Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HOJA ZA MALOTO: Kuzidisha siasa bungeni kunatishia hadhi yake

Mon, 24 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbunge wa Kasulu Vijijini (CCM), Augustine Vuma, kwa utashi wake, aliamua kuchana kitabu cha hotuba ya “Bajeti mbadala” kama ilivyowasilishwa bungeni na Kambi ya Upinzani.

Baada ya wabunge wa upinzani kulalamikia kitendo hicho, aliyekuwa anaongoza kiti cha Spika, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alimtaka aombe radhi na kufuta maneno yake.

Wabunge wa upinzani wakaona kufuta maneno na kuomba radhi haitoshi, walitaka apelekwe Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili ikibidi achukuliwe hatua zaidi.

Tulia alipokataa hilo, ilibidi awatoe nje ya Bunge, wabunge wa Chadema, John Heche (Tarime Vijijini), Esther Matiko (Tarime Mjini) na Immaculate Saware (Viti Maalum) ambao aliona wanakaidi uamuzi wake.

Hayo tayari yametokea, hapa tujadili hadhi ya Bunge. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kusema kuwa mtu akipewa nafasi ya kuongoza watu lazima ajiheshimu. Mbunge ni kiongozi, anaonyesha mfano gani kwa kuchana hotuba badala ya kuijadili?

Mbunge lazima aoneshe umahiri wa kujenga hoja. Kutetea ya kwake au kuiongezea uzani ile anayoiunga mkono, vilevile kuibomoa ambayo hakubaliani nayo kwa njia ya hoja. Siyo kuchana hotuba yenye maneno ambayo unakuwa hukubaliani nayo.

Pia Soma

Wabunge walioomba mwongozo wa kiti cha Spika walitumia Kanuni ya 64 ya Bunge. Kanuni hiyo vipengele f na g, vinasomeka hivi: “Mbunge hatamsema vibaya au kutoa lugha ya matusi kwa mbunge au mtu mwingine yeyote. Mbunge hatatumia lugha ya kuudhi au inayodhalilisha watu wengine.”

Dk Tulia alitoa ufafanuzi kuwa kanuni ya 64 inazungumzia maneno na mwongozo wa kikanuni ni kumtaka mbunge kuomba radhi na kufuta maneno yake.

Tulia akasema, kitendo cha Vuma kinafanana na cha mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Ester Bulaya, kwamba naye kuna siku aliondolewa bungeni, wakati anatoka alirusha vitabu lakini hakuadhibiwa.

Ukweli; makosa ya Bulaya na Vuma yapo tofauti. Huyu kachana hotuba, yule alirusha vitabu. Zaidi ni kwamba kutokuadhibiwa kwa Bulaya hakuhalalishi mtenda kosa mwingine asiadhibiwe.

Kama Bulaya aliachwa ili kosa lake lilipizwe kwa aina ya kitendo cha Vuma, hilo litakuwa ni Bunge la namna gani? Kwamba wamerusha, sisi tunachana.

Tuutafakari ukweli; hotuba iliyochanwa imeandaliwa na wapinzani (Chadema). Aliyechana ni wa CCM. Tulia ni wa CCM. Je, kwa sababu za kisiasa ndiyo kosa halisi la Vuma limeshindwa kuonekana.

Kanuni ya 74 ya Bunge, fasili ya 1, inazungumza mamlaka ya Spika kupeleka jina la mbunge kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ikiwa; (a) kwa maneno au vitendo, mbunge huyo anaonyesha dharau kwa mamlaka ya Spika; au

(b) Mbunge huyo atafanya kitendo chochote cha makusudi cha kudharau shughuli ya Bunge au mbunge yeyote anayeongoza shughuli hiyo.

Kanuni hii inasema kuwa mbunge anayedharau shughuli za Bunge anatakiwa kuagizwa na Spika kwenda Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge. Na hili ndilo ambalo Heche, Matiko na Saware walilipigania.

Tuulizane; shughuli za Bunge ni nini? Bunge lipo kwenye mjadala wa Bajeti ya Serikali. Utaratibu wa Bunge ni kuwa Bajeti inaposomwa na Waziri wa Fedha, Waziri Kivuli naye huwasilisha bajeti mbadala.

Hivyo, hotuba ya Bajeti ni shughuli ya Bunge, kadhalika maoni ya Kambi ya Upinzani. Ndiyo maana Bunge linagharamia maandalizi ya hotuba hadi kuwasilishwa kwake.

Katikati ya mjadala wa Bajeti, mbunge anachana hotuba, je, huko siyo kudharau shughuli ya Bunge? Kama kanuni ya 74 ingetafsiriwa vizuri, wala kusingekuwa na mabishano yoyote. Ni dhahiri Vuma anapaswa kupelekwa Kamati ya Maadili ili ahojiwe kwa kudharau shughuli ya Bunge.

Tatizo linaloonekana bungeni ni tofauti za kisiasa. Kitendo cha Vuma kuchana hotuba ya Bajeti mbadala, bila shaka kiliwafurahisha wengi. Na ingetokea kiti cha Spika kuuliza wabunge kama aadhibiwe au asamehewe, wabunge wa CCM kwa wingi wao wangemtetea asiadhibiwe.

Ni kama ingetokea mbunge wa upinzani angechana hotuba ya Bajeti Kuu, wabunge wa CCM wangepiga kura kwa nguvu aadhibiwe, wakati wapinzani wangemtetea. Siasa zinafanya Bunge likose misingi. Watu wanachagua ukweli wa kuuona kwa sababu za kisiasa. Kosa la mwana CCM wabunge wa CCM wanaona si kosa. Akikosea wa upinzani, ni kosa baya lisilofaa kusamehewa; vivyo hivyo kinyume chake.

Bunge la Tanzania limekuwa likituma ujumbe mbaya kwa jamii, kwamba makundi ya vyama ni muhimu kuliko misingi ya kibunge. Naiota siku ambayo mbunge atafanya kosa, kisha wabunge wote wakiwamo wa chama chake, wasimame pamoja kusisitiza aadhibiwe.

Kitendo cha Vuma kilifaa kuunganisha wabunge wote, maana hotuba ya Bajeti mbadala ni mali ya Bunge na haipaswi kuvunjiwa heshima. Mbunge mstaarabu atachambua yaliyoandikwa na kuyakosoa kwa hoja. Kuchana hotuba ni jambo la ajabu na kulidhalilisha Bunge. Na kumtetea mbunge huyo na kitendo chake ni kutetea hali hiyo.

Wakati wa Bunge la Tisa, mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba pia aliwahi kuchana hotuba ya Bajeti mbadala na hakuchukuliwa hatua yoyote, pengine ndiyo maana hayo yanajirudia. Vitendo hivyo vinapaswa kukomeshwa, maana vinadhalilisha Bunge. Ieleweke kuwa Bunge ni chombo cha kuiweka nchi kwenye mizania, si kijiwe cha kutambiana kisiasa na kuvunjiana heshima.

Kiongozi wa chama cha Labour, Uingereza Jeremy Corbyn aliwahi kusema: “Bunge ni sehemu ‘sirias’, siyo sehemu ubabaishaji na kushangilia bila mpangilio.”

Columnist: mwananchi.co.tz