Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Homa ya Jiji aeleza Yanga ilivyomteka hotelini akisubiri kutia saini Simba

99307 Makumbi+pic Homa ya Jiji aeleza Yanga ilivyomteka hotelini akisubiri kutia saini Simba

Thu, 19 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mashabiki wa Yanga wakiamua lao hawashindwi. Ndicho walichofanya mwaka 1983 kwa Makumbi Juma, mshambuliaji aliyetikisa soka hadi kupachikwa jina la “Homa ya Jiji”.

Makumbi, ambaye familia yake ni mashabiki kindakindaki wa Simba, lakini mshambuliaji huyo wa zamani aliyekuwa na nguvu, ana mapenzi na Yanga.

Makumbi, mtu wa miraba minne enzi hizo, nusura atue Simba mwaka 1983 lakini jaribio hilo liligonga mwamba muda mfupi kabla ya kutia wino kwa klabu pinzani ya Mtaa wa Msimbazi .

“Nilianza kuipenda Yanga tangu nikiwa Shule ya Msingi Uvinza, kabla ya kuhamia Kigoma Sekondari,” anasimulia.

Anasema enzi hizo timu za shule yeye alicheza upande wa Yanga ndipo mapenzi na timu hiyo kongwe nchini yalipoanza wakati huo akicheza nafasi ya kipa kabla ya kaka yake Abuu Juma aliyekuwa beki wa Simba kumshauri abadili namba na kuanza kucheza nafasi ya ushambuliaji

“Nilipohitimu sekondari niliajiriwa na Pamba Kigoma nikiwa mchezaji, lakini mfanyakazi wa Mamlaka ya Pamba. Huko ndiko safari yangu ya kutua Yanga ilianza,” anasema.

Pia Soma

Advertisement
Yanga walipata taarifa zake baada ya kuonyesha kiwango kikubwa katika ligi ya vituo iliyochezwa Iringa. Shabiki kindakindaki wa Yanga wakati ule aliyemtaja kwa jina la Mzee Joshua ambaye alikuwa tajiri Kigoma, alianza kumfuatilia.

“Walinifuatilia mwaka mzima pasipo mimi kufahamu. Juma Shamte na Issa Makongoro nao wakafanya skauti yao. Mwaka 1980 tulipangwa kundi moja na Yanga katika ligi ya vituo iliyofanyika Mwanza. Huko ndiko nilizungumza na uongozi tukamalizana,” alisema.

“Ligi ilipokwisha walimtuma Kitwana Manara kunifuata Kigoma na nikaja kuanza maisha mapya ya mpira katika klabu ya Yanga. Mechi yangu ya kwanza kuchezea Yanga ilikuwa Nairobi kwenye mashindano ya Cecafa.

“Wakati ule Yanga ilikuwa na magwiji wanaojua mpira kweli. Niliulizwa pale mimi nitakwenda kucheza nafasi gani? kwa kuwa nilikuwa nikijiamini, sikuhofu.”

Anasema wachezaji wa zamani walikuwa na upendo na ndicho alikikuta Yanga tangu anaingia mwaka 1981 hadi mwishoni mwa mwaka 1991 alipostaafu.

Umafia wa Simba

Akiwa ameitumikia Yanga miaka miwili, Makumbi anasema Simba ilimshawishi ajiunge nayo mwaka 1983.

Uongozi wa Simba ulimtumia kaka yangu Abuu (alikuwa mchezaji wa Simba wakati huo, ambaye Makumbi anamfuatia kuzaliwa) kumshawishi.

“Aden Rage alinitumia tiketi ya ndege kutoka Kigoma nikiwa likizo nyumbani, kuja Dar kwa ajili ya kumaliza nao,” anasema.

Anasema licha ya Rage kumtumia tiketi, Yanga walifika uwanja wa ndege kumpokea. Wakati wakimsubiri upande wa abiria wanaowasili, Rage alimpitishia mlango wa VIP na kuwaacha Yanga uwanja wa ndege hawajui ameondokaje.

