Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Hapa Tamisemi wanakwepaje lawama kwa mfano

14111 Ibra+Bakari TanzaniaWeb

Mon, 27 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katika eneo ambalo limesahaulika ama halipewi sana uzito, ni hili la michezo. Kama chama cha michezo hakikuchangamka, basi kisitarajie kama kutakuwa na mkono mwingine wa kuwabeba.

Ukiachana na vyama vya michezo au mashirikisho, iko tofauti katika maeneo mengine. Mfano, ninachofahamu katika Michezo ya Shule za Msingi na Sekondari, inaratibiwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Tamisemi.

Napongeza katika hili. Michezo imekuwa ya ufanisi, nafahamu kuna kasoro, na inafahamika kwamba palipo na wengi si lazima mambo yote yasimame kwenye mstari.

Mikoa imekuwa ikitengeneza timu zake na Tamisemi inamaliza mchezo mzima kwa michezo ya fainali ambayo ndiyo ngazi ya taifa.

Michezo hiyo inafanyika na ndiyo tunayoiona Serengeti Boys hii inayotesa kwenye Michuano ya CAF-Cecafa inayoendelea na tuliambiwa wakati ule inafanyika Mwanza kuwa wachezaji kadhaa watachomekewa. Safi, hapa kazi imefanyika kwa hivyo tulivyoambiwa.

Pamoja na yote, kuna jambo moja nimeliona nataka kulisemea, Tanzania kushindwa kupeleka Rwanda wanamichezo wa Shule za Sekondari kwa michezo ya shule kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati iliyomalizika huko wikiendi iliyopita.

Mashindano hayo yalifanyika Musanze nchini Rwanda, huku Kenya ikitwaa ubingwa wa jumla. Wakenya waliendeleza rekodi yao ya kutawala kanda hii kwa kufanya vizuri katika mashindano haya ya 17.

Kenya ilitwaa medali 28, kati ya hizo 10 za dhahabu, nane za fedha na 10 zingine za shaba wakati Uganda ilimaliza nafasi ya pili, walinyakua medali tisa za dhahabu, 10 za fedha na sita za shaba.

Wenyeji Rwanda walimaliza wa tatu na medali 16; nne za dhahabu, tano za fedha na saba za shaba.

Ilinisikitisha kusikia Tanzania haikupeleka wanamichezo wake ambao tuliwatengeneza katika Umitashumta na Umisseta mbili zilizofanyika Mwanza.

Mbali na Tanzania, mataifa mengine ya Afrika Mashariki ambayo hayakushiriki pia ni pamoja na Burundi na Sudani Kusini ambao walijiondoa kwa sababu zao za kibinafsi.

Ninakumbuka Kenya waliwahi kuandaa Tanzania ikapeleka wanamichezo wake na ilitumia pia michezo ya 2014 mashindano yaliyoandaliwa nchini Tanzania.

Ninachotaka kusema hapa ni kwamba tumewanyima haki wanamichezo wetu ambao ni wanafunzi kwenda kuonyesha umahiri wao.

Kama inavyoeleweka ni kwamba Michezo ya Umisseta ndiyo ya kutengeneza njia ya wanamichezo wa kutoka katika maeneo mbalimbali Tanzania.

Mfano, michezo huanzia ngazi ya wilaya hadi mkoa, sasa, hapo wanapatikana wanamichezo wa moja kwa moja.

Nakumbuka gazeti hili ndilo lililopeleka mwandishi wa kuripoti michezo hiyo Mwanza, Umisseta na Umitashumta na aliripoti rekodi mbalimbali kuvunjwa.

Kuna mikoa ilitengeneza rekodi zake, wanamichezo walifanya maajabu na wapo ambao vipaji vilionekana.

Sasa wale walitakiwa kwenda kuonyesha kweli wana vipaji, walitakiwa kwenda kuonyesha kuwa waliowateua hawakukosea.

Kenya wametwaa ubingwa wa jumla, Uganda na Rwanda ya tatu, ninaamini Tanzania ingekuwa ya kwanza na kuendeleza ubabe wa ukanda huu wa Afrika Mashariki kwani Kilimanjaro Queens mabingwa, Serengeti Boys mabingwa, Azam FC mabingwa hata hawa wangekuwa mabingwa tu. Kwa hapa Tamisemi wanakwepaje lawama?

Columnist: mwananchi.co.tz