Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

JICHO LA MWEWE: Maisha yalivyoenda kasi kwa Balinya na Yanga

88921 Balinya+pic JICHO LA MWEWE: Maisha yalivyoenda kasi kwa Balinya na Yanga

Wed, 18 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

HATA kwa Cristiano Ronaldo haikuwahi kutokea vile. Hakuwahi kutambulishwa katika mkutano wa wanachama wa klabu yoyote aliyohamia. Hakuwahi kutambulishwa mbele ya wanachama wa Manchester United, Real Madrid wala Juventus Turin.

Lakini ilimtokea mchezaji anayeitwa Juma Balinya. Watu wa Yanga walimteka uwanja wa ndege na kumpeleka katika mkutano wao pale Upanga. Heshima iliyoje. Mchezaji badala ya kutambulishwa kwa waandishi wa habari ikaamuriwa atambulishwe kwa wanachama.

Tukampokea Balinya. Yanga inadaiwa kwamba walimuiba kutoka katika mikono ya rafiki zao, Simba ambao walikuwa wanamtaka. Yanga wakajisifu sana. Inabidi uwakubali tu Yanga jinsi wanavyopenda kutembeza ubabe kwa Simba iwe wakati wa umaskini au utajiri.

Balinya alikuja na sifa nyingi lakini zaidi alitoka kuwa mfungaji bora katika Ligi Kuu ya Uganda. Waganda wametuzidi mpira kwa mbali. Kwa sasa wana kila kitu katika kutuzidi ila kitu kimoja tu. Hawana Mbwana Samatta katika soka lao.

Baada ya kelele zote kuhusu Balinya, wiki iliyopita amepewa barua ya kuondoka klabuni. Pande zote mbili zimeafikiana kuachana. Balinya na Yanga. Hivi ndivyo maisha yalivyoenda kasi. Balinya kwa sasa ni mchezaji huru. Mpira wa Tanzania umemshinda. Yanga nao hawamtaki.

Inaacha maswali mengi. Ni kweli mpira wa Tanzania umemshinda? Ninachojua ni kwamba mshambuliaji hawezi kuibuka mfungaji bora katika Ligi Kuu ya Uganda bila ya kuwa na kitu katika miguu yake na kichwa chake. Lazima ana vitu.

Waganda wametuzidi mpira. Hauwezi kuwa mfungaji bora katika ligi yao kirahisirahisi tu. Lazima kuna kitu. Ni kitu hiki ndicho ambacho Yanga wameshindwa kupata ubora wake.

Kwanza kabisa kocha wao aliyepita, Mwinyi Zahera. Chini yake wachezaji wengi wameshuka viwango. Kuanzia wale wa nje hadi hawa wa ndani. Hata leo nikimtazama Fey Toto huwa simuelewi ni mchezaji wa aina gani. Alipoingia Yanga alikuwa hatari. Sasa hivi kila siku kiwango chake kinashuka.

Huyu Balinya nilimtazama katika mechi alizocheza siku za karibuni nikagundua ni mchezaji hatari. Anajua namna ya kulisaka boksi la adui na kujiweka katika nafasi. Hata hivyo uwezo wake wa kujiamini ulishuka kwa sababu Zahera alikuwa hampangi.

Hapo hapo unajiuliza. Alifunga mabao mengi Uganda. Yanga walijua alikuwa anafungaje? Wanajua ni mshambuliaji wa namna gani. Kuna washambuliaji wa aina nyingi duniani ingawa wote kazi yao ni kufunga mabao.

Kuna washambuliaji ambao ni wazuri katika kumalizia tu. Kuna washambuliaji ambao wana ubora wa kujitengenezea nafasi na kufunga. Yanga walifahamu wanamsajili mchezaji wa aina gani? Walifahamu ni namna gani wanaweza kufanya kupata ubora wake? Hii ni sayansi ya mpira ambayo klabu zetu hazina.

Hawa akina Balinya ni aina ya wachezaji ambao baadaye tunasikia wanakuwa mastaa wakubwa katika klabu nyingine mbalimbali nje ya Afrika Mashariki. Wenzetu wanajua jinsi ya kutunza wachezaji wao na kujua namna ya kuwatumia.

Yanga wamejidanganya kwa kutafakari kiwango cha Balinya tu bila ya kutafakari mambo mengi yaliyowazunguka. Uwezo wao wa kulipa mishahara upo chini, uwezo wao wa kuwatunza wachezaji upo chini. Kuna wachezaji hawawezi kung’ara katika mazingira hayo.

Huyu Balinya ni mchezaji anayejiamini ndio maana nasikia yeye mwenyewe aliamua kuondoka baada ya kukosa nafasi. Anaujua uwezo wake na ndio maana hakutaka Yanga imuache ili imlipe fidia. Anajua kwamba Yanga inampotezea muda na atakwenda kukusanya noti sehemu nyingine.

Ushahidi wa mazingira haukuonyeshi kwamba Balinya ni mchezaji mbaya. Kinachotokea kwa sasa pale Yanga kila mtu ni tatizo. Kocha, viongozi, wachezaji, mashabiki na kila mtu anaonekana kuwa tatizo klabuni.

Kwa sasa wanasafisha klabu yao kwa sayansi ya soka letu. Ameanza kuondoka kocha. Viongozi walipoona kwamba mashabiki wameanza kuwageuka na wanahoji umakini wao katika kuiongozi klabu na wao wameanza kutupa mzigo kwa wachezaji. Kila mtu anamtoa kafara mwenzake.

Kwa mazingira yaliyopo Yanga kwa sasa nadhani wataachana na wachezaji wengi tu wazuri. Kama mchezaji bado hajafikia fomu yake vyema na anadai mshahara wa miezi miwili basi ataachwa. Hatukusikia matatizo kama haya wakati wakati wa utawala wa Yusuf Manji lakini sasa tunayasikia.

Donald Ngoma alisajiliwa kwa pesa nyingi kutoka kwao Zimbabwe. Hakuanza vyema pale Yanga. Alionekana kama mchezaji wa kawaida tu. Walimvumilia. Baadaye akaibuka kuwa staa mkubwa klabuni. Ingeweza kutokea hivyo kwa Balinya lakini mabosi wanaamini kwamba analipwa mshahara mkubwa na hafungi.

Mchezaji anayeitwa Makambo naye alianza kwa kudorora. Kuna baadhi ya mashabiki walihoji kiwango chake. Baadaye akaanza kufunga na kuwaziba mdomo mashabiki. Wakati ule yule kiongozi wa Yanga, Katibu Omary Kaya walau aliweza kuwalipa mishahara wakacheza. Hawa wa leo kwa sababu hawawezi kulipa mishahara basi wanakosa uvumilivu kwa wachezaji wao. Kwaheri Balinya.

Columnist: mwananchi.co.tz