Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Hivi BMT mna habari kuna vyama havina akaunti!

23484 Bmt+pic TanzaniaWeb

Mon, 22 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Duniani kote kampuni kubwa huwa na sera za kusaidia au kuwekeza katika sekta ya michezo na hapa nchini kuna baadhi yana sera kama hiyo.

Uwekezaji au udhamini kama huu husaidia wanamichezo kufanya vizuri katika michezo ambayo inahitaji fedha nyingi katika maandalizi yake.

Katika nchi ambazo makampuni yamewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye michezo, maendeleo yameonekana hasa ukizingatia sekta hiyo ni moja ya kiini cha kuzalisha ajira kwa vijana wengi.

Hata hivyo ukitupia macho hapa nchini unaweza kuona pengo kubwa la ukaribu kati ya Wadhamini, Klabu, Mashirikisho na vyama mbalimbali vya michezo kwani zipo sababu nyingi zilizotenganisha maeneo hayo, lakini zaidi ni wadhamini kutokuwa tayari kuwekeza maeneo yasiyokuwa na tija kwao.

Wadhamini ambao ni kampuni zinaona viongozi wa Mashirikisho na Vyama mbalimbali vya michezo hawana mipango na nia ya dhati ya kuzitumikia nafasi hizo kuleta maendeleo katika michezo, hali inayosababisha Mashirikisho na vyama mbalimbali vya michezo kukosa wadhamini.

Pia, wadhamini wanaona Mashirikisho na Vyama mbalimbali vya michezo vinashindwa kutoa ripoti za mapato na matumizi kila mwaka na viongozi hawaandiki mapendekezo ya kuyashawishi makampuni kutoa udhamini.

Kampuni ili iweze kudhamini inataka taarifa za benki (bank statement), kanuni za fedha (financial regulations), akaunti zilizokaguliwa (audited account) na mipango ya biashara (business plans).

Tatizo kubwa ni kwamba baadhi ya Mashirikisho na Vyama vya michezo havina akaunti za uendeshaji, vinatumia akaunti za watu binafsi katika kuweka na kupokea fedha zinazotumika katika uendeshaji wa shughuli za Mashirikisho na Vyama vya Michezo hapa nchini.

Kutokana na hali hiyo, hivi karibuni, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) lilitoa mwongozo wa kuendesha shughuli za michezo katika Mashirikisho na Vyama vya Michezo Kitaifa, ambapo mwongozo huo ulibainisha mambo manne ya kuzingatia katika uendeshaji wa shughuli za Mashirikisho na Vyama vya Michezo nchini. Mambo hayo ni: Kuwa na Ofisi na Anuani ya Makazi, Umiliki wa Akaunti za Benki, Mpango Kazi na Bajeti, na Misingi ya Utawala Bora.

Unaweza kuona, kati ya mambo hayo manne kuna suala la umiliki wa akaunti za benki, yaani sina hakika sana kama Baraza linajua kuna baadhi ya mashirikisho na vyama vya michezo nchini vinatumia akaunti za watu binafsi katika kuweka na kupokea fedha zinazotumika katika uendeshaji wa shughuli za mashirikisho na vyama vya Michezo.

Tatizo hili, limesababisha ukaguzi wa hesabu za mapato na matumizi ya mashirikisho/vyama kutokuguliwa (Auditing) jambo ambalo ni kinyume na Sheria ya Baraza ambayo inayataka mashirikisho na vyama vya michezo kuwasilisha taarifa za ukaguzi wa hesabu kwa Msajili wa Mashirikisho na Vyama vya Michezo nchini.

Hii ina maana kwamba baadhi ya mashirikisho na vyama vya michezo havifanyiwi ukaguzi hali inayosababisha hata wadhamini kushindwa kutoa fedha zao kwa ajili ya kuendeleza michezo husika.

Ni kweli, ushindani wa wanamichezo huonekana uwanjani, lakini ni wazi kuwa wadhamini wana nafasi kubwa ya kuleta ushindani uwanjani kwa fedha watakazotoa.

Ni matumaini yangu BMT itaweka wazi ni mashirikisho gani au vyama vya michezo gani au klabu gani ambazo hazina akaunti au hata kama zina akaunti ni klabu gani ambazo hazifanyiwi ukaguzi, pia ni klabu, mashirikisho au vyama vya michezo gani?

Columnist: mwananchi.co.tz