Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

JPM amethibitisha ‘ukweli hauna kura ya wengi’

Tue, 5 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nimeamua kuandika makala hii baada ya kupitia nukuu hii “Kanuni za maadili hazina kura ya wengi, kosa linabaki kosa hata kama watu wote wamekosea. Ukweli unabaki kuwa ukweli hata kama hakuna mtu mmoja aliye kweli.” Ni nukuu ya maneno ya Fulton Sheen, Askofu Mkuu wa Kikatoliki huko Marekani.

Rais John Magufuli amejitengenezea wapinzani wachache ambao wanaamini katika “Funika kombe mwanaharamu apite”, kwa kutuaminisha ndio “diplomasia au itifaki”.

Rais husema anachokiamini na ana uhakika wa kukisimamia au kukitekeleza. Hataki “mwiko uitwe kijiko kikubwa” maana jina lake ni mwiko. Hataki kumumunya maneno kuuelezea ukweli ili aungwe mkono na wengi au asiumize hisia za wachache.

Hasemi hapana akimaanisha ndio wala kusema ndio ili akuridhishe kwa muda tu kukidhi matakwa ya kadamnasi au kwa rafiki zake huku moyoni akijua ni hapana. Ameyaishi maneno ya Baba wa Taifa kwa kuonyesha bila mashaka mstari unaotenganisha majukumu yake aliyokabidhiwa na umma na mahusiano yake binafsi. Wengi tumemwelewa Rais Magufuli na kulifurahia hilo maana kuna wakati lilionekana kuwa tatizo sugu. Wachache wameliona ni bugudha kwa kukwamisha mambo yao yaliyotegemea vichochoro kumfikia ili kuyafanikisha kwa kujua kuwa hayana usahihi katika mkondo wa ukweli.

Nimehudhuria mkutano wa wadau wa sekta ya madini ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais Magufuli. Kama tulivyozoea, tulitegemea itifaki iongoze ushiriki wa Rais Magufuli katika mkutano huu. Bila kutegemea akaamua vingine kwa kuuweka ukweli mbele.

Aliiacha itifaki na kutanguliza ukweli kwa kuamua wadau waseme akiwapo, badala ya milolongo ya hotuba huku nusu ya muda ikitumiwa kutambua uwepo wa waheshimiwa, maana aliamini kuwa wadau wanamhitaji awasikilize.

Vinginevyo wadau hao wangeficha yale waliyotaka Rais wao ayasikie maana shida na changamoto zao tayari zinajulikana kwa watendaji wake na walishakutana nao mara nyingi. Mambo waliyoeleza wadau wa madini yalikuwa makubwa na muhimu sana katika kuhakikisha kila senti ya Watanzania inatumika kwa manufaa ya wote na sio vinginevyo. Kupenda kwake ukweli kulifanya Watanzania na hata wageni wenye nia njema na Tanzania kufunguka na kuwafundisha wateule wa Rais jinsi tunavyoweza kufaidika na madini yetu.

Hawa walikuwa ni Watanzania wa kawaida na wengine wenye uwezo mkubwa kifedha waliokuwa na uchungu na nchi yao na wakiwa na shauku ya kuisemea Tanzania changamoto zinazoikabili katika sekta ya madini na kutoa maoni yao kuhusu utatuzi wake.

Niliwaona Watanzania hawa walivyozungumza kwa uchungu kuhusu kupotea kwa raslimali zetu kutokana na kufanya kazi kwa kiburi na mazoea kwa baadhi ya watendaji. Walikuwa wawazi na wakweli na hawakuwa na diplomasia katika kuwasilisha mawazo na hisia zao kuhusu jambo hili muhimu katika uchumi wa nchi yetu. Walisema hali ilivyo katika lugha sahihi na isiyo na mafumbo wala kificho. Ni wafaidika wa tabia ya ukweli na uwazi.

Waliamini kuwa msema kweli ni mpenzi wa Mungu na kutekeleza kwa vitendo imani yao mbele ya Rais. Waligombea kipaza sauti ili kuelezea machungu yao kutokana na hasara tunayoipata kwa uzembe uliopo. Hawakuangalia faida zao binafsi bali ukweli kuwa maslahi mapana ya taifa yamepuuzwa. Wengi wetu tunasubiri mrejesho kutoka kwa wateule wa Rais kama ukweli umezaa matunda.

