Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Hongera Samatta, umefungua njia

93739 Samatta+pic Hongera Samatta, umefungua njia

Thu, 30 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

NAHODHA wa timu ya Taifa, Taifa Stars jana ametimiza ndoto yake na ya Watanzania kwa kucheza mchezo wake wa kwanza akiwa na klabu yake mpya ya Aston Villa inayoshiriki Ligi Kuu ya England.

Hakika ilikuwa furaha kwa Watanzania wote wapenda michezo na hata wasiopenda michezo kwani, wengi walikesha wakisubiri kuona mchezo huo ambapo, Samatta alikuwa akiingoza Aston Villa kuvaana na Leicester City kwenye mchezo muhimu wa nusu fainali ya pili ya Kombe la Ligi maarufu kama Qarabao.

Shauku kubwa ya Watanzania haikuwa kumuona Samatta akifunga, bali kuwepo kwenye kikosi cha kwanza kilichoanza kwenye mchezo huo, ilikuwa furaha kubwa kwao.

Licha ya kwamba hakufunga bao, lakini uwepo wa Samatta uwanjani uliongeza kiu ya kikosi chake kuondoka na ushindi dhidi ya Leicester City.

Aston Villa ilishinda kwa mabao 2-1 na kusonga mbele kwenye hatua ya fainali ikiisubiri Manchester United ama Manchester City ambazo jana usiku zilikuwa zikimalizana pale Etihad. Japo kwa hesabu za vidole tu ni kwamba, tayari Man City imeshasonga mbele hatua ya fainali baada ya mchezo wa kwanza kushinda kwa mabao 3-1 kwenye dimba la Old Trafford.

Kwa maana hiyo ni kwamba, Samatta anakwenda kuwapa Watanzania furaha nyingine ya kukabiliana na Man City, ambapo kama kawaida Watanzania wote watakuwa nyuma yake kama ilivyokuwa jana pale Villa Park.

Pia Soma

Advertisement
Watanzania wengi walisafiri kwenda jijini Birmingham kumshuhudia Samatta huku wengine wakibanana kwenye baa na vibanda umiza kumsapoti kwa namna tofauti.

Tunampongeza sana Samatta kwa hatua hiyo, lakini tunaamini hilo ni somo kubwa kwa wachezaji wetu ambao bado wapo nchini ama wako kwenye mataifa mengine.

Vijana wengi wamekuwa na shauku ya kucheza soka nje ya nchi, lakini walikuwa wakikutana na vikwazo tofauti tofauti ikiwemo wao wenyewe kutojitambua.

Samatta amejitambua na kuweka bidii na ndio sababu amefanikiwa kutimiza ndoto zake.

Jambo la msingi hapa ni kwamba, Watanzania wako nyuma ya Samatta kwa sababu ametengeneza historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu England.

Hivyo, Samatta amefungua njia kwa klabu zingine Ulaya na mataifa mengine kuanza kuimulika Tanzania. Kwa sasa England wamekuwa wakilitaja jina la Samatta kutokana na uwezo wake uwanjani ni wazi mawakala maarufu wa wachezaji barani Ulaya, wataanza kuangazia Tanzania kusaka akina Samatta wengine.

Mpaka sasa Samatta ameshatimiza wajibu wake kwa kuondoa vikwazo na kufungua milango kwa wachezaji wengine ambao, jukumu lao kubwa ni kuonyesha kwamba wanasoka wa Watanzania wana vipaji na wanaweza kuhimili mikikimikiki ya ligi kubwa barani Ulaya. Kwa maana hiyo, ule mzuka wa Watanzania kukesha wakisubiri kumuona Samatta, uende ukahamasishe vijana wenye vipaji na wachezaji waliopo kwenye ligi mbalimbali nchini kujituma na kuheshimu ndoto zao badala ya kuona ni jambo la kawaida tu.

Columnist: mwananchi.co.tz