Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Hotuba ya Mwalimu Nyerere: Tuna kazi moja tu, kumpiga Idi Amin

79933 Pic+nyerere

Tue, 15 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nimewaombeni mkusanyike tena hapa niwaelezeni jambo ambalo kwa sasa wote mnalijua. Lakini naona si vibaya nikieleza. Nitajaribu kueleza kwa ufupi.

Wakati nilipokuwa Songea katika ziara kule kuanzia juma la pili la mwezi uliopita (Oktoba) zilitangazwa habari kutoka Uganda kwamba jeshi la Tanzania limeingia Uganda na limechukua sehemu kubwa na kuua watu ovyo.

Siku hiyo zilipotangazwa habari hizo nilikuwa nimekaribishwa chakula cha jioni na vijana wetu wa jeshi pale Songea, na nikakanusha, na kwa kweli nikachukua nafasi hiyo kuvishutumu vyombo vya habari vya nje ambavyo vinapenda kutangaza tangaza uongo wa Amin.

Kila anapotangaza uongo wao huurukia na kutangaza kama kwamba ni kweli. Huo ndio uliokuwa uongo wake wa kwanza, na aliendelea endelea.

Baadaye akabadili sura ya huo akaongeza uongo wa pili katika shabaha hiyo hiyo kuwa Watanzania wanaua watu ovyo na kwamba wanasaidiwa na majeshi kutoka Cuba. Uongo huo nao tukaukanusha.

Kwa hivyo alivyozidi kusema habari hizo za uongo tuliendelea kuzikanusha na kuzipuuza. Lakini Alhamisi akatuma ndege za kivita Bukoba. Vijana wetu walizitupia risasi zikakimbia. Siku hiyo hiyo ikarudi tena moja, ikaangushwa.

Pia Soma

Advertisement
Ijumaa zikaja ndege katika eneo la Kyaka. Zikatupa mabomu. Vijana wetu walizitupia risasi, na mbili zikaangushwa.

Wakati huo huo ndege zetu mbili nazo zilikuwa zinatoka hapa (Dar es Salaam) kwenda Mwanza jioni. Kwa bahati mbaya zikakosea katika kutua shauri ya giza katika kiwanja cha Mwanza, na zikataka zigeuke na kujaribu tena.

Lakini ndege hizi zinakwenda kasi sana. Katika maeneo yale, tangu Amin alivyoanza kutangaza uongo, ni dhahiri tunaupuuza ule uongo, lakini hatuwezi kupuuza yote.

Kwa hiyo vijana wetu wamekwishaambiwa kuwa ndege za kivita zikionekana zipigwe. Kama vile zile za Bukoba na Kyaka zilipigwa, basi na hizi zikapigwa zilipofika Musoma. Walidhani ni za adui. Tukapoteza ndege tatu.

Lakini katika mambo ya vita ajali hutokea, na vijana hawa walikwishaambiwa ndege zikionekana zipigwe. Wangeziacha? Wanajuaje ni za adui? Kwa hiyo ikatokea bahati mbaya hiyo.

Matukio haya hatukuyatangaza. Hata kule kupigwa kwa ndege za Amin hatukutangaza. Hatukutangaza kwa sababu hatukutaka jambo lenyewe kulipa uzito mno. Tulisema akiendelea endelea kuleta ndege zake, tutaendelea kuziangusha kila zinapokuja.

Uwezo wa kuziangusha upo, na mwenyewe alijua uwezo upo. Ni vizuri akijua yeye. Tulijaribu. Tulikuwa tunaepuka kulipa uzito jambo lenyewe ambalo mwanzo wake ni uongo kabisa wa kuzua.

Kwa hiyo uongo wake akaendelea nao, na tukazidi kuukana. Na haya matukio ambayo nasema ni ya kweli, hatukutaka kuyatangaza kwa sababu hiyo niliyoieleza.

Sasa Jumatatu ndiyo akaivamia nchi yetu. Akaingiza majeshi yake kwa nguvu, nguvu kubwa. Yakachukua sehemu kubwa. Yakaingia ndani mpaka Kyaka. Hii tukatangaza kwa sababu lilikuwa ni jambo la kweli na yeye kama kawaida yake akakana akasema haikutokea hivyo.

