kukosa utulivu na umakini au kuwa na uchangamfu uliopitiliza ni hali inayowakuta baadhi ya watoto ambao huwaathiri katika maeneo mbalimbali ya kiutendaji au ukuaji.
Kama hali hii itabainika inahitaji msaada wa kitaalamu kutoka kwa madaktari ambao wanweza kumtambua mtoto mwenye hali hiyo. Ili mtoto ajumuishwe katika kundi la waliokosa utulivu, wataalamu huangalia mjumuiko wa dalili zifuatazo; Moja ni kukosa umakini.
Mtoto mwenye umri chini ya miaka 12 akionyesha mkusanyiko wa dalili sita kati ya hizi zilizotajwa hapa chini ndani ya miezi sita, ataweza kujumuishwa kama mtoto aliye na hali ya kukosa umakini.
Mara nyingi huwa ni mtoto ambaye anakosa uwezo wa kuzingatia kwa kadiri taarifa anazoambiwa au kuonyeshwa na kuzipa uzito unaostahili.
Hufanya makosa madogo madogo yanayoweza kuepukika katika kazi za shuleni, nyumbani au kwenye shughuli nyingine.
Jambo hili husababisha watu kudhani mtoto huyo anakosa umakini katika ufanyaji wa shughuli zake za kila siku na kumuona kama asiyejali.
Pili, mtoto anakuwa na changamoto ya kudumisha utulivu na kuzingatia kufanya jambo moja kwa wakati. mfano; anaweza kutoonyesha yali ya kuzingatia na kufuatilia kinachofundishwa na mwalimu darasani, hali inayomfanya aweze kuhama kimawazo kwa urahisi pale anapoona ama kusikia jambo lingine tofauti na anachofundisha mwalimu. Akiwa anazungumza na mtu mwingine huwa hafuatilii maongezi yamalizike na hushindwa kufuata maelekezo aliyopewa hadi mwisho.
Mtoto wa aina hii mara nyingi hushindwa kumaliza kazi anazopatiwa na walimu darasani na zile za nyumbani. Mfano anaweza akaanza kuosha vyombo lakini gafla akaviacha akaanza kufanya jambo lingine.
Tatu ni kwa mtoto huyo kukosa uwezo wa kupangilia kazi, majukumu na vitu vyake katika muundo unaoeleweka. Mara nyingi huweka vitu hovyo na hushindwa kuzingatia muda na ratiba iliyopangwa.
Wengine huamua kujiepusha na kazi au mambo yanayohitaji utulivu na matumizi ya uwezo wa kufikiri.
Mfano kushindwa kufanya kazi za shuleni au nyumbani, kutojihusisha na michezo yenye sheria, taratibu na hatua nyingi kama vile kombolela, rede inayohitaji kufuata utaratibu. Mara nyingi hupoteza vifaa muhimu vinavohitajika kukamilisha kazi.
Kwa mfano kupoteza kila mara vifaa vya shule kama kalamu, madaftari na funguo za nyumba
Pia huwa na tabia ya kuchukulia jambo kirahisi linaloendelea pembeni wakati akiwa anafanya jambo jingine.
Huwa pia na tabia ya kusahau kirahisi kufanya shughuli za kila siku. Mfano hujisahau kujifanyia usafi wa
wake wa mwili, wa nyumbani na kwenda shule.
Kukosa umakini na kuwa mchangamfu na msukumo wa kutenda jambo kulikopitiliza.
Tunapozungumzuzia kukosa umakini kuwa na mchangamfu kulikopitiliza ‘Hyperactivity’ inamaanisha tabia au hali inayoonyeshwa na mtoto huyo kwa kufanya mambo katika hali isiyotarajiwa. Hali hii katika jamii hutafsiriwa ni tabia ya kuhangaika bila kutulia anapofanya jambo moja, hivyo husababisha uharibifu wa jambo fulani au uvurugaji.
Dalili zinazoonyeshwa na mtoto mwenye uchangamfu wa uliopitiliza Mtoto anapokuwa amekaa katika mazingira yanayomlazimisha kutulia, yeye huonyesha tabia za
kuchezesha na kutingisha miguu au kurusha mikono na kubinua
kiti anapokuwa amekaa.
Pia, hushindwa kukaa mahala pamoja wakati unaotarajiwa awe na utulivu. Mfano; mkiwa kanisani au msikitini , hushindwa kutulia hadi ibada itakapoisha, au darasani anashindwa kukaa kwenye dawati lake muda wote wa kipindi.
Mtoto wa aina hii huwa pia na tabia za kurukaruka, kukimbia hovyo katika mazingira yanayohitaji utulivu, tabia ambayo hutafsiriwa na watu wazi kuwa si sahihi.
Pia hushindwa kucheza au kushiriki michezo au burudani kwa hali ya utulivu. Mfano mtoto anapokuwa anacheza lazima ahusishe kelele nyingi
zisizotarajiwa katika mchezo huo au kutarajiwa kwa umri wake.
Kuzungumza kuliko pitiliza bila kuwa na mtiririko wa sentensi zinazoeleweka. Ili kulibaini hili, utamuona mtoto akizungumza sana bila mpangilio katika mkusanyiko wa watu bila uwoga na bila kuzingatia sentensi ipi ianze na ipi imalizie.
Wataalamu wanasema mara nyingi watoto wa aina hii huamua kujibu jambo au swali kabla halijamaliza kuulizwa.
Na hupenda kumalizia sentensi ya mtu mwingine anapozungumza bila kusubiri zamu yake ya kuzungumza. Pia huwa hawana subira katika kutenda jambo. Kwa mfano wakati wa kula chakula, hawezi kusubiri zamu yake ifike aende akapakue chakula au kama kapanga mstari kwa ajili ya kuteka maji yeye atataka achote kabla ya wale aliowakuta.
Wengine katika michezo anaweza kuanza kung’ang’ania kutumia vitu vya mwenzanke bila ridhaa ya muhusika.
Kutokana na tabia nilizozitaja hapo juu, mara nyingi jamii hutafsiri tabia hizi kuwa ni utukutu, kufanya jambo kwa sifa au kusudi na matokeo yake huamua kuchukua hatua ya kumuadhibu mtoto huyo wakidhani anafanya kusudi.
Cha msingi
Mtoa tiba kwa vitendo atamsaidia mtoto mwenye hali kama hii, kujua jinsi ya kujitegemea, kujenga uhusiano na utulivu kwa kutumia mbinu mbalimbali hususani ya kumuhusisha moja kwa moja kwenye vitendo vyenye umaana wa kulenga kutatua changamoto zake.
DK Godfrey Kimathy ni mtaalamu wa Tiba kwa Vitendo (OT). Wasiliana naye kwa namba 0622 786 859.