Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HEKEYA ZA MLEVI; Machinga: Unabuni au unaiga?

31788 Gaston+Nunduma TanzaniaWeb

Sat, 15 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kwa muda sasa tumekuwa tukiongelea ujasiriamali. Juma lililopita tumepokea simu kutoka kwa mdau aliyejitambulisha kama “mfanya biashara mdogo wa nguo” kwa maana ya “Mmachinga”. Alikuwa anakumbusha kuwa nao wana hamu ya kupata mbinu mpya za kuimarisha biashara yao.

Kwa jinsi nilivyomwelewa nadhani yeye amejiondoa kwenye kundi la wajasiriamali kwa sababu ana utambulisho wake kama Mmachinga. Lakini ningependa ajue kuwa mfanya biashara yeyote mdogo anaweza kuwa mjasiriamali. Leo nataka kwanza kumfafanulia maana ya ujasiriamali na kisha tumfanye Mmachinga kuwa mjasiriamali kamili.

Mjasiriamali ni yuleyule mfanyabiashara mdogo aliyekuwa akiitwa “muuza ufuta”, “muuza pumba”, “muuza ubuyu”, “muuza matunda”, au “muuza nguo”. Kilichomfanya kuwa mjasiriamali ni kitendo cha kuongeza thamani ya bidhaa anayouza. Kwa mfano ubuyu ulikuwa ukiuzwa mafungu, lakini sasa tunaona ukiwa umefungashwa kwenye vikopo vya plastiki.

Ilikuwa ni nadra sana kumwona mtu mwenye hadhi yake akinunua fungu la ubuyu kando ya barabara. Ni watoto pekee walionunua bila kufikiria vumbi wala wadudu ambao wangeweza kuleta madhara katika miili yao kupitia chakula hicho. Ndipo wajasiriamali wakakiongeza thamani hadi ubuyu ukawa moja ya viburudisho.

Vivyo hivyo tukirudi kwenye mboga, ni watu wachache waliokuwa na ujasiri wa kununua dagaa kauzu (dagaa la uchungu) na kisamvu. Zilichukuliwa kuwa mboga za kimasikini ambazo mtu angekula kwa sababu tu hana fedha ya kununua mboga zingine. Kule Kenya dagaa linaitwa “sukuma wiki”.

Wabunifu walipoona hivyo wakaja na wazo la kuondoa vichwa vya dagaa, kuziosha na kuzikausha vizuri kisha kuzipaki kwenye vifungashio bora vya plastiki. Kisamvu nacho kilisagwa baada ya kuoshwa kabla ya kufungashwa kwenye vifuko vinavyoruhusu hewa kuingia. ‘Mabosi’ wakavutiwa nazo.

Kwa upande wa Wamachinga, bila shaka umeshawaona wale wanaomwaga nguo ardhini. Mbunifu atakuja hapo na kununua shati kwa Sh500 mpaka 1,000 Atakwenda kulifua na kulinyosha, kulipaki kwenye boksi safi na kuja kuliuza Sh5,000. Ina maana mzigo wa 10,000 yeye atauza 50,000.

Mjasiriamali ni mtu asiyeogopa kuthubutu wala kufeli. Changamoto za kibiashara kwake huwa fursa kwa sababu hupita pale waliposhindwa wengi. Na ni mshindani hasa anapokutana na wengine wa aina yake.

Machinga wa Ulaya anaitwa “Marching Guy” yaani “Kijana Mtembezi”. Biashara yake hufanywa kama hapa kwetu, lakini wao wanaamini zaidi katika kumfuata mteja kazini au nyumbani kwake. Na hujua mahitaji ya mteja wake, pale anapokuwa mjamzito humpelekea gauni maalum, na akishajifungua humsogezea vijiguo vya mtoto.

Silaha kubwa za “Marching Guy” ni pamoja na kufahamu mahitaji ya mteja wake, kumsikiliza anapolalamika au kushauri, kuwa na lugha nzuri kwa mteja na kumpa heshima na kumthamini. Inafikia mahala mteja anaona anafanyiwa huduma na si biashara, hivyo naye hasiti kulipa kiasi kikubwa hata kama ananunua kitu rahisi.

Mbinu hizi ni maarufu kwa wachuuzi kote duniani ingawaje katika baadhi ya maeneo bado wapo wasioelewa umuhimu wake. Wengine hudhani kuwa zinasaidia tu kumshawishi mteja anunue bidhaa. Wengi wetu tunazo namba za simu za waendesha pikipiki. Unapojiandaa kutoka nyumbani si ajabu ukampigia bodaboda aliye kilometa tano kutoka hapo kwako badala ya kuanza na aliye hatua kumi tu kutoka ulipo. Na wakati mkiendelea na safari si ajabu tena kumwona bodaboda aliyekupakia akipokea simu ya mteja mwingine.

Mahusiano haya hujengwa na silaha nilizozitaja hapo juu.

Mtu anapoisikia historia ya matajiri wakubwa duniani anaweza kutoamini siri ya mafanikio yao. Wengi wao walipita kwenye ujasiriamali wakiwa hawana misingi mikubwa, bali walinunua kiasi kidogo cha bidhaa na kukiongezea thamani. Lakini pia wenyewe wanakiri kuwa uaminifu na unyenyekevu kwa mteja hukuza biashara.

Siku moja katika miaka ya 1990, Reginald Mengi aliyeasisi harakati za kuondoa umasikini kwa vijana (SKUVI) alifanya mkutano wa wazi na vijana wake. Aliwasimulia jinsi alivyoanza kununua kalamu na kuziboresha vifungasho vyake, kisha kuzirudisha sokoni. Kalamu yake ikapendwa na kuhitajika kote nchini.

Badala ya kununua boksi moja, sasa alilazimika kununua katoni kadhaa na kuajiri vijana wa kufungasha. Akagundua kuwa mjasiriamali anaweza kubuni jambo lisilokuwa vichwani mwa wenye mitaji. Huo ulikuwa ndio mwanzo wa yeye kuingia ubia na baadhi ya makampuni makubwa.

Orodha ya matajiri wa Afrika haikamiliki bila kutajwa bilionea wa Malawi, Mike Mlombwa. Alilelewa na watu baki kwa sababu mama yake alikuwa masikini kiasi cha kushindwa kumpatia elimu ya Msingi.

Alianza kufanya vibarua akiwa na umri mdogo sana kwa malipo ya kusomeshwa.

Alipoanza kujitambua ndipo akaingia kwenye ujasiriamali. Alizunguka kwenye mipaka ya Zambia, Msumbiji na Afrika Kusini akinunua bidhaa duni zilizouzwa kwa bei ya chini, akaziongeza thamani na kuziuza kwa bei ya juu nchini kwao. Baada ya biashara ndogo kuvamiwa na wageni ndipo alipoanza biashara ya kukodisha magari maana alishapata mtaji.

Sasa ni bilionea mkubwa barani mwetu.



Columnist: mwananchi.co.tz