Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Hivi ndivyo ilivyo safari ya Ezra kuwa daktari wa binadamu

11146 HVI+PIC.png TanzaniaWeb

Tue, 10 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Watanzania wengi wenye ulemavu wa aina mbalimbali wakikosa fursa za elimu kwa sababu ya changamoto mbalimbali, wapo walioamua kupambana na changamoto hili ili kutimiza ndoto walizonazo maishani.

Takwimu za watu wenye ulemavu zilizotolewa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Stella Ikupa bungeni April 11 mwaka huu bungeni, zinaeleza kuwa Tanzania ina jumla ya watu wenye ulemavu 2,641,802 milioni, wakiwamo wasioweza kutembea 525,019.

Katika orodha hii, yumo mwanafunzi Ezra Mwambasi (12), aliyeamua kupambana na changamoto za ulemavu wake na maisha kwa jumla.

Kwa umri wake mdogo akishirikiana kwa karibu na wazazi wake, ameamua kupambana vilivyo na changamoto ya elimu ambayo kwa walemavu wengi imekuwa mzigo mzito kwao.

Ezra anayesoma dasara la tano katika Shule ya msingi Lufulu… iliyopo wilayani Kilombero, anaeleza kuwa baada ya kujitambua kuwa yeye ni mlemavu, hakuweza kukata tamaa katika masomo yake licha ya kukutana na misukosuko mbalimbali nyumbani na shuleni.

Hakukata tamaa kwa kuwa ndani ya nafsi yake kuna wito na shauku inayomsukuma kuwa daktari bingwa wa kutibu magonjwa ya binadamu.

“Ndoto yangu kubwa ni kuwa daktari wa binadamu, napenda kuwa daktari kwa sababu napenda kuwatibu wagonjwa. Nikimuona mgonjwa nashikwa na huruma sana; hilo linanisukuma kupenda taaluma ya udaktari kutoka moyoni mwangu,’’ anasema Ezra akiwa na sura inayoonyesha tabasamu tabasamu siku alipozungumza na mwandishi.

Ndoto ya udaktari na wito alionao wa kuvunja mwiko wa dhana kuwa walemavu ni watu wasiojimudu, vimekuwa vikimpa msukumu wa kufanya vizuri katika masomo yake. Anasema tangu alipoanza darasa la kwanza mwaka 2014 hadi sasa amekuwa akishika nafasi ya kwanza darasani.

“Namshukuru baba kunipeleka shuleni, nawashukuru walimu na wanafunzi wenzangu kwa moyo wao wa upendo kwangu kwa namna wanavyonipenda na mimi nafarijika, japo wakati mwingine najiona nina upungufu wa kimaumbile lakini haunikatishi tamaa.”anaeleza.

Baba mzazi azungumza

Baba mzazi wa Ezra, Amon Mwambasi, anaeleza kuwa mwanawe alizaliwa Septemba 24 mwaka 2006 akiwa na ulemavu wa miguu.

Kabla ya kumuanzisha shule, anasema alianza kumfundisha masomo ya awali nyumbani kwa muda wa miezi sita na januari mwaka 2014 alianza masomo rasmi ya darasa la kwanza.

“Ezra amekuwa mtoto anayependa kujifunza mambo kila kukicha na kuchezea vifaa hasa vinavyotumia umeme au betri,” anasema na kuongeza;

‘’Kwa mfano, amekuwa akiunganisha vifaa vinavyotumia umeme vilivyoharibika kama redio, vifaa vya umeme wa jua na kuvitengeneza na baadaye hufanya kazi.’’

Ezra apata baiskeli

Tangu mwaka 2014 Mwambasi anasema amekuwa na kibarua cha kubeba mwanawe kwenda na kurudi shule kwa kuwa hakuwa na uwezo wa kumnunulia baiskeli maalumu ya kutembelea.

“Baada ya kuanza shule ya msingi mwaka 2014 nimekuwa nikimbeba Ezra mgongoni na kwenye baiskeli na ikitokea naumwa basi siku hiyo hawezi kwenda shule,’’ anasema.

Hata hivyo Mei mwaka huu, Ezra akapata wasamaria wema walioongozwa na mwandishi wa makala haya, ambaye kwa kushirikiana na wenzake walimwondolea kero hiyo kwa kumtengenezea baiskeli maalumu ya kutembelea.

Mwambasi anaeleza kuwa kabla ya kupata baiskeli, Ezra muda mwingi alikuwa nyumbani; hakuweza kwenda sehemu nyingine kutokana na mazingira yake, lakini sasa atakuwa na fursa ya kwenda kanisani, shuleni na kutembelea ndugu na jamaa bila ya msaada wa mtu mwingine.

‘’Milango ya neema kwa Ezra imeanza kufunguka, kilichobakia ni yeye kutimiza ndoto zake kwa kukazania masomo na kufikia malengo yake,’’ anasema Mwambasi mwenye jumla ya watoto tisa.

Mwalimu wake amzungumzia

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Lufulu, Fadhil Mkhoi anasema kuwa Ezra amekuwa akifanya vizuri katika taaluma tangu akiwa darasa la kwanza.

Hata hivyo, kilio cha Mkhoi ni shule hiyo kutokuwa na mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu kama Ezra.

“Mazingira ya shule sio rafiki kwa Ezra kutokana na hali yake ya ulemavu hasa upande wa vyoo. Hiyo imekuwa changamoto kubwa kwake kutokana na kutopatiwa ufumbuzi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu,”anasema na kuongeza:

‘’Licha ya changamoto za kimazingira na kimwili amekuwa mwanafunzi anayefanya vizuri darasani kwa kushika nafasi ya kwanza na mtihani darasa la nne kuingia darasa la tano ameshika nafasi ya nane katika wilaya yetu ya Kilombero.”

Ezra na maendeleo ya taaluma

Katika matokeo ya kuingia darasa la tano mwaka 2018, Ezra alipata ufaulu wa jumla wa alama B, akiwa na mgawanyo ufuatao wa alama za kila somo; Hisabati- A, Kiswahili – A, English - B Maarifa ya Jamii – B, Sayansi – C, Haiba na Michezo – C.

Awali, katika matokeo ya mitihani ya upimaji wa darasa nne kwa ngazi ya wilaya, Ezra alishika nafasi ya nane kati ya watahiniwa 8788 kutoka shule 132 za Wilaya ya Kilombero.

Uongozi wa wilaya

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero James Ihunyo, anasema tayari ameagiza shule zote zinazojengwa sasa zizingatie mahitaji ya watu maalumu wakiwamo walemavu, huku akishangazwa na hatua ya viongozi kushindwa kutatua changamoto ya usafiri kwa mtoto huyo.

Columnist: mwananchi.co.tz