Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Hii ‘michambo’ kwenye mitandao inatengeneza kizazi chenye ‘wagonjwa wa akili’

12623 Julie+kulangwa TanzaniaWeb

Sat, 18 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Anayeweza kuelezea maumivu ya kushambuliwa mtandaoni ni yule aliyekumbwa na mikasa ya aina hiyo. Wengine tunabaki kusimulia tu lakini kwa kujaribu kuvaa viatu vya mtu aliye katikati ya msuto katika mitandao unajua kwa kiasi gani inasababisha vidonda visivyopona.

Hakuna haja ya kuwataja majina lakini orodha ni ndefu ya watu waliowahi kukumbana na mashambulizi katika mitandao. Maisha yao baada ya ‘michambo’ huenda ni tofauti na mwanzo.

Unyanyasaji kwenye mitandao (cyber bullying) si jambo geni duniani kote ila hapa kwetu inaweza kuwa inavunja rekodi. Kama ambavyo Watanzania wanaongoza kwa ushapu wao katika mitandao ya kijamii, ndivyo walivyo katika kuwashughulikia watu.

Mimi nimelitazama kwa namna nyingine na kuona haya mambo yanayoendelea katika mitandao ya kijamii yasipodhibitiwa yatatengeneza kizazi cha ajabu…kizazi cha watu wenye matatizo ya akili.

Kwa mfano sasa ni rahisi mtu yeyote kuwa maarufu akitaka. Atapiga picha za utupu, atazitupia katika mitandao ya kijamii mara paap jamii imempokea amekuwa maarufu. Mwingine anajirekodi akifanya mambo ya ajabu ajabu yasiyo ya staha hata kidogo, siku mbili naye katoboa kawa maarufu.

Lakini hiyo si mbaya zaidi kama watu kushambuliwa wenzao katika mtandao kwa matusi ya nguoni na kashfa za kukosoa za kila aina. Watu wamesahau kama mwenye kazi ya kuumba watu ni Mungu maana wanavyokosoa huko mitandaoni utasema kuna mtu anauwezo wa kuchagua anavyotaka awe.

Mtu anaweza kushambuliwa kwa matusi na kashfa zote mpaka unajiuliza upo nchi gani maana unayoshuhudia huko si ya nchi hii kabisa.

Mimi natazama namna watu wanaokumbwa na manyanyaso hawa wanavyobadilika baada ya mashambulizi. Hakika watu hawa pamoja na kwamba mbele ya macho yetu wanajikaza, naamini wanatetereka na kupata msongo wa mawazo.

Huenda hata staili yao ya maisha inabadilika baada ya kupitia manyanyaso na kama wakifuatiliwa huenda wanaweza kukutwa wamepata sonona. Jaribu kuvaa viatu vya mtu anayeshambuliwa mtandaoni halafu vaa viatu vyake.

Nawaona watu wengi wakipatwa na ‘magonjwa ya akili’ kutokana na utamaduni tunaouendekeza mitandaoni wa kuumbuana.

Columnist: mwananchi.co.tz