Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Hakuna serikali dhaifu duniani ila vyama dhaifu

89605 Serikali+pic Hakuna serikali dhaifu duniani ila vyama dhaifu

Mon, 23 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Serikali nyingi duniani zinatokana na vyama vya siasa baada ya kushinda uchaguzi, kwa zile nchi ambazo zinafuata misingi ya demokrasia ya mfumo wa vyama vingi.

Vyama vya siasa hufanya kampeni kwa kushindanisha ilani zao ambazo zinaelezea kwa kina kuhusu mambo ambayo vitafanya baada ya kupata ridhaa ya kuongoza.

Katika mchakato huu, baada ya chama cha siasa kupata kura nyingi ikilinganishwa na vinginevyo hupata ridhaa ya kuunda serikali inayotokana na chama hicho.

Kwa hapa kwetu Tanzania, CCM ndiyo ilipata kura nyingi wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2015 na kuunda serikali. Ni serikali ya CCM kwa sababu ndio chama ambacho ilani yake ilichaguliwa baada ya kupigiwa kura.

Hivyo basi, mambo yote ambayo yatafanyika katika muhula huo wa uongozi yatatokana na ilani hiyo. Ilani ndiyo mwongozo wa wapi nchi inataka kuelekea na miradi ipi itafanyika na kwa muda upi.

Baada ya muhula kumalizika chama hutoa mrejesho wa utekelezaji wa ilani ili kutetea nafasi ya kuchaguliwa kuendelea kuongoza muhula unaofuata.

Lakini mara nyingi pia viongozi wa kisiasa hutoa mrejesho wa utekelezaji wa ilani katika kuleta maendeleo ya watu na vitu pamoja na kuboresha huduma za jamii.

Kwa kuwa serikali unaundwa kutokana na chama cha siasa, ni jukumu la chama husika kuizalishia mawazo ya mambo yote muhimu.

Katika nchi zinazofuata mfumo huu, ikitokea serikali imepwaya au kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ni kutokana na chama kilichoiunda kuwa dhaifu kuyasimamia yale ambayo yapo kwenye ilani yake.

Kwa mazingira hayo, hakuna serikali dhaifu kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo, bali vyama dhaifu ndivyo kushindwa kuisimamia serikali kutekeleza majukumu yake.

Katika kuboresha utendaji wa usimamizi wa vyama vya siasa, baadhi ya nchi zimeamua kuboresha muundo wa vyama vya siasa

ili kuongeza uwajibikaji kwa kutenganisha nafasi ya utendaji kazi kwa serikali na nafasi ya chama cha siasa.

Muundo huo ni rais wa nchi kutokuwa mwenyekiti wa chama ila kuwa kiongozi wa chama na kuwa msimamizi mkuu wa kutafsiri na kusimamia utekelezaji wa ilani kwa serikali anayoiongoza na kuwajibika kwa mwenyekiti wa chama kuhusu utendaji wa serikali.

Hii inasaidia kukuza uwajibikaji kwa chama cha siasa kuisimamia serikali na wakati wa vikao vya kamati kuu ni rahisi mwenyekiti wa chama cha siasa kumtaka rais ambaye si kiongozi wa chama kutoa ripoti ya uwajibikaji wa serikali.

Katika nchi ambazo rais wa nchi ni mwenyekiti wa chama ni vigumu kumpa majukumu au kuhoji kama kuna jambo analifanya ambalo haliendani na msimamo wa chama au halina manufaa kutokana na yeye kuwa mwenyekiti wa chama na anao uwezo wa kukataa hoja husika isijadiliwe ikiwa ataona si salama kwake.

Nchi kama Afrika Kusini, Kenya, Uingereza ni baadhi ya nchi zenye mifumo yenye wenyeviti wa chama kuwa tofauti na kiongozi wa chama.

Rais anakuwa kiongozi wa chama na mwenyekiti wa chama ni mtu mwingine ili kurahisisha uwajibikaji pale ambapo rais atatakiwa kutoa maelezo ya kina kuhusu utendaji kazi wa serikali.

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa si mwenyekiti wa ANC ila ni kiongozi wa ANC, Rais Uhuru Kenyata wa Kenya si mwenyekiti wa Jubilee ila ni kiongozi wa Jubilee na Boris Johnson ambaye ni waziri mkuu wa Uingereza si mwenyekiti wa chama cha Conservative ila ni kiongozi wa chama hicho.

Mara nyingi vyama vya siasa ambavyo vinaongoza nchi changa ama zinazoamini katika sera za ujamaa ndio zimefungamanisha nafasi ya mwenyekiti wa chama na rais hasa kwa lengo la kujenga utaifa katika nchi husika kati ya chama, serikali na wananchi. Nchi hizo hukijenga chama cha siasa katika mikono ya wananchi.

Kwa nchi kama Tanzania ilikuwa haikwepeki kwa Tanu kufuata mfumo huu kutokana na sera ya ujamaa na kujitegemea ambayo ilikuwa inapatikana katika Azimo la Arusha la mwaka 1967 lililosaidia kujenga misingi ya utaifa na kubomoa ukabila, udini na aina yoyote ya ubaguzi ambayo ingehatarisha umoja na amani ya nchi.

Hata hivyo ni miaka 58 sasa tangu tupate Uhuru, na ni miaka 42 ya CCM madarakani kuiongoza Tanzania lakini bado tunafuata mfumo huu fungamanishi? Ni nini faida zake? hasara zake je? na nini kifanyike? Maswali hayo nakuachia ndugu msomaji na unaweza kutoa mrejesho kupitia:

Columnist: mwananchi.co.tz