Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Irene Uwoya na unafiki wa Bongo Movie

9821 Levy TZWeb

Sun, 24 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanzoni mwa wiki hii jioni moja nikiwa mitaa ya Kurasini baada ya shibe ya mwaliko wa futari kwenye mkeka mujarabu nimelaza mbavu zangu kilofalofa huku nikiperuzi simu yangu.

Bongo Movie siyo kitu kidogo. Lakini wasanii wenyewe wanataka kionekane kitu kidogo. Cha kipuuzi na kisicho na faida yoyote kwa jamii. Wanakosea sana.

Inashangaza kuona mashabiki wanaumizwa na sanaa kuliko wenye sanaa wenyewe ambao ni wasanii. Wasanii wanaona poa tu bora liende.

Wakati wengi wakitaja vitu vingi vya kufanya ili soko la filamu lipande tena au zaidi. Mimi naamini mashabiki wakiwa wasanii na wasanii wakiwa mashabiki sanaa itakua haraka.

Joyce Kiria alipata umaarufu na pesa baada ya kuendesha vipindi vya Bongo Movie runingani. Kama ilivyo kwa Zamaradi Mketema, sanaa ya filamu imewapa maisha.

Vipindi vyao vilikuwa maarufu kwa sababu viligusa sanaa yenye mashabiki wengi. Nao wakawa maarufu kama wasanii na kufuatiliwa sana.

Ilianza kama utani. Wakati picha zikisambaa mitandaoni na magazetini wakipokewa uwanja wa ndege wa Jijijini Kigali, Irene Uwoya na wasanii wenzake kadhaa miaka 10 iliyopita.

Ilikuwa ngumu kuamini kilichotokea kwa fundi huyu wa kike kwenye kuigiza, mwanadada mwenye macho yake. Mpaka rangi bora wa ‘muvi’ kwa muongo mmoja uliopita.

Kichaa wa kuigiza mahaba. Mwenye mwili uliyofunga ndoa na filamu. Anajua kuigiza na anajua kuwa anajua na zaidi ni mzuri na anajua kuwa yeye ni mzuri. Ogopa sana mwanamke wa hivyo.

Endelea kubishana kwa sababu hujamshuhudia uso kwa macho. Ukipewa sifa zake mbaya tu, lakini utampenda ghafla na kusahau kila kitu akiibuka mbele ya uso wako.

Inatokea kwa wachache sana ambao vipaji vyao vinafunika maovu yao. Uwoya alipendwa na watoto. Akakubalika kwa vijana na watu wazima. Na zaidi akahusudiwa na wasichana wenzake.

Jibu utakalopewa na mashabiki wa Rwanda kuhusu uwezo wake wa kuigiza, litakuwa Kulwa. Na jibu utakalopewa na mashabiki wa Bongo kuhusu uzuri na muonekano wake litakuwa Dotto.

Wengi hawakuamini kama Irene Uwoya na wenzake wamealikwa kwenye viunga vya Ikulu ya Kagame pale Kigali. Ilipoandikwa mitandaoni na magazetini ilikuwa kama uongo tu.Ndoa yake na Marehemu Ndikumana, ikawaaminisha wengi, na kuamini kuwa sanaa ya filamu nchini imesambaa ukanda wote wa Afrika Mashariki na Rais Paul Kagame ni miongoni mwa mashabiki wake.

Baada ya ndoa, Uwoya akawa wakili wa Bongo Movie nje ya mipaka ya Tanzania. Na shahidi wa namna gani sanaa ya filamu ilivyosambaa na kupendwa na mamilioni ya watu.

Huyu Uwoya hakuwa wa dunia hii. Shangwe lake huko Rwanda ukawa mfereji kwa wasanii kama Kanumba kuwavamia kina Ramsey Noah huko Nigeria na kufanya nao kazi.

Ni muigizaji ambaye watu walitamani kumuangalia kuliko kuelewa stori ya filamu husika. Walifurahia kumtazama Uwoya kuliko kuelewa kisa cha filamu ya Oprah.

Wengi wanaikumbuka filamu ya Oprah, ila stori yake hawaikumbuki. Uwoya anavutia kumtazama runingani. Na ukikutana naye ‘laivu’ utaamini kuwa kamera zina chuki naye.

