendelea kutafuta kiki kwa kuweka watu mahabusu.

Bahati mbaya sana, baadhi ya ma-DC inaonekana hawajaipitia vyema sheria hiyo ya mwaka 1997 kifungu cha 15(1-9) na hawajui kama watakapoitumia vibaya wanaweza kuadhibiwa.

Kifungu cha 1 kinasema DC anaweza kuagiza kukamatwa kwa mtu yeyote aliye mbele yake, aliyetenda kosa au anafahamu ametenda kosa ambalo kisheria anaweza kukamatwa na kushtakiwa.

Ukienda kifungu cha pili kinasema pale ambapo DC ana sababu za kuamini kuna mtu anavunja amani au kuvuruga mshikamano wa wananchi, atamuagiza afisa wa polisi kumweka mtu huyo mahabusu.

Lakini, kifungu cha 3 cha sheria hiyo kinasema wazi kuwa mtu huyo atawekwa mahabusu kwa muda usiozidi saa 48, na baada ya muda huo ni lazima apepekwe mahakamani na kushtakiwa kwa jinai.

Kwa bahati mbaya, wateule hawa hawajui kifungu kidogo cha 9 cha sheria hiyohiyo, kimetoa fursa kwa DC aliyetumia vibaya madaraka yake, kuadhibiwa chini kifungu cha 96 cha kanuni ya adhabu kama kilivyofanyia marejeo mwaka 2002.

Wakuu wa wilaya wanapaswa kuelimishwa kuwa hawako juu ya sheria kwa kuamuru watu wawekwe ndani pengine hata kwa kupishana tu kauli au kumkomoa kwa sababu za kisiasa.

Kuna mwalimu huko wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, aliwekwa mahabusu kwa amri ya DC kwa sababu tu ameshindwa kutaja jina la DC. Unajiuliza kosa la jinai liko wapo hapo? Kiki za kisiasa.

Wapo viongozi wa kisiasa wakiwamo wabunge, madiwani, wenyeviti wa vijiji, vitongoji au mitaa, wamewekwa mahabusu kwa saa 48 amri za ma-DC, lakini baadaye hawakufunguliwa mashtaka, maana yake hawakuwa na makosa.

Ni lazima kabla DC hajaamuru mtu kuwekwa mahabusu ajiulize, ametenda kosa gani la jinai? Kama linahusu nidhamu ya mtumishi wa umma basi aagize mamlaka yake ya nidhamu ichukue hatua.

Kuna masuala mengine yanashughulikiwa na taasisi za Serikali kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), DC anaamuru kuwekwa mahabusu kwa watendaji wa kampuni inayodaiwa kodi. Masuala ya kodi yana utaratibu wake.

Bahati mbaya sana, wapo ma-DC wanaona kwa kuamuru kuwekwa ndani hovyo hovyo kwa watu (hasa wa kisiasa), ndio anapata kiki ya kuukwaa u-RC, bila kujua jamii inamdharau na kumpuuza.

Ndio maana nasema Jaffo amenena, na ma-DC wetu sasa warudi kwenye msitari na watambue kuwa kiki zao hizi wanazozitafuta bila kufuata sheria, zinajenga chuki kati ya Serikali na wananchi.

Columnist: mwananchi.co.tz