Baada ya wadau wa madini, Rais Magufuli akakutana na viongozi wa dini ili kuwasikiliza hoja zao ana kwa ana. Alikuwa na haja ya kufanya hivyo kama mkuu wa nchi kwa kutambua nafasi ya viongozi wa dini katika ustawi wa Taifa letu, hasa tunapozungumzia amani ya Tanzania. Rais Magufuli aliwapa nafasi ya kusema kwa uwazi mkubwa viongozi wetu wa dini na wao waliitumia vizuri kwa kuelezea changamoto nyingi zinazohusiana na utekelezaji wa imani zao, maendeleo ya nchi, siasa, na upatikanaji wa huduma za jamii.

Rais hakuwaza na kuzipa nafasi rabsha zilizopita huko nyuma huku viongozi wa dini pia wakionyesha kuyaishi maandiko kwa kuganga yajao, Askofu Gwajima na Askofu Kakobe walikuwapo. Ulikuwa ni mkutano wa Watanzania na kiongozi wao kuhusu ustawi wa nchi yao. Walikuwa Watanzania kama familia moja wakijadili suala la kifamilia bila kuangalia faida au hisia za mtu mmojammoja. Yote hayo waliyaweka pembeni na kutafuta majibu ya masuala mazito kwa ajili ya mustakabali wa nchi yao.

Walikuwa wamoja na kufikiri na kujadiliana kama mwili mmoja wenye viungo mbalimbali, lakini vyenye lengo moja tu. Ilikuwa ni tunda la tabia ya ukweli ya Rais Magufuli.

Walitukumbusha unyenyekevu na kuheshimu mawazo ya wenzetu bila kejeli au matusi. Waliamini katika tabia ya ukweli ya Rais Magufuli na aliwajibu ukweli bila kupepesa macho kwa kuamini “ukweli hauna kura ya wengi”. Hakukuwa na jaziba katika maswali, maoni, na majibu yaliyotolewa zaidi ya ukweli.

Ukweli wa Rais Magufuli umeonekana katika matendo yake. Alisema ukweli kuwa matumizi ya fedha za serikali hayalengi kuwanufaisha wachache. Amethibitisha hili kwa kuhakikisha kodi inakusanywa na kutumika kwa manufaa ya wote. Ametumia kodi zetu kujenga reli ya kisasa, kutuhakikishia umeme wa uhakika siku chache zijazo, kufufua shirika la ndege, kujenga barabara mpaka za vichochoroni, kuboresha huduma za afya na elimu, na mengine mengi. Tunaambiwa na wapinzani wa ukweli kuwa alichoharibu ni kutumia fedha za ndani kutekeleza ukweli huu maana angekopa. Ila ahakikishe deni la taifa halikui! Yaani ahakikishe keki imeliwa lakini ibaki kama ilivyo! Hii inaitwa ghiliba au uongo. Hakusita kusema ukweli kuwa hatufaidiki na raslimali zetu hasa madini. Akauonyesha ukweli huo kwa kutoogopa kusema ukweli machoni mwa matajiri wenye nguvu ya fedha na uwezo wa propaganda katika vyombo vya habari vya kimataifa kuwa wanatuibia.

Ajabu, hata mtangazaji mmoja mahiri wa BBC katika kipindi cha mahojiano na Mtanzania mwenzetu ametukumbusha hili na kutushangaa kwa kutotambua ukweli huu.

Wageni walitaka waendelee kugawana faida huku tukiaminishwa uongo kuwa madini yetu ni hasara tupu. Matokeo yake Rais Magufuli amepata uungwaji mkono mkubwa nchini na kimataifa na kuwafanya wababe wa dunia kuwa wapole na kutafuta muafaka.

Ukweli ndio umewafanya baadhi ya wadau wa sekta ya madini nchini waliokuwa wakinufaika na uongo kutoka hadharani na kukiri kuwa wanaiba na wanajisikia vibaya huku wakipendekeza njia za kuziba mianya na vishawishi vya wizi.

Amesema ukweli kuhusu safari za Rais na wateule wachache nje ya nchi zisizo na sababu maalumu na gharama kubwa na akaamua kubaki nyumbani na kuthibiti safari za nje za wateulwe wake ili tufaidike wote.

Wahanga wa tabia ya ukweli ya Rais Magufuli hawalali ili kulazimisha awe muongo, eti ni itifaki na diplomasia. Wanajitahidi uongo uwe ukweli ili wafaidike na hizo itifaki na diplomasia maana ukweli umewanyima ulaji.

Ukweli unabaki kuwa ukweli hata kama hakuna mtu mmoja aliye kweli. Umetuthibitishia msemo huu wa hekima kwa matendo.

Catherine Magige ni mbunge wa Viti Maalumu kupitia CCM. email: [email protected]



Columnist: mwananchi.co.tz