Katika hali ya kawaida, uchaguzi wa kupata viongozi wa umoja ambao unajumuisha mahakimu na majaji, mtu mwenye wadhifa wa jaji angekubalika kirahisi na kushinda, lakini haikuwa hivyo kwa Chama cha Majaji na Mahakimu (JMAT).
Hakimu ndiye aliyeshinda na kuwa kiongozi wa umoja huo na timu yake inayomjumuisha makamu wake, katibu, katibu msaidizi, mhazini na katibu mwenezi, ambao wataongoza kwa miaka mitatu ijayo.
Hiyo ni historia iliyowekwa kwa mara ya kwanza katika chama hicho tangu kilipoanzishwa mwaka 1984.
Msimamizi wa uchaguzi huo ambaye ni mkuu wa Taasisi ya Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Jaji Dk Paul Kihwelo alimtangaza Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kishapu, Wilberforce Luhwago kuwa mshindi baada ya kuwabwaga wagombea wenzake wengine watatu, wakiwamo majaji wawili.
Hakimu Luhwago aliibuka na ushindi wa kishindo baada ya kupata kura 85 kati ya kura 147, akifuatiwa na Jaji Ilvin Mugeta aliyepata kura 41, wakati Jaji Sophia Wambura alipata kura 16 na Hakimu Mkazi Pascal Rwagesa akapata kura tano.
Jinsi Hakimu Luhwago alivyopata uongozi huo ni kama mtu aliyeokota embe chini ya mwarobaini, hakutumia nguvu wala kutokwa jasho jingi, kwani hakuwa amejiandaa wala kupanga kugombea nafasi hiyo. Mkutano huo wa uchaguzi ulifanyika Dodoma, ambako Hakimu Luhwago aliamua kusimama kwa muda kuhudhuria ndipo aendelee na safari ya kuelekea katika kituo chake cha kazi.
“Kwa kuwa kulikuwa na mkutano wa Chama cha Majaji na Mahakimu jijini Dodoma, uliokuwa unaambatana na uchaguzi wa viongozi wakuu wa chama hicho, nikiwa mwanachama, niliamua kusimama hapo kushiriki kwanza mkutano huo ndipo niendelee na safari yangu,” alisema Hakimu Luhwago.
Anasema alipofika maeneo ya Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma, alipata ajali baada ya gurudumu la gari lake kuchomoka. Licha ya gari kuharibika sana, alitoka salama na akafanya utaratibu kulivuta gari hilo hadi eneo la Mahakama Kuu.
Alisema baadaye alienda kulala na kupumzika siku iliyofuata kusubiri mkutano ambao ulikuwa Ijumaa.
“Nikiwa nimepumzika hotelini siku ya Alhamisi, nilifuatwa na watu wapatao 30 kunishauri nigombee,” anasema Hakimu Luhwago.
“Niliwauliza sababu za kufanya hivyo, wakanijibu kuwa chama kinaonekana kama kipo kwa jina tu, lakini hakionekani katika utekelezaji wa majukumu yake. Walisema wameona mimi ndio naweza kukifufua, kukipeleka na kurejeshea sifa yake kama chama cha kitaaluma.
“Hata hivyo, nikawaambia kuwa watangaza nia wameshatangaza karibu wiki mbili zilizopita. Mimi kuchukua fomu zikiwa zimebaki saa chache inanipa tabu kidogo.
Wakasema kwa kuwa katiba haijakataa tunachukua,” alisema.
Anasema alipotafakari maneno yao pamoja na malalamiko ya mahakimu, kama changamoto wanazokumbana nazo kwa mwajiri wao Tume ya Utumishi wa Mahakama, huku kukiwa hakuna wa kuwasemea, alikubali nao wakaenda kumchukulia fomu.
Luhwago anasema ili kuepuka fitina na mizengwe ya kiuchaguzi kama ambavyo huwa inatokea kwenye siasa, walikubaliana jina lake lisijulikane mapema bali iwe ni kushtukiza tu ili washindani wake wasipate muda wa kujiandaa.
Anasema wapigakura wengine walibaini katika hatua za mwisho kuwa anagombea baada ya msimamizi wa uchaguzi kutangaza majina ya wagombea.