“Simba walinipeleka Kariakoo Mtaa wa Manyai nikiwa kule nawasubiri viongozi wa Simba, Rage akiamini niko na makomandoo wa Simba hotelini ghafla makomandoo wa Yanga wakavamia na kunichukua tukaondoka na mipango ya kujiunga na Simba ikaishia hapo.

Siri jina la Homa ya jiji

Makumbi anasema jina la utani la Homa ya Jiji alipewa na mtangazaji Charles Hilal akiwa katika moja ya mechi.

“Nilicheza mpira mwingi na katika kutangaza ndipo akanipachika hilo jina. Nilipolisikia binafsi nilifarijika ukizingatia nimetoka kijijini huko Kigoma na kutikisa Dar es Salaam hadi kupewa jina hilo, ilinifariji,” anasema Makumbi ambaye pia hujulikana kwa jina la ukoo la Bongabonga.

Afukuzwa Yanga

Mwaka 1988 Yanga ilimfukuza Makumbi kwa kile kilichodaiwa kuwa alikuwa akiwafundisha wachezaji utovu wa nidhamu.

“Tuliweka kambi Musoma wakati ule kina Sure Boy (Abubakari Salum) Zimbwe (Said Zimbwe), (Selestine Mbunga) Sikinde walikuwa rafiki zangu hivyo wakawa wananifuata,” anasema.

“Kocha Mwinda Ramadhan akasema mimi nawachukua wachezaji nawapeleka disco. Ile taarifa aliituma kwa uongozi Dar es Salaam.”

Anasema waliporudi Dar es Salaam uongozi ukamuita na kumtuhumu kabla ya kumtupia virago.

“Wakati ule hatukuwa na mkataba hivyo walivyonifukuza nikawaaga wachezaji wenzangu, nikaondoka kurudi Kigoma kujiunga na RTC,” anasema.

Anasema aliporudi RTC alipewa zawadi kubwa na meneja wa RTC wakati ule. Hata hivyo hakuitaja zawadi hiyo ingawa anasema ni kubwa na mpaka sasa anayo.

“Hawakuamini kama narudi kucheza nyumbani Kigoma,” anasema.

Anasema alipoondoka aliwambia Yanga na Simba wakienda Kigoma atawafunga na akija Dar es Salaam yeye atazifunga timu hizo kongwe.

“Nilitimiza ahadi yangu mwaka 1990 Yanga ikanirudisha kwa mara ya pili,” anasema.

Makumbi hatasahau hii

Katika matukio ambayo yanabaki katika historia ya Yanga ni kipigo cha mabao 3-1 ilichotoa dhidi ya Simba wakati wapinzani hao wakiwa wametoka kuweka kambi Brazil.

Makumbi, akiwa mmoja wa wachezaji wa Yanga waliofunga katika mchezo huo, anakumbuka namna mashabiki na wapenzi wa Simba walivyoikejeli Yanga wakati ule.

“Wakati Simba inaondoka ilikuwa gumzo sisi tukaenda Ngerengere. Walitukebehi kwelikweli walituita majina ya kila aina kwa sababu tu ya tofauti ya kambi yao na yetu,” anasema.

Anasema Simba waliporejea mechi ya kwanza ilikuwa dhidi ya Yanga na wapinzani wao walicheza mpira wa kiwango cha juu, lakini hawakufanikiwa kuifunga Yanga na mpira ukamalizika kwa suluhu kabla ya Simba kuifunga CDA Dodoma mabao 5-0.

“Tuliwaambia kama wametukosa safari hii, basi hawatufungi tena. Kweli mechi ya marudiano tuliwafunga 3-1,” anakumbuka Makumbi.

Anasema kambi ya Ngerengere ilikuwa imara kulinganisha na ile ya Simba ya Brazil.

“Kambi yetu ilikuwa na utulivu, tulikuwa jeshini, ulinzi uliimarishwa ukitaka kutoka getini unakutana na mwanajeshi anakurudisha,” anasema.

