Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ibarikiwe bunduki ya mlinzi, ilaaniwe ya jambazi

61842 BUNDUKI+PIC

Mon, 10 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kijana mmoja alifuata mafunzo ya dini kupitia kwa Walii. Walisaidiana kwenye shida na raha. Kijana alikuwa mchapa kazi na mtii na Walii alikuwa mcha Mungu na mwenye busara. Pengine ndiyo maana kila mmoja alimtegemea sana mwenzie.

Katika safari zao walipita kwenye nchi moja tajiri lakini iliyokuwa na migogoro chungu nzima. Hakukuwa na shida ya chakula wala mali lakini watu wake walikuwa na tamaa isiyomithilika. Kila siku bei ya bidhaa ilipanda na kuwafanya wanunuzi wakose msimamo.

Mfalme wao alikuwa juha kwa maana ya nusu chizi, saa mbovu. Kila siku alitoa maamuzi yaliyowaacha mawaziri wake midomo wazi. Sasa lilipokuja hili la mfumuko wa bei ndipo alipokuja na kali ya kufungia milenia:

“Nimeshatoa maagizo kwa wafanyabiashara kutowadhulumu wananchi wangu. Nawaonya kuwa wasiponisikia mara hii nitaamuru bidhaa zote zigawiwe bure kwa watu wangu. Lakini kabla ya hapo naamuru kuwa kila kitu kiuzwe kwa hela moja…”

Alishangiliwa sana. Nyumba ikauzwa hela moja, mbuzi hela moja na wembe wa kunyolea ndevu ukauzwa vivyo hivyo.

Yule kijana aliipenda fursa hiyo. Pamoja na Walii kumuasa kuwa nchi hiyo haitabaki salama, kijana aligoma kuendelea na safari. Akaweka kituo hapo na kufanya kazi kwa bidii. Akanunua mali nyingi sana na kuwa tajiri mkubwa aliyejulikana kila mahala.

Pia Soma

Alinunua mashamba ya chakula na akafuga wanyama wa kitoweo. Kila asubuhi alichinja mbuzi wa supu, mchana alikula pilau ya ng’ombe na usiku alikula kuku wa kupaka. Nyumba yake haikuisha harufu ya madikodiko, biriyani na rosti. Akawa mnene sana. Kuna wakati alivunja magurudumu ya magari yake ya farasi kwa uzito aliokuwa nao, lakini hakujali sana maana maisha yalikuwa matamu kwa upande wake. Siku moja alitembea ikiwa ni kwa ajili ya mazoezi na kufurahia mandhari. Akapita kwenye maeneo yaliyokuwa na ujenzi wa makazi ya watu.

Ghafla fundi muashi alishtuka sana kumuona mtu mnene kupita kiasi akikatiza karibu yake. Mshtuko wake ulisababisha amwage maji bila kipimo sahihi kwenye udongo wa kujengea. Fundi wa matofali naye kwa mshtuko alijikuta akiutumia udongo huo uliotoa tofali zisizo imara. Walipozisimamisha ukuta ulibomoka na kusababisha vifo vya mafundi hao pamoja na ndugu yao mjenzi.

Bi ajuza aliyekuwa akiwategemea wajukuu wake alikwenda kumlilia mfalme. Ikaamuriwa bwana huyo mnene akamatwe na kupelekwa kwenye baraza la mfalme asubuhi. Akashtakiwa na kupewa adhabu ya kunyongwa kwa kusababisha vifo vya vijana wasio na hatia.

Walii akapelekewa taarifa hiyo ya kusikitisha. Akafunga safari na kuwasili siku iliyopangwa kutekelezwa adhabu ya kijana wake. Aliingia barazani akiwa anahema kwa nguvu na kuombwa asikilizwe japo kwa dakika tano. Kwa wadhifa aliokuwa nao haikuwa rahisi kumkatalia:

“Mtukufu mfalme,” alianza akiwa na haraka zilezile, “kwa heshima na taadhima naomba uihamishie adhabu ya kijana huyu nitunukiwe mie…”

Kila mtu alishtuka. Alipoulizwa sababu ya maombi yake alisema: “Kwa miaka yote ya kazi yangu nimekuwa nikiisubiri nafasi hii kwa hamu kubwa. Nashangaa kwa nini kijana niliyemfundisha maandiko ya dini akitaka kunidhulumu kwa urahisi namna hii…”

Alipoagizwa kutoa ufafanuzi akasema: “Maandiko yanasema mtu atakayeuawa leo ataingia peponi moja kwa moja. Atapokelewa na wanawali kwenye meza kuu yenye kila aina ya starehe, watamlisha na kumnywesha kwenye karamu bora kabisa huku akipepewa kwa manukato yaliyo mema. Nakuomba sana…”

Mfalme na baraza lake walishtuka zaidi. “Kumbe wewe mtoto una hila sana, Mfalme alikuja juu”. “Unajifanya kuangua kilio kumbe unatucheka kimoyomoyo mnafiki mkubwa wewe! Je, hukuyajua yote haya?” Kijana aliapa kutofahamu lolote lakini Waziri Mkuu aliingilia kati kumuuliza Walii kuna chakula gani kilichoandaliwa kwenye karamu hiyo.

Akajibiwa kuwa kuna kila aina ya nyama mchemsho, za kukaangwa na za kuchomwa. Kuna minofu ya kuku wa kupaka na samaki, pilau, biriyani pamoja na juisi ya zabibu.

Mfalme alijiweka sawa kuzuia udenda, akauliza “sasa kwa nini juisi ya zambarau imesahaulika?” akajibiwa kuwa hadi ya forosadi imeandaliwa.

Sasa akawa mkali: “Kuanzia sasa wewe Walii na kijana wako sitaki kuwaona mjini kwangu. Mi sipendi hata kidogo wachoyo wa fadhila. Kila siku najituma kuhakikisha mnapata raha, lakini wenzangu mnanificha thawabu ziletwazo na Jalia.

Na wewe mnyongaji unasubiri nini wakati adhuhuri ishawadia? Funga kitanzi haraka tuanze zoezi letu, na ole wako umnyonge mwingine baada yangu”. Kwa staili hii Mfalme akanyongwa na Walii akamchukua kijana wake na kutokomea kusikojulikana.

Kuna uongo wa aina nyingi lakini aina tatu ndizo zilizo maarufu zaidi miongoni mwa walimwengu. Upo uongo ambao mtu huzusha ili kujilinda, mwingine mmoja anausema ili kumnusuru mwenzie (huu ndio alioutumia Walii), na tena kuna uongo unaozushwa ili kumkwaza mwingine.

Imeandikwa “usiseme uongo”, lakini kisu cha jikoni kina matumizi mazuri zaidi ya kisu cha mkabaji. Hapa wajuzi nadhani tutasaidiana hasa tukimkumbuka mwanamuziki aliyesema “ntakununulia ndege” wakati hana uwezo hata wa baiskeli.

Columnist: mwananchi.co.tz