Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HOJA ZA KARUGENDO : Tujadili mambo muhimu yanayoligusa Taifa letu

38013 Pic+taifa HOJA ZA KARUGENDO : Tujadili mambo muhimu yanayoligusa Taifa letu

Wed, 23 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kwa maoni yangu kabla ya kuwajadili watu na vyeo vyao kama tunavyoshuhudia ya CAG, Bunge, Spika, wanasheria na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa, tujadili mambo yanayoligusa Taifa.

Haina maana ya kuwa na mjadala mkubwa juu ya watu na vyeo kabla ya kuongelea maadili ya Taifa. Kwa nini tukimbilie kwingine kabla ya kujadili demokrasia, vyama vingi na dhana nzima ya uchaguzi mkuu na hasa juu ya Tume huru ya uchaguzi?

Bila Tume huru ya uchaguzi, sioni matumaini ya Taifa. Kwa nini tusijadili umaskini wetu kabla ya kitu kingine? Kuna haja ya kujadili namna ya kulijenga Taifa.

Bado kuna kazi kubwa ya kuwaelewesha Watanzania kwamba nchi ni yetu sote. Tunaona kiburi cha baadhi ya Watanzania wanaofikiri nchi hii ni yao peke yao.

Hili ni lazima lifahamike na ni jambo la haraka kuliko kumjadili CAG na Spika.

Kama kweli CAG si bosi wa wabunge lakini je, wanatambua wao bosi wao ni nani? Wamewekwa? Je, ni Serikali au Rais? Spika anamtambua bosi wake? Anamsikiliza?

Jambo la haraka kujadiliwa ni maadili, mfumo wa kutumia kufundisha kitaifa kwa vijana wetu na kwa Taifa zima. Sasa maadili yameegemea dini za kigeni. Ukristo na uislamu. Pamoja na heshima zangu kwa dini hizi za kigeni, bado tunahitaji kuwa na maadili ya kitaifa kama Watanzania.

Pia, suala la demokrasia na vyama vingi. Mwaka 2005, nilipata bahati ya kuwa mwangalizi wa uchaguzi katika Mkoa wa Mtwara. Na mwaka wa 2010 nilikuwa Zanzibar. Ukiwa mwangalizi wa ndani wa uchaguzi unagundua mengi juu ya demokrasia yetu changa. Jambo nililojifunza ni kwamba demokrasia na vyama vingi bado ni wimbo usiyojulikana na wengi.

Mwenye uwezo wa kupika pilau, kununua mipira, na pombe anachaguliwa.

Laini kuwa mwana CCM, hata kama huna uwezo unachaguliwa maana elimu ya uraia hakuna na bado kuna wanafikiri kuwa mwanaCCM ndio Utanzania.

Wapo wanaviona vyama vya upinzani kama usaliti. Uchaguzi wa 2005 Mtwara, walikuwa bado wanataka kumchagua Mkapa au mtu wa Mwalimu. Kwamba mtu anachaguliwa kufanya nini, bado ni somo gumu. Mawazo, ya kitemi na ubwana, ndio yanatawala, ukizingatia kwamba Mtwara, kuna historia ya utumwa na kutawaliwa na Mamwinyi.

Wakati wa somo hili ndipo mijadala kama demokrasia, siasa za vyama vingi, na shirikisho la Afrika ya Mashariki au muungano wa Afrika nzima, vinaweza kujadiliwa.

Tufundishe maadili, demokrasia na kuhimiza uzalendo wa Taifa. Cha msingi ni kuwaelewesha watu ili watambue kwamba Tanzania ni yetu sote.

Hakuna mwenye haki zaidi ya mwingine. Tunaweza kutofautiana kama kabila zetu, dini na itikadi lakini utaifa na uzalendo ni kitu cha lazima kwa kila Mtanzania. Tofauti zetu zisitutenganishe, bali zituunganishe! Daima chanya na hasi, zinazaa chanya! Hiyo ni sayansi ya maumbile na sisi hatuko nje ya maumbile hayo. Mawasiliano; 0754-633122 au [email protected]



Columnist: mwananchi.co.tz