Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ifahamu tabia ya pesa kwenye maeneo mbalimbali ya maisha yako

Mon, 26 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katika miaka ya hivi karibuni wanasaikolojia na watafiti wengi ulimwenguni wamekuwa wakiandika na kuchambua mengi juu ya saikolojia ya pesa, hili ni eneo linalokuja kwa kasi sana wengi wakipenda kujua na kuchimba kuhusu saikolojia iliyopo kwenye suala zima la pesa.

Katika makala hii najaribu kupita maeneo mbalimbali ya maisha ya kila siku nikiyahusisha na pesa katika mtazamo wa kisaikolojia zaidi.

Pesa na hisia

Utakubaliana nami kwamba kuwa na pesa nyingi hakumaanishi kuwa na furaha, inaweza kufanikiwa kukupa kicheko na wengine wakakuona kama vile una furaha lakini unajua kabisa kuwa ndani yako imejaa huzuni, ingawa ukweli upo kwamba umasikini sio furaha pia.

Tafiti zinaonyesha kwamba watu hutumia pesa zaidi wakiwa kwenye hisia zilizoshuka, kama vile wakiwa wanajihisi upweke, ingawa hawagundui wakati wanafanya matumizi hayo. Kwa kufanya hivi mtu huhisi kuitafuta furaha tena hususani pale ambapo huitumia pesa yake kwa wengine, kama vile kuwanunulia vitu, chakula au vinywaji. Hapa ni rahisi kuhisi kuwa pesa inaleta furaha.

Pesa na manunuzi

Wengi wetu hatufahamu vizuri mambo yahusuyo manunuzi, wengi huwa tunadhani kwamba bidhaa fulani ni bora kwa sababu tu bei yake iko juu. Mara nyingine manunuzi huanzisha kasi ya kununua kila unachokiona mbele yako, kwa mfano, mara nyingine unafungua pochi yako unatoa hela na kununua kitu, kabla hata ya kuifunga pochi yako macho yanaona kitu kingine, na kingine, na kingine tena mara unajikuta umenunua hata ambavyo hukupanga kununua tena unaweza kufika nyumbani ukashangaa hata hauvitumii vile vitu ulivyonunua na baadaye hata kuvitupa au wala kutofurahia matumizi yake. Lakini ulishanunua na pesa ulishatoa.

Pesa na haiba

Ni vema ukifahamu kwamba kila mwanadamu ni tofauti na mwenzake hii inamaanisha pia kwamba hata namna unavyoshughulikia pesa ni lazima iendane na haiba yako. Kwa mfano kama wewe ni kati ya watu ambao huhisi mambo ya kesho yatakuwa vema tu na hakuna lolote baya litakalo tokea basi kuna uwezekano ukatumia pesa zako pasipo uangalifu, wala bila kuwaza habari ya kuweka akiba. Ziko tafiti ambazo pia zimeonyesha uhusiano kati ya akili na pesa, na kwamba, watu wenye akili zaidi wana uwezekano wa kuwa makini zaidi katika mambo yahusuyo pesa kuliko wengine. Hii haimaanishi kwamba watu hawa mara zote wanakuwa matajiri. Kuna uhusiano mdogo sana kiutafiti baina ya akili na utajiri.

Pesa na ubongo

Ingawa ubongo una uvumilivu sana lakini madhara yeyote katika ubongo huathiri utendaji kazi wa ubongo na kama ubongo umeathirika mambo mengi sana huathirika, ikiwemo pia ujuzi na uwezo wa kuishughulikia pesa, mfano, kuitafuta, kuitumia, na kuiwekeza. Mawazo yako kuhusu pesa lazima yataathirika, matumizi yako yanaweza kutokuwa ya kawaida kabisa.



Columnist: mwananchi.co.tz