Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Hiki ndicho kilichopunguza ajali Dodoma

Mon, 23 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ajali za magari barabarani huleta hasara za aina mbalimbali kwa Taifa, kazini, familia, wami-liki wa magari, ndugu na jamaa za waathirika.Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), moja ya malengo endelevu ya dunia ni kupunguza nusu ya vifo vitokanavyo na ajali ifikapo mwaka 2020. Inadaiwa kuwa kupunguza mwendo kwa asilimia tano kunasaidia kupunguza uweze-kano wa kutokea ajali kwa asilimia 30.

Pia, inaelezwa kuwa kuendesha gari kwa mwendo kasi usioendana na miundombinu ya barabara husika, kunachangia kwa kiasi kikubwa ajali nyingi zilizosababisha vifo na watu kupata majeraha.Nchi za Ulaya, Amerika Kaskazini na Australia zilifanikiwa kupunguza ajali baada ya miongo mingi ya kutumia mfumo wa mbinu salama wa kutekeleza, kuheshimu, kudhibiti na kutoa adhabu kali za kudhibiti makosa ya usalama barabarani.Nchini Tanzania, ajali zitokeapo,

Jeshi la Polisi - Kikosi cha Usalama Barabarani - huwakamata madereva na kuwafungulia mashtaka na wakati mwingine wamiliki wa vyombo husika vya moto.Hata hivyo, licha ya maeneo mengi ya nchi kukumbwa na matukio ya mara kwa mara ya ajali kama ilivyotokea kwa Mkoa wa Mbeya katika siku za karibuni, Dodoma ajali zimetajwa kupungua kwa asilimia 14, huku trafiki makao makuu ikieleza chanzo cha mafanikio hayo.

Kaimu Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani (RTO) Mkoa wa Dodoma, ASP Swaleh Digega anasema ikilinganishwa na mwaka 2017, mwaka huu ajali zimepungua kutokana na mikakati ambayo waliweka kuboresha usalama barabarani.

Digega ambaye ni mratibu msaidizi wa polisi, anasema, “Katika Mkoa wa Dodoma tumejitahidi kupunguza ajali kwa kiasi kikubwa. Kwanza tulianza kupambana na madereva wa mabasi wenye mwendokasi, tukiwakamata tunawaweka mahabusu na baadaye mahamakani. Tulifanya hivyo hata wa magari madogo pia.”

Digega anasema changamoto ambayo wamekuwa wakikutana nayo ni madereva wa Serikali ambao wamekuwa wakikiuka sheria za usalama barabarani.

“Tangu Serikali imehamia Dodoma hawa madereva wapo kule Udom (Chuo Kikuu cha Dodoma), wengi tunawakamata sababu eneo lile wanatakiwa kutembea spidi 50, lakini wanakimbiza kwenye ule mlima na wakati mwingine wanakuwa na mabosi wao tunawatoza.

“Sisi tunashtaki madereva hatumshtaki waziri, mbunge au kiongozi yeyote wa Serikali. Ndiyo maana leseni inayotolewa hapa nchini ya udereva ni moja haina Polisi, Magereza wala kiongozi mkubwa.”

Anasema kufuatia hilo, waliamua kuweka sheria ya kuwaweka mahabusu wale wote waliorudia makosa na ikibidi kufikishwa mahakamani, jambo linalowafanya madereva kuheshimu sheria za usalama barabarani wawapo mkoani humo.

Miundombinu

Akizungumzia miundombinu, anasema hakuna barabara zenye mashimo na hata madereva wa bodaboda wamedhibitiwa pia.

“Kwa bodaboda, tunashikirikana na wenyeviti wao, ukiangalia barabarani karibu kila pikipiki ina kofia ngumu, haya ni matokeo ya semina tuliyowapa viongozi wao. Hata hivyo, tukimkamata bodaboda hajatimiza masharti na ana abiria zaidi ya mmoja tunampeleka mahakamani,” anasema.

Ofisa Operesheni wa Trafiki Mkoa wa Dodoma, Josephat Mjema anataja takwimu za jumla katika kipindi cha mwaka 2017 kuwa ajali zilizotokea ni 23.

Anasema vifo vilivyotokana na ajali vilifikia 50. Wanaume waliofariki dunia walikuwa 43 na wanawake saba.

Mjema ambaye ni mkaguzi msaidizi wa polisi anasema, “Hata ukifuatilia hakuna ajali kubwa iliyotokea sasa, ni mtu mmojammoja na hilo tulikuwa tumeungana wilaya zote kuanzia yanayotokea Gairo, Morogoro tunapeana taarifa.”

Pia anasema ukaguzi wa kushtukiza unaofanyika katika maeneo mbalimbali umesaidia kupunguza ajali hizo.

Anasema pia wameanzisha mawasiliano ya pamoja kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp na huo unawasaidia kupambana na wahalifu wa usalama barabarani kwa wakati.