Mashabiki wake wanavutiwa naye runingani na mitandaoni. Wasanii wenzake, na watu wake wa karibu wanavutiwa naye zaidi akiwa nje ya runinga na mitandao.

Wakati wazazi wake waliogopa sanaa kumkosesha familia. Mashabiki waliogopa familia itawakosesha kivutio chao kwenye sanaa. Alikuwa sehemu ya utalii wa ndani.

Kuna kundi la watu lilichukia alipoolewa na Ndikumana na likakerwa kwa ndoa yake na Dogo Janja. Sababu ni mwanamke ambaye kila mwanaume angetamani awe wake.

Inaweza kuwa filamu mbaya, lakini ukijua Uwoya yumo ndani utajilazimisha kutazama.

Kuna wakati alionekana anawaonea wenzake au kalazimishwa kuigiza nao. Alikuwa juu sana.

Walikuwepo waigizaji wengi wa kike. Lakini yeye alikuwa kama mtende ulioota katikati ya Jangwa. Alionekana peke yake kama alama ya filamu kwa viumbe uzao wa Eva.

Huyu wa leo tofauti na yule aliyetetemesha miwani ya Rais Kagame kule Ikulu Kigali. Aliyefanya Hamad Ndikumana apigwe upofu asione warembo waliojaa Rwanda na kuja kuona Bongo.

Huyu wa sasa ukiondoa wazazi wake pengine ni Dogo Janja pekee anayemuelewa. Uzito wa thamani yake kaubomoa bila tingatinga kama lile la nyumba za wakazi wa Kimara.

Ukubwa wa jina na ubora wa sura, umbile na rangi yake havina uhusiano wenye tija na tabia zake za sasa. Walioumizwa na kuolewa kwake wanaweza kujiua kwa kukengeuka kwake.

Uwoya wa sasa ni yeyote tu. Siyo kwa kupatikana hovyo ila kwa kuonekana hovyo. Akiwa mzazi tayari anaanika maungo yake mitandaoni huku akajiita mtoto wa Kiislamu eti.

Msanii wa Bongo tofauti na Hollywood. Tunazidiwa kila kitu kasoro kimoja ambacho ni aibu na utu. Ila tunakoelekea hata hilo watatuzidi kwa sasa.

Wakati tukio la video ya kipuuzi ya Nandy na Bilnass tukidhani bahati mbaya, Uwoya anatuambia tunakosea na tuko nyuma na akili za mastaa wetu kwani ni maisha waliyochagua kuishi.

Wasanii badala ya kuitazama jamii yao kabla ya kufanya jambo hadharani. Wao wanapeleka jambo hadharani kwanza ili watazame jamii itasemaje.

Kwa tamaduni zetu msanii kufanya anachofanya Rihanna, utakera na kupoteza watu. Utakutengwa na kupunguza mvuto wa sanaa kwa mashabiki.

Leo hii Uwoya ameamua kupiga picha za utupu na kutundika mitandaoni. Akiacha mwili wazi ili tuone sehemu nyeti anazostahili kuona Dogo Janja.

Na haoni kama ni kosa na anatushangaa tunaomshangaa na kutuona washamba na kutusuta. Anabishana na mashabiki wanaopinga upuuzi wake.

Uwoya anaiga kwa kina Kardashian wakati tamaduni ni tofauti. Wenzao kukaa utupu wanalipwa na majarida kama PlayBoy, yeye anaanika utupu wake Instagram bila malipo.

Wakati mashabiki wakilalamika, Shamsa Ford anamuunga mkono. Na yeye ni msanii pia na mke wa mtu siyo mdangaji. Huu ndo unafiki wa Bongo Movie.

Any way haishangazi sana kwa mwanamke ambaye aliwahi kukiri hadharani kuwa aliolewa lakini hakuwahi kumpenda mumewe, unategemea nini?

Hiki ni kiherehere chetu tu. Tuwaache wenyewe wameamua kuishi hivyo. Hasira zinakuja pale wanapoomba pesa za walipa kodi kujitibia magonjwa yao.

Columnist: mwananchi.co.tz