Anasema baada ya taratibu zote za uchaguzi kukamilika, alitangazwa kuwa mshindi, akiwa amepata kura 85 na kuwazidi wagombea wote kwa pamoja kwa kura 23 na hivyo kuwa rais mpya wa chama hicho.
Pamoja na kutofanya kampeni, Hakimu Luhwago anasema anadhani kilichompa ushindi ni ajenda yake kuweka mbele utawala wa sheria.
“Ajenda yangu ilikuwa moja tu, utawala wa sheria. Utawala wa sheria ndani na nje ya mahakama. Ndani ya mahakama ni kwamba mwajiri anapowashughulikia watumishi wake anatakiwa awashughulikie kwa mujibu wa utawala wa sharia,” anasema.
“Sio kuna watu wa Escrow, anawafunika lakini wanaotumia mihuri vibaya anawashughulikia. Hilo likitokea ni lazima mahakama i-expect serious counter statement (itarajie tamko kali la kupinga) kutoka kwa rais wa JMAT.”
Katika kashfa ya akaunti ya escrow, iliyohusisha uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka akaunti ya pamoja ya kampuni binafsi ya IPTL na Tanesco, majaji walituhumiwa kuhusika na baadhi kutajwa kuwa walipata mgawo wa fedha, lakini muhimili huo haukutoa tamko la kulaani kitendo hicho.
Kwa mujibu wa mmoja wa wapigakura ambaye ni hakimu kutoka Mwanza, siri ya kumtaka Luhwago kuwania nafasi hiyo na kisha kumchagua ni misimamo yake katika kusimamia haki, sheria na taratibu.
“Kabla ya kumjua kwa sura Mheshimiwa Luhwago, nilikuwa namsikiasikia tu wakati akiwa hapo Mahakama ya Wilaya ya Ilala Dar es Salaam. Hivyo kitu kilichofanya watu wengi wamkubali ni kuwa huyu jamaa anafuata zaidi utaratibu na sio siasa,” anasema hakimu huyo bila kutaka jina lake litajwe. Hakimu huyo anasema kuwa yeye alifika Dodoma akiwa amepanga kumchagua mgombea mwingine ambaye ni jaji.
“Lakini tulivyokuwa tukitembea watu wakawa wanasema Jaji (anamtaja jina) kweli ni mzuri, lakini wale wameshakuwa watu wakubwa (hivyo) hawezi tena kuwakumbuka watu wa chini,” anasema hakimu huyo.
“Halafu wakasema hata huku chini pia tuchague mtu ambaye ana misimamo ambaye anaweza kutetea haki za wengine bila woga na ambaye anafuata utawala wa sheria. Mtu aliyetajwa wa kwanza ni Hakimu Luhwago.”
Anasema katika kumjadili Hakimu Luhwago ilielezwa kuwa kutokana na msimamo wake aliwahi kumwandikia Jaji Kiongozi wito wa kufika mahakamani aliyetaka kumpa maelekezo katika kesi moja, ili akaeleze mahakamani kama alikuwa analijua jambo hilo.
“Sasa hicho kitu kikawa-impress (wavutia) watu wengi kwamba huyu mtu inawezekana akatuvusha kwa sababu ana msimamo na ujasiri, mkweli na si mwoga, maana kuna changamoto ambazo zinataka mtu asiye mwoga, mkweli, anayeweza kusimamia jambo kwa haki na kwa data bila kutetereka.”
Kwa upande wake Hakimu Honorina Kambadu wa Kibaha anasema Hakimu Luhwago ni mkweli na muwazi, aliye tayari kutetea haki sawa kwa wote.
“Ni mtu anayeweza kupigania haki hata kwa mambo ambayo anaona ni changamoto katika kazi na maslahi kwa wote. “Hata katika uchaguzi huu alifanikiwa kupata kura nyingi kutokana na weledi wake, heshima na maadili aliyo nayo hasa katika kufanya kazi kwa kufuata utawala wa sheria. Hakika anastahili nafasi hiyo na ninaamini anaweza kuongoza vizuri.”