Akaendelea kusema tu kwamba Watanzania ndio wako Uganda, ndio wamechukua sehemu ya Uganda. Akakana ukweli huo. Lakini tukawaeleza jamaa na mabalozi walioko Dar es Salaam kuwa huo ndio ukweli.

Huyu mtu ameivamia nchi yetu. Sasa jana ametangaza mwenyewe kwamba ni kweli majeshi yake yameivamia nchi yetu na yamechukua sehemu hiyo ya Tanzania iliyoko Kaskazini mwa Mto Kagera na kwamba tangu sasa eti sehemu hiyo ni ya Uganda na itatawaliwa kijeshi kama Uganda inavyotawaliwa.

Ndivyo alivyotangaza mwenyewe. Sisi ametusaidia katika kutangaza jambo hili, kusudi kwa sasa ubishi uishe. Hatuna tena tatizo la kuwaambia watu wenye akili duniani ni nini kimetokea.

Sasa hiyo ndiyo hali. Tufanye nini! Tunayo kazi moja tu. Watanzania sasa tunayo kazi moja tu, ni kumpiga.

Uwezo wa kumpiga tunao (vigelegele na makofi). Sababu ya kumpiga tunayo (vigelegele na makofi), na Nia ya kumpiga tunayo (vigelegele vingi na makofi zaidi). Tunataka dunia ituelewe hivyo. Kwamba hatuna kazi nyingine.

Na tunaomba marafiki zetu wanaotuomba maneno ya suluhu waache maneno hayo. Kuchukua nchi ya watu wengine si kwamba majeshi yamekosea njia na kusema kuwa sasa sehemu hiyo umeichukua na kutangaza vita kwa nchi ile nyingine. Si sisi tuliofanya hivyo. Amefanya hivyo mwendawazimu.

Na amefanya hivyo kwa jambo ambalo aliwahi kutangaza zamani. Aliwahi kusema zamani kidogo kuwa mpaka wa haki wa Uganda na Tanzania ni Mto Kagera, na kuwa siku moja atachukua sehemu hiyo. Ametimiza hivyo.

Sasa rafiki zetu, kama ni marafiki wa kweli, watataka tumwondoe mtu huyu. Hawawezi kutuomba suluhu au jambo la ajabu kabisa turudishe majeshi yetu nyuma. Niyarudishe wapi?

Kwa hiyo nasema tunayo kazi moja tu kumpiga. Hatukupenda kufanya hivyo. Maadui zetu ni mabeberu, na kwa hivi sasa wako Kusini. Serikali ya Afrika, hata kama hatupendi matendo ya viongozi wao, hatuwahesabu kama adui wetu.

Na kama Amin angekuwa amesema tu kwamba Tanzania ni adui wetu, sisi tungeendelea kumpuuza kama ni maneno hayo. Lakini kafanya kitendo cha uadui, hatuwezi.

Ameingia Tanzania mwenyewe. Na mtu huyu ni mshenzi. Ameua watu wengi sana. Kwa hiyo nasema tuna kazi moja tu. Tutampiga. Vijana wetu wako mpakani sasa hivi. Wako kule. Wako kule na mapambano yanaendelea.

Sasa hayo si mapambano ya TPDF (Tanzania People Defence Force) peke yake. Ni yetu wote. Kwa hiyo ninachowaombeni wananchi, hiyo kazi iliyoko mbele yetu muielewe.

Pili, tuwasaidie vijana wetu. Kila mtu kwa mahali alipo. Tutaendelea kila mapambano yanavyoendelea kueleza nini la kufanya na nani afanye nini.

Tutaelezana wakati wote huo mpaka tumemwondoa huyu nyoka katika nyumba yetu. Na tunawaomba mtulie. Katika mambo haya ya vita, na hasa kama watu mlikuwa mmezoea amani mnaweza kubabaika sana.

Msibabaike. Tulieni. Fanyeni kazi kama kawaida. Lakini mjue vitendo hivyo kazi yake ni hiyo moja, kumpiga mshenzi huyu aliyekuja katika nchi yetu.

Itaendelea kesho...

Columnist: mwananchi.co.tz