Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Hivi ndivyo unavyoweza kuzigeuza changamoto za kazi kuwa fursa

75667 Ajira+pic

Mon, 16 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Huenda kuna mambo yameanza kukukatisha tamaa ofisini kwako. Matarajio makubwa uliyokuwa nayo wakati ukianza kazi yameanza kuyeyuka. Sasa una wasiwasi na mustakabali wa ajira yako.

Huna tena ile furaha ya kazi uliyokuwa nayo wakati unaajiriwa. Umeanza kuwa na visingizio vingi vya kutokwenda kazini na hata ukienda kazini unatamani saa za kuondoka zifike. Maisha ya kazi yamekuwa magumu.

Kwenye makala haya ningependa kukushawishi kwa kutumia mifano michache kuelewa kuwa changamoto kwenye maeneo ya kazi zinaweza kuwa kichocheo cha mafanikio yako.

Huna ujuzi wa kutosha?

Huna amani kwa sababu umeshaanza kugundua huna ujuzi wa kutosha? Ulichosoma chuoni sicho unachokitumia ofisini? Je, umeanza kujisikia fedheha kuwa unauliza karibu kila kitu?

Huna sababu ya kuogopa. Tunachokisoma shuleni mara nyingi ni nadharia za jumla jumla kukusaidia kupanua ufahamu wako. Unapoingia kwenye ajira unakuwa na kazi kubwa ya kutafsiri maarifa hayo ya jumla jumla kuwa ujuzi. Kazi hii haifanyiki siku moja.

Pia Soma

Advertisement
Jenga uhusiano mzuri na wafanyakazi wazoefu. Tafuta watu waaminifu wa kukusaidia pale unapokwama. Usione aibu kujifunza mambo mapya.

Unaweza pia kujiandikisha kwenye kozi za muda mfupi baada ya saa za kazi. Vyuo vingi vinaendesha mafunzo kwa njia ya masafa. Uzuri wa mafunzo kama haya ni kwamba unasoma kile unachokihitaji kulingana na mazingira yako.

Unalipwa mshahara mdogo?

Ulipokuwa chuo uliamini maisha yangekuwa rahisi ukipata kazi. Mshahara mnono, posho za hapa na pale. Ulikuwa na mawazo kuwa ndani ya muda mfupi ungenunua gari, ungejenga nyumba yenye hadhi ya msomi na kufanya mambo ya maendeleo.

Leo mwaka wa tano mambo hayaendi. Mshahara hautoshi. Kila mwisho wa mwezi unakukuta ukiwa hoi. Madeni, majukumu yasiyoisha, gharama kubwa za maisha zinafanya ujihisi akaunti yako ya benki inatumika kupitishia mshahara wako kuwafikia wengine.

Usikate tamaa. Mafanikio yanayodumu huwa yanakuja hatua kwa hatua. Unaowaona wamefanikiwa leo wamepambana kwa muda mrefu. Pia, hakuna mtu amewahi kuridhika na mshahara. Siku zote mshahara haujawahi kumtosha mfanyakazi. Ishi kwa malengo wakati huo huo ukitumia vipaji na uwezo ulionao kutafuta fursa ya kujiongezea kipato baada ya saa za kazi.

Unaathiriwa na siasa za ofisi?

Kila ofisi ina siasa za nani ni nani nje ya mfumo rasmi, nini hufanywa na nani, nani hukwamisha mambo, nani mwenye ushawishi wa kusukuma mambo yaende.

Kadhalika kuna namna kampuni na taasisi hujiweka mbele za macho ya umma, wakati mwingine kinyume na uhalisia wake, kwa lengo la kujenga taswira inayowezesha shughuli zifanyike.

Siasa hizi, kwa namna moja au nyingine, zinaweza kumwathiri mfanyakazi mmoja mmoja. Inaweza kutokea, kwa mfano, ukajikuta kwenye upande usiosikilizwa. Jinsia yako, dini, kabila, chuo ulichosoma, mtazamo wako wa kisiasa, marafiki ulionao wanaweza kukufanya ukawekwa upande wa watu wasiokubalika.

Jifunze kusoma mwenendo wa ‘siasa’ za ofisi. Baini watu wenye ushawishi na uone namna gani unaweza kuongeza imani yao kwako. Mbali na kuchapa kazi kwa bidii, fahamu ‘propaganda’ zinazotumika kujenga sifa ya taasisi yako.

Unaonewa na bosi?

Maoni ya mkuu wako wa kazi yana nguvu kubwa ya kuamua mustakabali wako. Mara nyingi vile anavyokutazama ndivyo utakavyokuwa. Huwezi kupanda cheo, kwa mfano, kama kuna namna fulani mkuu wako anaamini hufai.

Kutokupendwa na bosi kunaweza kumaanisha haamini unaweza kazi, haoni namna gani unaweza kuaminiwa kwa majukumu makubwa zaidi na hivyo kukuweka kwenye orodha ya watu wanaopishana na fursa zinazopatikana kwenye eneo la kazi. Unafanyaje?

Jitathmini kwa nini bosi hakupendi. Je, kuna tabia ulizonazo zinamfanya aamini hufai? Je, ni namna yako ya kuzungumza ndiyo tatizo au uwezo wako wa kuhusiana vyema na watu? Badilika. Ikiwa tatizo ni bosi mwenyewe, wekeza muda wako kwenye kazi. Wakati mwingine kuaminika kwako ni matokeo ya jitihada zako za muda mrefu.

Umefukuzwa kazi?

Umepata matatizo umefukuzwa kazi bila kujiandaa. Ulikuwa na mipango mingi binafsi iliyotegemea kazi uliyokuwa nayo lakini ghafla mambo yameharibika. Unafanyaje?

Utulivu ni jambo la muhimu. Usikurupuke kuwachukia watu unaoamini wamehusika na kufukuzwa kwako. Wakati mwingine watu hutumika tu kukuondoa mahali pasipokufaa ili ulazimike kwenda panapokufaa. Usiwe mwepesi kulaumu.

Christian Bwaya ni mhadhiri wa Saikolojia na Unasihi, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Twitter: @bwaya , 0754 870 815

Columnist: mwananchi.co.tz