Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

JICHO LA MWALIMU : Wizi wa mitihani unatokana na elimu kugeuzwa bidhaa

Wed, 17 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bidhaa ni vitu vinavyouzwa na kununuliwa katika biashara.

‘Ubidhaishwaji’ ni kitendo cha kufanya kitu kuwa bidhaa kwa lengo la kufanya biashara.

Ubidhaishwaji wa elimu ni chanda na pete na ubinafsishwaji wa elimu. Kitu kinapobinafsishwa ni ile hali ya kukifanya umiliki wake ambao ni mali ya umma kuhamishiwa kwa wamiliki binafsi.

Mchakato huo husababisha changamoto nyingi katika utoaji wa huduma mbalimbali.

Hapo awali Serikali ilichukua jukumu la kutoa huduma hiyo nchi nzima tena kwa sera ya elimu bure. Changamoto zilianza kujitokeza baada ya Serikali kufungua milango ya sera za kiliberali na utandawazi kwa taasisi za mashirika ya dini, asasi za kiraia, watu binafsi na wadau wengine wa elimu kusaidia Serikali katika kutoa huduma ya mbalimbali ikiwemo elimu.

Hapo ndipo suala la elimu kuwa kama bidhaa na shule kama kampuni au viwanda lilipoanza kujitokeza; na changamoto kadhaa zikajitokeza katika utekelezaji wake.

Ubinafsishwaji wa elimu una faida nyingi na changamoto zake pia. Baadhi ya faida ni kutoa fursa ya idadi ya watu wengi kupata elimu na tena iliyo bora.

Athari za mfumo huo huweza kutokea tu pale usiposimamiwa kwa sera madhubuti, kwani huweza kuwa sababu ya kuligawa taifa.

Huweza kutengeneza matabaka kati ya wasomi waliopata elimu bora na fursa na kundi jingine la wasomi waliopata bora elimu ambao hukosa fursa za mtandao wa wenye uwezo..

Aidha, katika mfumo wa ubidhaishwaji wa elimu, wananchi (wanafunzi) hugeuzwa kuwa wateja na kama ambavyo inafahamika katika mifumo ya soko huria, bei ya bidhaa huamuliwa na nguvu ya soko.

Hivyo, kuwapo kwa watoa huduma waliojikita kibiashara zaidi ili kupata faida kubwa, ni jambo lisilokwepeka.

Watoa huduma hao wanapoigeuza elimu kuwa biashara, ndipo hata mbinu chafu huanza kutumika. Ili shule hizo za kibiashara siyo za kihuduma ziweze kupata wateja wengi, itazilazimu zijikite kule wanakohitaji wateja wao.

Wateja wanahitaji ufaulu. Wanahitaji elimu ya ufaulu. Wateja wanataka kusikia alama za juu na nafasi za juu kitaifa. Lakini hao hao wateja huziba masikio kuhoji umahiri wa walimu, nidhamu na maadili ya wanafunzi. Husahau kuhoji uzalendo wao, utayari wao wa kujitolea kwa nchi yao.

Kwa nini wezi wa mitihani ni wezi na siyo walimu?

Yapo maswali mengi ambayo jamii haina budi kuyatafakari. Kwa nini wanaoitwa ‘walimu’ huiba mitihani? Na humwibia nani na kwa sababu zipi?

Pia, ifahamike kwamba wezi wa mitihani siyo ‘walimu’, bali tunapaswa kuwaita ‘wezi, wahalifu au wahujumu uchumi’ kama walivyo wahalifu wengine.

Kwa nini wanaiba mitihani?

Sababu zinaweza kuwa nyingi, lakini moja kubwa ni ukosefu wa maadili. Wezi wa mitihani wanaoitwa walimu huwa na sababu kadhaa nyingine ni msongo, woga, kutojiamini, kutaka sifa wasizostahili, tamaa ya fedha na msukumo usiokuwa wa kitaaluma kutoka kwa wamiliki wa shule hizo.

Pia, ieleweke wazi kuwa wizi huo hauko tu katika shule binafsi. Hata shule za umma pia zipo ambazo wanaojiita walimu wameshiriki michezo hiyo michafu inayohujumu maslahi ya elimu.

Sababu nyingine ni kigezo cha ushindani wa kishule, kiwilaya, kimkoa na kitaifa ili wahusika kutaka sifa wasizostahili.

Athari za wizi wa mitihani kwa taifa

Sifa au jina baya huenea kwa kasi kuliko kujenga jina safi na imara. Kujenga uaminifu na umahiri, huhitaji muda, lakini kuharibu uaminifu na sifa njema, hakuitaji muda mwingi bali hata tukio moja tu.

Wizi wa mitihani ni tendo baya. Hata wizi wa kazi za kitaaluma au za kisanii za watu wengine, una uhusiano na wizi wa mitihani. Vitendo vya wizi wa kura katika uchaguzi, pia vinaweza kuhusishwa na mmomonyoko wa maadili ulioanzia katika wizi wa mitihani.

Sifa mbaya ya wizi wa mitihani katika mfumo wa elimu wa ngazi yoyote ile, huathiri maslahi mapana ya maendeleo ya taifa, hivyo kinapaswa kuchukuliwa kama kitendo cha kuhujumu taifa.

Fikiria itakapofika wakati ambapo mataifa mengine yatakapokuwa na mashaka na wasomi wetu. Sisi wenyewe ndani ya nchi tunahudumiwa na daktari, lakini unamtazama mara mbili mbili na kujiuliza moyoni kama ana sifa.

Athari kubwa ni kupata watumishi wa kada mbalimbali ambao siyo waadilifu. Hawana maadili kwa sababu wamekulia hivyo katika mfumo huo tangu shule ya msingi.

Huwezi kutegemea mtu huyu akikabidhiwa madaraka makubwa abadilike; bado atakuwa na harufu za udanganyifu. Wizi wa mitihani hutengeneza tabia na utamaduni wa kupata taifa lisilo na maadili.

Hivyo basi, Serikali ikumbuke kuwa taasisi za kielimu za mashirika binafsi au ya dini, wadau wengine siyo washindani wake bali ni wasaidizi tu au washirika katika maendeleo.

Serikali ndiyo yenye dhamana nambari moja ya kuhakikisha jamii inapata kilicho bora kwa thamani ya fedha stahiki.

Wathibiti ubora wa elimu, wana nafasi kubwa ya kubaini viashiria mbalimbali vya michezo michafu katika ngazi yoyote ile ya elimu, endapo tu watawezeshwa ipasavyo.

Columnist: mwananchi.co.tz