Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche amesema ili kufanikiwa kupata uongozi bora na siasa safi nchini Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi haziepukiki.
Heche ametoa kauli hiyo leo Jumamosi, Julai 23, 2022 kwenye kongamano la kudai Katiba Mpya, Tume Huru na Uchaguzi, wilayani Magu huku akisema chama hicho kitaendelea kupambana hadi katiba na tume huru ya uchaguzi ipatikane kabla ya mwaka 2024.
Amesema hata nchi zilizoendelea duniani zilianza kwa kupata Katiba Mpya iliyochangia kuleta uongozi bora na siasa safi inayoruhusu upinzaji wa hoja ndiyo maana zilifanikiwa kupata maendeleo hayo.
Huku akionyesha kushangazwa na ukosefu wa ajira kwa vijana, Heche ametupa lawama kwa viongozi kuchangia uwepo wa changamoto hiyo huku akisema iwapo vyama vya upinzani vikipewa nafasi ya kutoa mapendekezo kuna uwezekano changamoto ya ajira kwa vijana ikatokomezwa nchini.
Kuhusu mfumuko wa bei za bidhaa unaoikumba nchi, Heche amesema unachangiwa na kukosa uongozi bora unaoweza kutumia rasilimali zilizopo kujitosheleza kwenye uzalishaji na mahitaji.
"Bidhaa zinapanda bei kila siku, sukari, sabuni, vyakula, mafuta ya kupikia hadi zao la Pamba limeshuka bei sasa unajiuliza Pamba inashukaje bei wakati mahitaji ya muhimu ya mwanadamu ni pamoja na mavazi na pamba ndiyo inayotumika hapa ukiangalia kwa undani unakuta kwamba tatizo ni uongozi," amesema
Advertisement Ili kukabiliana na changamoto hizo, Heche ameishauri serikali kuongeza uwezo wa kuuza bidhaa nje (exportation) kuliko kuagiza kutoka nje ili kuongeza mapato na fedha za kigeni ambazo alitaja kwamba zitachangia kuimarisha uchumi na kushusha bei ya bidhaa nchini.
Ameongeza, "Ili tuweze kuuza nje (exports) lazima tuzalishe kwa wingi kwa hiyo serikali isikwepe kuwekeza kwenye kilimo na uzalishaji ili tuweze kuzalisha vya kutosha na tuuze nje ya nchi. Tutumie rasilimali maji na ardhi tuliyonayo ili tuachane na dhana ya kuagiza hadi chakula tunachoweza kuzalisha nchini kutoka mataifa ya nje."
Kwa upande wake, Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zakaria Obadi amesema chama hicho kitaendelea na msimamo wake wa kushiriki katika uchaguzi mkuu na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ujao pale Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi itakapokuwa imepatikana.
"Tuna kazi ya kufanya maandalizi ya ujenzi wa chama na kushinikiza ajenda za Chadema ambazo ni kuwa na Katiba na Tume Huru ya Uchaguzi kabla ya mwaka 2024," amesema Obadi