Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Hisabati si janga, ni dawa ya Taifa

48693 Hisabat+pic

Tue, 26 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mkurugenzi wa Idara ya Elimu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi) Julius Nestory amewafunda wanafunzi akiwaeleza kuwa hesabu sio ugonjwa wa Taifa kama wengi wanavyodhani isipokuwa ni dawa ya taifa.

Alisema sababu moja wapo ya wanafunzi wengi kufeli somo hilo ni dhana finyu kuwa hesabu ngumu na ni kama ugonjwa wa taifa, ilhali hakuna maisha bila hesabu.

Kwa zaidi ya miaka 10 mfululizo ufaulu wa hesabu kwa shule za sekondari upo chini ya asilimia 20 na hivyo kulifanya somo hilo kuwa la mwisho kila matokeo yanapotangazwa.

Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya Hisabati duniani yaliyoandaliwa na Chama cha Hisabati Tanzania (Chat/Chahita), Nestory alisema hesabu ni dawa kwa sababu hakuna maendeleo yoyote pasipo hesabu.

“Kama kuna mtu alikuwa anawaambia kuwa hesabu ni ugonjwa wa taifa, ukitoka hapa nenda kaanze kusoma kwa bidii. Hesabu ni dawa sio ugonjwa wa Taifa,” alisema.

Alisema mtu anaweza kuishi bila kujua kusoma wala kuandika, lakini hawezi kuishi bila kujua hesabu kwa sababu maisha yake yamezungukwa na ufanyaji wa mahesabu.

“Ukiamka utapiga hesabu ya chakula kiasi gani kinawatosha watoto wako, hesabu ni maisha na ni muhimu somo hili lipatiwe kipaumbele,” alisisitiza Nestory.

Mkurugenzi huyo wa elimu aliwataka wanafunzi kuwekeza kwenye hesabu akidai kuwa ni mkombozi wao sio tu baada ya kumaliza masomo yao lakini hata katika kuongeza ufaulu darasani.

“Kwa hiyo watoto tuokoeni wazee kwa kusoma hesabu. Ili Tanzania isiwe ombaomba kwa mataifa tajiri, lazima watoto wetu muwekeze kwenye hesabu. Hivi mlishawahi kusikia mtu ameenda mwezini bila kujua hesabu? Kwa nini basi tunapanda pikipiki kutoka China na ndege kutoka nchi za watu” alihoji kiongozi huyo.

Alisema lazima kuwe na mkakati wa kuhakikisha wanafunzi wanapenda kujifunza hesabu ili kuleta mageuzi ya somo hilo.

Aliwataka walimu kutokuwa sababu ya kuzalisha hofu kwa wanafunzi kuchukia Hisabati, badala yake wawafundishe kwa upendo. Alisema Serikali inaendelea kushughulikia changamoto mbalimbali zinazofanya somo hilo kudorora ikiwamo uhaba wa walimu.

Mbinu ufaulu wa hesabu

Awali Mwenyekiti wa Chat/Chahita Dk Said Sima alisema zipo njia zinazoweza kusaidia katika kuinua ufaulu wa somo hilo.

Alishauri Serikali kuhakikisha kuwa walimu wa Hisabati wanapomaliza masomo, wasichukue uamuzi wa kwenda kufanya kazi kwenye sekta nyingine kutokana na kucheleweshewa ajira serikalini.

“Pia nashauri kuwapo kwa mpango wa kutumia wahadhiri na wanafunzi wa vyuo vikuu hasa siku za likizo na mwisho wa wiki. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tulijaribu kufanya hivyo tukafanikiwa kuongeza ufaulu kwa shule zilizokuwa zimeshika mkia mwaka jana hapa Dar es Salaam,” alieleza.

Dk Sima alisema kutokana na mzigo mkubwa walio nao walimu wa Hisabati shuleni, upo umuhimu wa kupewa motisha ili kuwaongezea ari ya kufundisha.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Aga Khan, Veronica Sarungi alisema walimu wanapaswa kuandaliwa mafunzo wakiwa kazini ili kuwaongezea ujuzi wa kufundisha somo hilo.

Alisema kufeli kwa wanafunzi kunatokana na baadhi ya walimu kutokuwa na ujuzi wa kufundisha somo hilo, huku wengi wao wakifundisha nadharia bila vitendo.

“Naungana na wanaosema hesabu sio ngumu, hili ni somo rahisi ila ugumu unakuja mtu asipojua afanye nini kufanya hesabu fulani. Hesabu ni kama ujenzi wa nyumba lazima uanze kitu hiku, kifuate kingine kwa mpangilio,’’ Alifafanua.

Baadhi ya wanafunzi wa shule za sekondari na msingi waliohudhiria maadhimisho hayo, walisema Siku ya Hisabati inapaswa kupewa kipaumbele kama ilivyo siku ya wanawake, ili kuijengea jamii msingi wa kupenda hesabu.

Columnist: mwananchi.co.tz