Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HOJA ZA KARUGENDO: Siasa mbaya ni mauti, nzuri ni maendeleo

51531 Pic+siasa

Wed, 10 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Jumapili Aprili 7 Rwanda ilifungua siku 100 za maombolezo ya kumbukumbu ya miaka 25 ya mauaji ya kimbari. Kwa Kinyarwanda inaitwa “Kwibuka”.

Umekuwa ni utamaduni wa Rwanda kukumbuka matukio ya mwaka 1994, ambapo raia zaidi ya milioni moja waliuawa kinyama kutokana na siasa mbaya za serikali ya Rwanda ya wakati huo.

Mataifa mengi ikiwamo Tanzania iliyowakilishwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Rais mstaafu, Benjamin Mkapa na mkewe Mama Anna Mkapa yalihudhuria, pia mwandishi wa makala haya alialikwa kushiriki.

Dunia yote inajua kwamba mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 yalitokana na siasa mbaya za ubaguzi, watu wachache kuitawala nchi kwa manufaa yao na chuki, zinazowatenga watu badala ya kuwaunganisha.

Siasa mbaya inatengeneza propaganda chafu za kutukuza kikundi kidogo cha watu ndani ya nchi na kuwadharau wengine. Tuna mifano mingi duniani, lakini wa Rwanda uko hai. Rais Paul Kagame anasema mauaji ya kimbari hayatatokea tena Rwanda.

Kwa miaka 25 iliyopita Rwanda imekuwa ikipiga hatua kutoka katika siasa mbaya na kuingia kwenye mfumo wa siasa nzuri, inayolenga kujenga taifa moja lenye amani na mshikamano.

Ili kuonyesha ukweli huo, kabla ya ufunguzi wa siku za kumbukumbu, iliandaa kongamano la kimataifa la siku mbili lililowakutanisha washiriki zaidi ya 400 kutoka duniani kote kujadili jitihada hizo za miaka 25. Mada ilikuwa “Tunza kumbukumbu, tanguliza ubinadamu”.

Msimamo wa Rwanda, ni kuwa ili taifa lisonge mbele ni lazima kusamehe kwa gharama kubwa, yale yalitokea wakati wa mauaji ya kimbari, lakini ni muhimu sana kukumbuka ili kuhakikisha matukio hayo hayatokei tena katika historia ya mwanadamu.

Hoja kubwa ni kile tunachojifunza kutoka Rwanda, kwamba siasa mbaya ni mauti na daima itatafuta kulipiza kisasi. Siasa nzuri inasamehe, inatanguliza ubinadamu na inatunza kumbukumbu.

Kumbukumbu hiyo, kwa maoni yao, ni lazima iwe endelevu kwa vizazi vijavyo. Ndiyo maana waliazimia kufanya kongamano la kimataifa kujadili jambo hili la “Tunza kumbukumbu, tanguliza ubinadamu”. Hivyo mada mbalimbali zilizojadiliwa katika kongamano hilo ni pamoja na changamoto za vijana, kihistoria, haki na maendeleo.

Washiriki na wachokoza mada walizungumza mambo mengi kuhusu tukio la mauaji kimbari na namna Wanyarwanda wanavyoishi kwa amani sasa. Kwamba pamoja na yote, Rwanda inasonga mbele ina amani na mshikamano.

Rwanda inakumbuka yaliyotokea, lakini kwa uongozi bora na siasa safi, inasonga mbele. Mjumbe wa Tume ya Taifa ya maridhiano, Edouard Bamporiki anasema katika kongamano hilo kwamba kizazi cha sasa kimekuwa katika mfumo wa watu kuishi kwa haki sawa na kupata elimu sawa.

“Ni kweli watu wataendelea kupata maumivu kwa kile kilichotokea, msongo wa mawazo, lakini maisha ya amani ni ahadi… Kwa pamoja tunaweza kujiponya,” anasema Bamporiki.

Akaongeza: “Mauaji hayo yalitokea wakati nikiwa na umri wa takriban miaka 10. Nilikuwa hospitali na niliona mtu akikatwa kichwa pembeni ya kitanda changu. Nilikuwa sijui kwa nini kikundi kimoja kilikuwa kinaua kingine,”

Sasa anatambua umuhimu wa kuulinda ubinadamu na kuutetea kwa gharama yoyote ile.

Mchangiaji kutoka Afrika Kusini, Musupyoe Boatamo anasisitiza juu ya elimu ya watoto na wajukuu kuhusu mauaji ya kimbari kwa sababu familia zao ni waathirika wa mauaji hayo.

Wazo hili la kuwafundisha watoto na kutokaa kimya juu ya mauaji ya kimbari lilisisitizwa pia na wachangiaji wengi. Hata hivyo linaenda pia na msimamo wa Rwanda, wa kukumbuka na kutanguliza ubinadamu.



Columnist: mwananchi.co.tz