Katika Malengo ya Milenia inaelezwa kwamba kutungwa na kutekeleza kwa sheria zinazodhibiti kiwango cha kilevi kwa madereva, kutasaidia kupunguza idadi ya ajali zinazosababishwa na ulevi kwa asilimia 20.

Sheria inayoweka mkazo wa dereva kuwa na kiwango cha kilevi ni 0.05g/dl au chini ya 0.05g/dl katika damu ya dereva.

“Wenye makosa ya ulevi tulianza kwa kuwalaza ndani badala ya faini. Tukiona halina uzito analipa faini ya Sh90,000 na tunamuachia, akirudia ni mahakamani haina msamaha. usumbufu anaoupata akitoka pale harudii na wapo tuliowafunga.

“Leseni unafungiwa mpaka kesi yako itakapoisha mahakamani na kwa kutumia kifungu cha 23, tunamfungia na haruhusiwi kuendesha gari kwa wakati huo. Hii inasaidia kupeleka meseji kwa watu wengine na pia imetusaidia hata ajali Dodoma hazipo tena,” anasisitiza Mjema.

Anasema kuwapa hofu madereva kumesaidia na kama mtu anaendesha gari anajua wakati wowote anaweza kupimwa kilevi.

Ofisa huyo anasema wamekuwa wakitoa elimu katika stendi za mabasi kila alfajiri. Kila basi linapata elimu kwanza na kisha kutoa namba za polisi. Baada ya hapo wanahakikisha kwamba kila abiria amefunga mkanda.

Mjema anasema ukaguzi wa magari unapofanyika kama hakuna mikanda wanatoa namba za usajili wa gari kumfanya mmiliki atengeneze kwa wakati gari kisha anarudishiwa namba zake anaingia barabarani.

Hata hivyo, anasema wanapambana na madereva wa bodaboda ambao hawafuati sheria za barabarani na pindi inapotokea wakawakamata zaidi ya mara moja huchukua vyombo vyao vya usafiri.

“Kuna taratibu ambazo hufanyika na iwapo mhusika hatajitokeza kuchukua pikipiki yake zaidi ya miezi sita kituoni tunatangaza kuzipiga mnada kisheria, hakimu akiidhinisha zipigwe mnada tunafanya hivyo,” anasema huku akionyesha bodaboda zinazotarajiwa kupigwa mnada zilizopo katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini humo.

Nchi zilizofanikiwa

Nchini Urusi, utekelezaji wa sheria kali na kampeni za vyombo vya habari umesaidia kuongeza viwango vya uvaaji wa mikanda kati ya mwaka 2010 na 2013. Mjini Lipetsk Oblast kiwango kimeongezeka kutoka asilimia 50 hadi karibu asilimia 80.

Katika mji wa Ivanovo Oblast, kiwango kimeongezeka kutoka asilimia 50 hadi asilimia 90. Hata matumizi ya vizuizi vya watoto yameongezeka kwa mara nne zaidi katika mji wa Oblast kutoka asilimia 20 hadi asilimia 80.

Nchini Vietnam, serikali ikishirikiana na WHO imeendeleza kampeni ya kuboresha sheria na kanuni za usalama barabarani kutoka mwaka 2007.

Nchi hiyo imeendelea kuhimiza uvaaji wa kofia ngumu kwa waendesha bodaboda na sheria pia inawawajibisha wazazi kuhakikisha kwamba watoto wao wanavaa kofia ngumu wanapokuwa abiria au kuendesha pikipiki. Pia kumekuwapo na ongezeko la faini.

Wizara inasemaje?

Mkurugenzi msaidizi wa Kitengo cha Dharura na Maafa wa Wizara ya Afya, Dk Elias Kwesi anasema licha ya uwepo wa changamoto katika namna ambavyo vyombo vya habari vinaripoti masuala ya usalama barabarani, kuna changamoto pia kwenye takwimu.

Anasema watu 4,000 hufariki dunia kila mwaka nchini, lakini bado watu wengi zaidi hawajaweza kufikiwa kitakwimu.

“Takwimu za WHO zinakadiria watu 16,000. Kuna ajali ambazo zinatokea hatupati takwimu zake, ni vigumu kupata takwimu sahihi za ajali hasa watu waliokufa na majeruhi ni kiasi gani,” anasema Dk Kwesi.

Anasema takwimu hizo hupatikana kupitia wale wanaoripoti kwenye vituo vya polisi lakini wengine hawapatikani, hivyo lengo la wizara kwa sasa ni namna ya kuboresha upatikanaji wa takwimu.

Hata hivyo, anasema vyanzo vya ajali nyingi ni tabia na mwenendo wa dereva, matumizi ya simu, kutofunga mikanda na mwendokasi ambao huchangia asilimia 16 ya ajali zote nchini.

“Watu wanasafiri, wanasimama wanakunywa pombe, wanaendelea na safari na tabia ambazo zimechangia ni kutokufunga mkanda. Watu hawafungi mikanda, magari hayana mikanda, wengi wanakufa kutokana na kutofunga mkanda,” anasema Dk Kwesi.

Columnist: mwananchi.co.tz