Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HOJA ZA KARUGENDO: Tutumie Bongo Flava kupata amani, uzalendo

Thu, 4 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wiki iliyopita Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF) na washirika wengine waliandaa kongamano la amani. Nililetewa mwaliko, lakini sababu zilizo juu ya uwezo wangu zikanizuia kushiriki lakini niliweza kufuatilia kila kitu baadaye kwenye mitandao.

Kila mtu ni bingwa wa kuongea juu ya amani hata na wale ambao mioyo yao imejaa chuki, fitina, ubaguzi na upendeleo wa waziwazi wanaongea juu ya amani.

Niwapongeze walioandaa mdahalo huo na walioshiriki na wanaotamani tuwe na amani nchini. Kwa maneno ya Joseph Butiku, mkurugenzi wa MNF, watu wanazungumza kwa kumung’unya maneno na kwa kigugumizi… hata yeye (Butiku) hivyohivyo.

Ningeshiriki, ningesema hivi: Tuache kumung’unya maneno na tuachane na kigugumizi, amani inajengwa, inafanyiwa kazi, inatunzwa na kulindwa kwa gharama kubwa. Hivyo, tunahitaji mifumo na mbinu za kujenga amani kwa amani, mifumo ya kujenga uzalendo wetu kwa amani. Njia mojawapo ya kujenga amani kwa amani, ni kutumia Bongo Flava. Sote tunajua kwamba Bongo Flava inafurahisha na kuhamasisha vijana lakini wakati mwingine ujumbe wake ni mchungu na unapenya ndani ya jamii.

“Afrika nakutamani, nikikumbuka sifa zako, ingawa niko nchi mbali furaha haishi moyoni. Sina budi kukumbuka, Afrika nakutamani… Utumwa ni kitu kibaya, tuliuzwa kama samaki, samaki wa kwetu wanono, si kama hawa wa Amerika.”

Hizi ni baadhi ya beti za wimbo ulioimbwa na watumwa enzi zile. Kama tujuavyo utumwa ni unyama wa hali ya juu, ni unyanyasaji uliopindukia. Wakati ule wanyonge walionewa na haki zao kama binadamu zilipotea. Kwa kujituliza waliimba na wakati mwingine kucheza muziki.

Kuna mifano mingi inayoonyesha jinsi nyimbo, ngoma na muziki zilivyo kitulizo cha watu wanaoonewa au wale wanaotaka kujenga uzalendo na utambulisho wao. Daima inakuwa njia yao ya kujituliza, kutoa ujumbe katika jamii lakini pia kama njia ya kuhamasisha wanaoonewa kushikamana na kupigania haki zao.

Hoja ninayotaka kuijenga hapa ni kwamba nyimbo, muziki na ngoma vimekuwa kichocheo cha mapambano na harakati kwa watu wanaoonewa, wanaotawaliwa au wale wanaotaka kuwa na uzalendo wao na kujitambua kama kitu kimoja.

Afrika Kusini ni mfano mwingine. Waimbaji mashuhuri kama Miriam Makeba na wengine wengi walitumia nyimbo na muziki kuhamasisha mapambano ya ubaguzi wa rangi. Inaelekea mwanadamu ana tabia ya kutumia nyimbo kuelezea machungu aliyonayo moyoni, ya jamii na wakati mwingine ya taifa. Hata enzi za Waisraeli, tunawasikia wakiimba: kitabu chote cha Zaburi ni nyimbo walizoziimba wakimlilia Mungu, kuwaletea ukombozi.

Mimi ninaamini kwamba ujumbe wa Bongo Flava ni mchungu. Kwa mtu anayejali maisha ya leo na kesho kwa taifa letu, ujumbe wa Bongo Flava, ni lazima utauona ni mchungu. Muziki unapendeza, wanacheza vizuri na kuonyesha ubunifu wa hali ya juu, lakini maneno yao yanachoma kwa ncha kali. Ujumbe wao hauna tofauti na ujumbe ulio kwenye nyimbo za watumwa, Waamerika weusi wala Afrika ya Kusini wakati wa ubaguzi.

Bongo Flava ina ujumbe wa wanyonge, wanaonyanyaswa na wasiosikilizwa. Inabeba sauti za watoto yatima, watoto wa mitaani, machinga, vijana wa vijiweni wasiokuwa na ajira na walalahoi.

Bongo Falava inabeba ujumbe wa ufa mkubwa unaoendelea kupanuka kila siku kati ya walionacho na wasiokuwa nacho, matajiri masikini. Hii ni changamoto kubwa inayolisakama Taifa letu. Serikali ina mipango gani kupunguza ufa huu, maana kadiri ufa unavyoendelea kuongezeka ndivyo na mashaka ya kizazi kijacho kuishi kwa amani yanaongezeka.

Bongo Flava, ni kioo cha jamii, ni sauti ya wanyonge na Watanzania. Watu wengi wanaanza kuipenda, si kwa kusikia na kufurahi tu, bali na kutafakari pia. Imani yangu ni kwamba tukiitumia kimkakati inaweza kutusaidia kujenga amani na uzalendo katika taifa letu.



Columnist: mwananchi.co.tz