Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HOJA ZA KARUGENDO: Mzee Mengi na ulemavu wa fikra, siasa za Tanzania

Wed, 8 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Buriani Mzee Reginald Mengi. Mungu akupokee na upumzike kwa amani. Kuandika tanzia yako, ni sawa na kuandika kitabu au vitabu. Maisha yako yamekuwa ni mwongozo wa maisha. Tangu kifo chako yamesemwa mengi na sifa nyingi zimetolewa. Hata hivyo kuna moja la muhimu katika siasa na maisha ya Watanzania ambalo bado sijasikia wakilitaja – Ulemavu wa fikra.

Nilimsikia Mengi akiongelea “ulemavu wa fikra” kwenye matukio mawili tofauti. Kama si ulemavu wa fikra, maoni hayo ya Mengi yangezua mjadala mkali. Watu wangejiuliza ana maana gani, lakini yalipita hivyohivyo.

Mara ya kwanza nilimsikia akiongea suala hilo wakati akiongea na watu wenye walemavu. Aliwaambia wasifikirie kwamba kwa vile wana ulemavu wa viungo vya mwili, basi wao ndio walemavu; au kufikiri kwamba wao si watu muhimu katika taifa; au kujisikia unyonge na kukata tamaa.

Alisema hata watu wenye viungo kamili wanaweza kuwa walemavu na hasa ulemavu wa fikra. Kwa maoni ya Mengi, mtu mwenye ulemavu wa fikra hata kama ana viungo kamili, anaweza kuwa mnyonge na mtu asiyefaa katika jamii kuliko mtu mwenye ulemavu wa viungo.

Ukiziangalia siasa za Tanzania za matusi, vijembe, ubaguzi na ushabiki wa kupindukia; zinazotanguliza vyama badala ya uzalendo na utaifa, zinazoangalia madaraka badala ya utumishi na huduma kwa wananchi. Zinazopiga kisogo uhai na utu wa mtu na kutukuza madaraka na vyeo. Utakubaliana na Mengi kwamba kuna watu wana ulemavu wa fikra.

Maana kama mtu ana macho lakini hawezi kuona, ana masikio hawezi kusikia, ana pua, hawezi kunusa, huyu anakuwa ni mlemavu. Ni wangapi wanauona umasikini wa taifa letu? Wangapi wanayaona magonjwa yanayotishia uhai wetu?

Wapo watu wanazaliwa wakiwa punguani, vichaa na wendawazimu lakini pia kuna ulemavu wa fikra wa kujitakia au kulazimishwa. Lakini pia kumtawala mtu kimawazo kunaweza kusababisha ulemavu wa fikra.

Mtu ambaye ana ulemavu wa fikra, hawezi kutafakari. Atakazana kulimbikiza pesa ambazo hazitamnufaisha yeye wala familia yake. Pamoja na mifano hii ya wazi, bado kuna watu hapa Tanzania wanaendelea kulimbikiza pesa. Watu wanakufa kwa njaa, watoto hawawezi kwenda shule, Watu wanakufa kwa magonjwa yanayotibika, wakati kuna watu wachache wamelimbikiza pesa ambazo zingeweza kumaliza matatizo yote hayo!

Ndiyo maana tunakumbushwa kila wakati tunapowachagua viongozi wetu, tusiwapime kwa ubora wa viungo vyao – pua, miguu, urefu, ufupi au uzuri wa sura na uwezo wa kuongea lugha za kigeni.

Kiongozi ambaye ubongo wake hauwezi kutengeneza kumbukumbu na kuzitunza, anayeitizama maiti bila kutafakari, anayeziangalia kuni zikiteketea na moshi ukiishia mawinguni bila kutafakari, kwake mlemavu wa viungo vya mwili anaweza kuwa mzuri. Asante Mzee Mengi, kwa somo hili la maisha, Upumzike kwa amani.



Columnist: mwananchi.co.tz