Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HOJA ZA KARUGENDO: Vijana wa Afrika wana jukumu zito leo na kesho kuliko jana

60297 Pic+africa

Thu, 30 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Vijana wa jana wa Afrika, akina Mwalimu Julius Nyerere, Nelson Mandela, Patrice Lumumba na wengine ambao bado wako hai kama Kenneth Kaunda, walipambana kufa na kupona ili kuleta ukombozi wa Afrika.

Walipambana na ubeberu na ukoloni mambo leo. Walitaka kuleta na kujenga uhuru wa Afrika na kumkomboa Mwafrika kifikra. Chuo kikuu cha Dar es Salaam, kilianzishwa wakati wa vuguvugu la ukombozi wa Afrika. Na kufuatana na sera za Mwalimu za ukombozi wa Afrika, chuo hiki kiliwapika na kuwaivisha wapambanaji na wanazuoni wengi wa Afrika.

Vijana wa leo na kesho wa Afrika ni muhimu kuwa makini na changamoto iliyo mbele yao; Uhai wa Afrika uko mikononi mwa vijana wa leo na kesho.

Vijana wa jana wa Afrika walikuwa na changamoto nyingi; walipambana na ukoloni na kuhakikisha kwamba nchi zote za Afrika zinakuwa huru. Wengine waliuawa kama Lumumba, wengine walifungwa kwa muda mrefu kama Mandela na wengine walipambana hadi mwisho wa uhai wao kama vile Nyerere. Tunaweza kusema kwa kiasi fulani walifanikisha mapambano yao. Umoja wa Afrika hata kama bado unachechemea, lakini hatua waliyoifikia ni ya kupongezwa. Jukumu la Umajumui wa Afrika liko mikononi mwa vijana wa leo na kesho.

Hoja yangu ni kwamba vijana wa leo pia wana changamoto nyingi mbele yao. Kuna tishio la ubeberu na ukoloni mambo leo, utandawazi na soko huria, ukosefu wa ajira na tatizo la uongozi katika nchi za Afrika.

Kuna tatizo la umilikaji wa ardhi, mfano Zimbabwe, kule Loliondo na sehemu nyingine nyingi. Pamoja na jitihada za serikali kushughulikia suala la ardhi, bado ni tatizo kubwa na lenye utata.

Pia Soma

Mapambano tunayoyasikia Misri, Tunisia na Libya, kwa kiasi kikubwa yameongozwa na vijana. Kule DRC, wanaopigana ni vijana na wakati mwingine tunasikia hata na watoto wanalazimishwa kushika bunduki.

Hata hapa Tanzania, vyama vya upinzani vimejaa vijana; lakini hata CCM, tumeshuhudia jinsi vijana wanavyojitahidi kujitokeza kupinga yale wanayofikiri hayana lengo la kuiandaa Tanzania ya miaka 50 ijayo.

Wakati vijana wa jana, wanamalizia kazi yao ya miaka 50 ya kuijenga Afrika, ni lazima vijana wa leo kutafakari kwa makini kazi iliyo mbele yao ya kuijenga Afrika ya miaka 50 ijayo. Tena ni bora vijana wakakumbuka kwamba mapambano ya silaha za moto yanaanza kupungua umaarufu wake. Enzi hizi za utandawazi zinatulazimisha kutumia fikira zaidi ya silaha za moto.

Tumeona kilichotokea kule Sudan. Rais, ameondolewa bila kutumia silaha za moto. Vijana wameshikamana, kwa kutumia fira pevu na teknolojia ya kisasa, wamefanikisha malengo yao.

Na wala tatizo si umasikini tena; Libya ilikuwa imepiga hatua kimaendeleo; huduma za jamii kama barabara, maji, umeme na hospitali ziliwafikia watu wengi, hata wale wasiokuwa na ajira walipata mshahara. Watu wanataka uhuru wa mawazo, uhuru wa kuamua maisha yao wenyewe, uhuru wa kumchagua kiongozi wanayemtaka.

Kuna haja kubwa ya ukombozi wa kifikira; kuna haja kubwa ya kujadiliana na kubadilishana mawazo. Kama majukwaa ya fikra yaliyoanzishwa na Mwananchi. Tunahitaji mijadala mingi ya ukombozi wa kifikra. Bila kujikomboa kifikira na vijana kupambana kwa pamoja kwa lengo la kuijenga Afrika; kuna hatari Afrika kutawaliwa tena au kumezwa ndani ya utandawazi.

Vijana wasisukumwe na ushabiki au kutumiwa na walafi kama tunavyoona kwenye uchaguzi wa wanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kwenye vyama vingine vya siasa.

Vijana watambue jukumu zito lililo mbele yao linahitaji maandalizi, elimu iliyo bora, maadili mema, kumcha Mungu, uzalendo, hekima na busara.

Watu wamekufa Darfur, Somalia, Rwanda, hatukusikia msamiati huu wa “kulinda maisha ya raia” kama tunavyosikia kule Libya.

Ni kulinda raia au ni kulinda uwekezaji na wawekezaji katika nchi husika? Kama nchi haina wawekezaji wa nchi za kigeni; Jumuiya ya Kimataifa inakaa kimya. Hivyo kuna haja vijana wa Afrika, wakafumbua macho na kuona ukweli wa ubeberu ndani ya Afrika na kujiandaa kupambana kufa na kupona.

Tunaweza kutofautiana kimawazo, na si lazima tuwe na mawazo na maoni yanayofanana; lakini tukigusa umoja wetu ni lazima kushikamana. Umoja ndani ya nchi za Afrika, ndio utajenga umoja wa Afrika nzima. Nchi za Afrika zikisambaratika (ubeberu ukiwa na nguvu), na Afrika nzima itasambaratika.

Columnist: mwananchi.co.tz