Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HOJA ZA MALOTO: Adui wa umma ni watekaji au wanaotangazwa kutekwa?

66616 PIC+UMMA

Sat, 13 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Vitendo vya utekaji vinashamiri. Hapohapo yanaibuka malumbano kati ya dola na wenye kutangaza kutekwa au wale wanaotoa taarifa kuhusu wapendwa wao kuchukuliwa. Ikiwa hali inayoibuka ni hiyo, je, adui wa umma ni nani? Watekaji au wanaotangazwa kutekwa?

Kuna msemo wa Kilatini “Hostis Publicus”, ukiwa na maana ya adui wa watu. Aprili 1930, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uhalifu ya Chicago, Marekani, Frank Loesch, aliutumia msemo huo wa Kilatini, kumtangaza haramia Alphonse Capone ‘Al Capone’ kuwa adui wa watu wa Chicago.

Al Capone au Scarface kwa jina lingine, alikuwa mtu hatari kwa wakati wake, alimiliki mtandao mkubwa wa uhalifu wa kupangwa, ulioitwa Chicago Outfit. Aliihenyesha dola, mpaka Loesch akaamua kumtangaza kuwa adui wa watu.

Baada ya tangazo la Loesch kuhusu Al Capone, maeneo mbalimbali ya Marekani yaliitika, majina ya wahalifu yalitajwa kwenye mamlaka za majimbo na majiji. Umma wa Wamarekani walijulishwa kuhusu maharamia mbalimbali.

Matamko hayo kwa wingi wao kuwalenga maharamia mbalimbali waliokuwa wakiitikisa Marekani kwa wakati huo, yalisababisha kipindi hicho kiitwe zama za Adui wa Umma, yaani “Public Enemy Era” kwa lugha ya Kiingereza.

Public Enemy Era ni kipindi cha kati ya mwaka 1930 mpaka 1935. Wahalifu wakubwa zaidi waliosababisha miaka hiyo iitwe zama za adui wa umma Marekani ni Al Capone, John Dillinger, Baby Face Nelson, Bonnie na Clyde.

Pia Soma

Maharamia wengeni ni Pretty Boy Floyd, Machine Gun Kelly, Ma Barker na Alvin Karpis. Public Enemy ni nyakati zilizoibuka kipindi cha mdororo mkubwa wa kiuchumi kati ya mwaka 1929 mpaka 1939. Mdororo huo ulisababishwa na anguko la uchumi wa viwanda na kuporomoka kwa soko la hisa kwenye nchi za Magharibi.

Marekani ikiwa inateswa na hali mbaya ya kiuchumi, vilevile ilikuwa ikisumbuliwa na uhalifu wa mipango uliokuwa ukitekelezwa na makundi hayo hatari. Mashushushu wa FBI walipelekwa puta na maharamia hao ambao walijijengea umaarufu wa kuogopwa.

Maneno Public Enemy yamekuwa yakirudiwa mara kwa mara na kutamkwa kwenye vipindi tofauti. Rais wa 37 wa Marekani, Richard Nixon, mwaka 1969 alitangaza biashara ya dawa za kulevya kuwa ni adui wa umma.

Tanzania inasimamia wapi?

Umma lazima uambiwe adui yao ni nani. Mamlaka za nchi zina wajibu wa kuwahamasisha wananchi kumtambua adui yao. Katika mkasa wa utekaji, adui ni nani? Wanaosemwa kutekwa? Kwa nini mamlaka zinasuguana na watoa taarifa za utekaji?

Hivi karibuni kulitokea kizaazaa cha kutekwa mfanyabiashara raia wa Kenya, Raphael Ongagi ambaye ni rafiki wa Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe. Vilevile Ongangi alipata kuwa msaidizi wa Zitto kwa miaka saba.

Ilielezwa kuwa Raphael akiwa kwenye gari na familia yake Oysterbay, Dar es Salaam, gari lake lilizuiwa na watekaji wenye bunduki, wakamchukua na kuondoka naye. Siku nane baadaye Raphael alipatikana Mombasa, Kenya.

Taarifa ya Kamishna wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa ametilia shaka utekwaji wa Raphael. Anahoji iweje atekwe Dar akaachiwe Mombasa jirani na kwa shangazi yake?

Mwandishi Azory Gwanda anaelekea kutimiza miaka miwili tangu alipotekwa na watu wasiojulikana. Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, alisema Azory alitoweka kwa sababu zake za kimaisha.

Kada wa Chadema, Ben Saanane ambaye alikuwa msaidizi binafsi wa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, anaelekea kutimiza miaka mitatu tangu atoweke. Taarifa za kupotea kwake zikawa mvutano wa dola na watoa taarifa. Mpaka leo imekuwa kimya, watu wameelekea kukata tamaa.

Hata juzi waziri wa mambo ya nje akiwa Uingereza alipotoa kauli iliyoonekana kutoa mwanga, bado baadaye aliikana kuwa alinukuliwa vibaya.

Kijana mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Abdul Nondo, aliingia kwenye matatizo na polisi alipopatikana Iringa, baada ya kupita siku mbili ikielezwa alitekwa. Polisi walisema alijiteka.

Swali ni hili; kwa nini polisi hawashirikiani na watoa taarifa za kutekwa au watekwaji wanaopatikana ili kuwapata watekaji, badala yake unaibuka mvutano kati ya watekwaji na dola? Nani adui wa umma, watekaji au watekwaji?

Mwandishi wa Marekani mwenye asili ya Ukraine, Chuck Palahniuk, alipata kusema: “Tunapokuwa hatujui mtu wa kumchukia, huchukiana sisi wenyewe.” Inaonekana adui wa umma hajulikani, hivyo waathirika wa vitendo vya utekaji na jeshi la polisi, wanachukiana badala ya kushirikiana.

Vitendo vya utekaji vinashamiri. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibondo, Simon Kanguye ana miaka miwili hajulikani alipo. Pia, hivi karibuni Allan Kiluvya ambaye ni msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani, Bernard Membe alitekwa lakini baada ya siku chache alipatikana.

Majibu yenye kunyooka hayapatikani hata kwa walioripotiwa kutekwa na kupatikana. Mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘MO’ alitekwa kwa siku nane mwishoni mwa mwaka jana na taarifa za kupatikana kwake zilitengeneza alama nyingi za mshangao.

Ajabu polisi hawakutoa taarifa iliyonyooka kuhusu kutekwa na kupatikana kwa MO. Ni kwa sababu hiyo, Rais John Magufuli, aliliambia Jeshi la Polisi Tanzania kuwa Watanzania sio wajinga.

Alitekwa kijana kada wa Chadema, Mdude Nyagali, mbunge wa Mbozi (Chadema), Paschal Haonga, alikamatwa na polisi kwa sababu ya kutamka kuwa kijana huyo alitekwa. Mdude alipatikana akiwa ameumizwa vibaya.

Shida ni nini? Polisi hawawaamini wanaotoa taarifa za kutekwa au watekwaji? Kwani adui wa umma wa Watanzania ni nani hasa? Tukimjua adui, misuguano ya dola na watekwaji itakwisha.

Columnist: mwananchi.co.tz