Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HEKAYA ZA MLEVI : Ushirikina hadi kwenye ibada!

46986 Gaston+Nunduma

Mon, 18 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kama kuna habari, matukio na mikasa inayoongoza kuchefua katika miaka hii ni ushirikina. Uite vyovyote upendavyo; juju, uchawi au nguvu za giza, kama inatendeka hadharani au sirini, kwa sifa au kwa machukizo hapa tutaiita ushirikina.

Uchawi ni jambo lisilokubalika kwenye jamii zote, lakini hasa kule kwenye makabila yasiyojua utani. Mtu anaweza kuchinjwa hata kabla hajathibitika kuhusiana na kadhia hiyo. Pengine akionekana kuwa na macho mekundu tu basi imekula kwake. Au yule anayetumia pesa bila kuonyesha anavyozitafuta… ole wake.

Nguvu za giza (au nguvu za shetani) ni neno linalotumika zaidi kwenye nyumba za ibada. Ushirikina umepachikwa jina hilo kwa sababu inasemekana hufanywa gizani, na pia ni kwa sababu unahusishwa moja kwa moja na shetani. Suluhu za kimaisha hupatikana kwa Mungu na siyo kwa shetani.

Kule Naijeria Jujuman ni mtu aliyeheshimika sana. Aliweza kwa nguvu zake kuzuia ama kuleta mvua, kujaza watu kwenye sherehe na mikutano ya hadhara na hata kuongeza mvuto wa wanasiasa na watu maarufu. Inasemekana viongozi wa kiimani, wa kisiasa, wasanii na wanamichezo wengi nchini humo hutengenezwa na juju.

Lakini unapomtazama Jujuman kwa jicho la tai unamwona ni mshirikina. Tofauti pekee ni tafsida inayotumika kuheshimu neno la juju. Na hizi ndizo ambazo hutuponza na kutuingiza kwa yule mwovu huku tukimshangilia kwa nderemo na mapambio.

Mifano mizuri imejitokeza siku za karibuni mkoani Njombe. Kila kukicha tumekuwa tukipokea taarifa za vifo na upotevu wa watoto. Hivi majuzi mtoto mwingine alipatikana akiwa amefariki katika kijiji cha Matembwe wilayani Njombe huku visa vya mauaji vilikuwa vimeshika kasi kabla ya kukomeshwa hivi karibuni.

Watoto wengine wakiwemo watatu wa familia moja wenye umri chini ya miaka 10 walipatikana wakiwa wamefariki katika mazingira ya kutatanisha huku baadhi ya viungo vyao kama macho, meno na sehemu za siri vikinyofolewa.

Kwa mujibu wa Serikali, uchunguzi wa awali ulibaini kuwa mauaji ya watoto sita wilayani humo yalichochewa na imani za kishirikina.

Washirikina wanaamini wanafanya hivyo kutimiza matambiko yao ya kijadi. Lakini kama nilivyotangulia kusema ushirikina hata ukipakwa uturi kuvutia nyumba za ibada bado ni dhambi, mwiko na makosa makubwa.

Kwenye imani tunawasoma makuhani wakitoa kafara za ndege na wanyama. Ni nabii mmoja tu mwenye habari ya kujaribiwa kumtoa mwanaye lakini zoezi likasitishwa ghafla. Maana yake halikuwa sahihi. Kwenye historia za Wahenga tunasoma na kuhadithiwa habari za “vijumba” vinavyojengwa chini ya miti mikubwa ya Uzaramoni. Sijawahi kusikia mtoto aking’olewa jicho na likatupwa hapo, bali nilishuhudia unga wa mahindi au ngano ukitumika kama sadaka au kafara.

Sasa michezo hii ya Njombe asili yake ni nini? Kule Kenya, muungano wa makasisi wa imani ya Kikristo umedai kuwa matukio ya mikasa hapa nchini yalitokana na kuingizwa itikadi ya uchawi katika siasa. Ulisema kuwa siyo hali ya kawaida kuanza kushuhudia mikasa ikifuatana hapa nchini, mingi ikiwa na taswira ya mazingaombwe.

Katika taarifa ya kuitisha maombi ya kitaifa ili kukomboa Taifa hili kutokana na nguvu hizo za uchawi wa wanasiasa, Askofu Kimani Wainaina anasema, “ushahidi kamili kuhusu hali hiyo ni kuporomoka kwa daraja la Sigiri katika Kaunti ndogo ya Budalang’i.”

Anasema, “daraja hilo likiwa chini ya ujenzi wa wanakandarasi watajika kutoka Uchina halingebomoka kiurahisi na kwa ghafla ikiwa hakuna uchawi ulihusika.”

Kama umeisoma kwa umakini taarifa hiyo, utagundua kuwa ushirikina ni nguvu inayotegemewa kubadili maisha, siasa na uchumi wa bara hili katika siku za usoni. Wakati binadamu wa leo anapaswa kuwekeza kwenye sayansi na teknolojia, huyohuyo anaharibu maandiko na kutangaza uhuni.

Ajabu kuu ni kwamba vitabu vyote vya kiimani vinafundisha kuwa tamaa si chaguo zuri. Lakini wasaka utajiri kwa njia za mkato wanazidi kuvamia nyumba za ibada na kuwachanganya kondoo wa Bwana. Ikumbukwe pia kuwa hao watoa kafara nao wanasaka utajiri.

Kila mmoja anayo haki ya kuabudu anachokiamini kwa mujibu wa Katiba, ilimradi tu havunji sheria. Na mimi siyo kwamba nafundisha namna ya kuabudu, ila nawashtua msije mkapelekwa mkengeni na wajanja. Rejeeni kwenye misingi yenu ya imani ili kusimamia unyofu wa dini zenu.

Vilevile msichoke kusoma historia na misukosuko ya kiimani. Mbona si muda mrefu sana kuna mjanja aliwafilisi waumini na akawatia moto kwa kisingizio cha “mwisho wa dunia?” Nasikia mjanja huyu alikwenda kujibadilisha uso na pua, na hata ukipishana naye usingeweza kumtambua.

Nafahamu jitihada za Serikali za kukomesha mawimbi haya yanayoibuliwa kwa nyakati tofauti. Lakini pia tunaiomba iongeze ukali wa meno yake kukomesha kafara zinazohusisha viongozi na nguvukazi ijayo ya Taifa. Yeyote anayehusika na utekaji au kuua watoto atazamwe kama adui mkuu wa Taifa letu.

Tena mwisho wa siku tumtwishe adhabu itakayomsimika kuwa mfano kwa wote wenye mwenendo kama wake.



Columnist: mwananchi.co.tz