“Tofauti na wenzetu ukiachana na kambi kwa wachezaji wa Kitanzania kwa kambi kama zile watataka kwenda Copa Cabana kuangalia mji kidogo, hivyo utulivu wa kambi unakosekana.”

Kikosi bora Yanga hiki hapa

Makumbi licha ya kutaja kikosi bora cha Yanga amewataja makocha wawili kuwa ndiyo bora katika maisha yake ya soka.

“Kwanza ni Rudi Gutendorf (raia wa Ujerumani) na Syllersaid Mziray,” anasema.

“Katika maisha yangu ya mpira sijawahi kukutana na makocha wa aina hii. Waliwapenda wachezaji na walijua uwezo wa mchezaji achana na mbinu zao.”

Anasema mbali na makocha, Yanga ya miaka ya themanini ilikuwa na vifaa na kwamba hajawahi kuona ukuta wa Berlin kama ule ulioundwa na Ahmed Amasha, Yussuf Bana, Allan Shomari/Isihaka Hassan ‘Chukwu’ na Athuman Chama ‘Jogoo’ wakiwa na makipa Hamisi Kinye na Joseph Fungo.

Anasema kikosi hicho pia kilikuwa na nyota wengine kama Charles Boniface Mkwasa, Juma Mkambi ‘Jenerali’, Omari Husein na Abeid Mziba.

Mechi za Yanga, Simba

Licha ya utani wa jadi wa timu hizo kongwe kuendelea kushamiri, Makumbi anasema enzi hizi ni tofauti na enzi zao.

“Zamani mechi ya Simba na Yanga ilikuwa ni shamrashamra mwezi mzima mtaani kila kona ndiyo habari ya mjini. Hata wachezaji tulikuwa tunapeana hamasa hatukukubali kufungwa enzi zile,” anasema.

Licha ya kuwepo tetesi kuwa mechi hizo kuna nguvu ya ziada inatumika kwa timu kufanya mambo ya ushirikina, Makumbi anasema hizo ni imani na zinatengenezwa na watu wanaojiita makomandoo.

“Walikuwa wanafanya hivyo ili kutengeneza ulaji wao, lakini si kweli kwamba kuroga kunaweza kukupa matokeo uwanjani. Huko wanakokwenda kuroga ingekuwa ni hivyo basi wangekuwa na timu za Ligi Kuu,” anasema.

Anasema enzi zao licha ya kutolipwa mishahara minono na klabu, faraja yao ilikuwa ni hamasa wanayopewa na mashabiki mitaani.

“Mfano mimi nacheza Yanga lakini nikiwa mtaani shabiki wa Simba ananipa lifti na nikipita sokoni napewa bidhaa bure kutokana na mapenzi ya mpira,” anasema.

Mabao 5-0 yamtoa machozi

Miongoni mwa kumbukumbu mbaya kwa Yanga ni kipigo cha mabao 5-0 dhidi ya Simba mwaka 2012 matokeo ambayo Makumbi anasema yalimtoa machozi.

“Sikuwahi kulia Yanga ikifungwa katika maisha yangu, lakini mabao 5-0 yaliniliza baadaye nikasikia ilikuwa ni mbinu ya kumuondoa Llyoid Nchunga madarakani,” anasema.

“Niliumia kwani mchezaji kama una mapenzi huwezi kukubali ufungwe na Simba eti sababu tu ya kumuondoa kiongozi madarakani.”

Wachezaji wa zamani

Makumbi anasema zamani vipaji vilikuwa vingi ingawa pesa haikuwepo wachezaji walijituma.

“Tulikuwa tunajifua hatukusubiri mazoezi ya kocha kizazi cha mpira cha zamani kilikuwa vizuri ukiachana na mazoezi pia hivi sasa maumbo makubwa ya wachezaji yamepotea,” anasema nguli huyo.

Columnist: mwananchi.co.tz