Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HEKAYA ZA MLEVI: Timiza ndoto, usitimize jinamizi

50796 Gaston+Nunduma1

Sun, 7 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Chinga alikuwa na fulana nne na suruali nne tu siku hiyo. Akamaliza Jiji zima kuanzia asubuhi lakini sijui hakuwa na bahati au ndo mzunguko wa hela kwa wateja wake ulikuwa umebana… sijui. Mpaka saa kumi za jioni alikuwa hoi kwa uchovu na njaa.

Lakini hapa Jijini ukiwa na kazi hushindi na njaa. Alirudi jirani na maskani yake Magomeni akamvaa mama lishe. “Matajiri wengine kichefuchefu kweli,” alianza kumpanga. “eti nimemwonesha pamba akachomoa. Mi nshaondoka ndo anapiga simu kusema eti amezielewa”.

Mama alikuwa anaendelea kumsikiliza na ghafla akapigwa mzinga: “Ebu nipakulie wa kushiba maana Kinondoni parefu pale”. Mama akaingia kwenye jungu na kumpakulia ugali nyama miksa maharage, dagaa na mchicha. Bwana mdogo akapiga menyu na kuaga “dakika sufuri tu nakuletea”. Akala kona.

Ukweli siku hiyo kwake ilikuwa imekwisha. Akajifanya anaelekea Kinondoni lakini akakunja mtaa wa pili na kuingia skani. Alijitupa jamvini tumbo wazi na kuanza ndoto za Alinacha:

Aliota anamuagiza Jay Zee amletee viwalo ambavyo ndio kwanza vimetengenezwa na havijawahi kuonekana popote zaidi ya kwenye matangazo ya TV. Wauza nguo kutoka Marekani, Ulaya, Dubai na kwingineko wakajazana uwanjani kwake.

Jay Zee akiwa anajiandaa kuondoka, Chinga akapiga simu kwenye kampuni ya usafiri wa anga na kuagiza ndege ya kukodi imrushe Marekani mara moja. “Mwambie Kelvin Clain alete Jeans modo, na Nike walete traki, kapelo na raba”. Alisema huku akimkabidhi begi la dola, kisha akainua glasi yake ya mvinyo.

Papo hapo aliingia binti wa Sultani wa Oman. Akavua mtandio, akawasha udi na kumpulizia uturi kisha akafungua kasiki lake na kumimina matunda ya kiarabu… doriyani, kungu na mazagazaga kibao. Dogo wakati huo alikuwa amekunja nne akipepewa na kulishwa tunda moja moja la zabibu.

Alikuja kuzinduka saa tatu usiku washikaji walipotaka mchango wa ‘nguna’.

Maisha ni kama ndoto; hujui leo utaota nini. Zipo ndoto tamu lakini pia zipo za kutisha. Kwa kupenda ndoto tamu, watu wanajifanya kutozitambua zile za kutisha. Bongo tunaziita “jinamizi” na kule mamtoni badala ya kuziita dreams wanaziita nightmares.

Hata ukizipa tafsida, ndoto ziwe mbaya au nzuri zinabaki kuwa ndoto. Chanzo chake kikubwa ni mawazo yanayotokana na pilika za mchana kutwa, lakini pia na mawazo au matumaini ya maisha ya baadaye. Kwa asilimia kubwa mtu huwa anaota mawazo yake mwenyewe.

Kama huamini fikiria kinachokukumbusha yale yote uliyoota. Si ulilala fofofo? Sasa asubuhi unakumbukaje?

Tena ukitaka kuamini kwamba ndoto ni matokeo ya pilika zako za kila siku, jiulize kama ulishawahi kuota unamwangalia Mungu. Ni vigumu kwa sababu hujawahi kumwona, na akili yako haijatunza kumbukumbu ya sura yake.

Wakati mwingine unaweza kuota matukio ya wakati wa utoto au ujana kipindi ukingali mzee. Si jambo la ajabu kwa sababu nyuma ya jicho kuna retina inayotunza picha na kumbukumbu. Ieleweke kuwa wavumbuzi wa kamera walichukua mfano wa jicho kwa maana ya lensi, mkanda n.k.

Na ikumbukwe pia kuwa jicho na ubongo vinafanya kazi kwa ukaribu sana. Hii ndiyo sababu ya mtu kukumbuka matukio ya miaka kumi iliyopita. Au kukumbuka sura aliachana nazo tangu zama hizo.

Mchunguze mwanao mdogo akiwa amelala. Utagundua kuwa macho yake yanapepesa na kuzunguka akiwa ndotoni. Kitendo hicho kinathibitisha uhusika wa “pilika za mchana kutwa” katika ndoto.

Hapa Bongo utamsikia kila mtu anadai kutaka kutimiza ndoto zake. Kama nilivyosema awali, watu hupenda kuota kama chinga wetu hapo juu, akiota misukosuko hataki kuiita ndoto bali jinamizi. Lakini kaukweli kanabaki kuwa ndoto zako ni matokeo ya mawazo yako mwenyewe.

Nina maana kuwa si kila ndoto lazima itimizwe. Dogo mmoja aliyelelewa na babu Mchungaji wa Kanisa aligundua kuwa baba yake ni jambazi na mama ni kahaba. Kwa jinsi alivyoepushwa na nyendo za namna hiyo akajikuta akiota mauzauza kila usiku.

Siku moja aliota yeye na familia yake wakiwachinja na kuwala majirani zao. Babu yake alipokuja kuwafokea wakamkamata na kumfunga mikono. Mzee alikamata kisu, akaanza kuchinja kama kuku. Damu nyingi kama debe zima ikamrukia dogo, akashtuka na kupiga uyowe akiwa chini ya meza ya kusomea.

Huyu hatakiwi kabisa kufuata ndoto zake. Labda kama atapewa ushauri nasaha wa namna ya kuziepuka ndoto zake na kutengeneza ndoto mbadala. Kwani hazitengenezeki? Mbona Chinga na Alinacha waliweza?

Yupo bwana mmoja mkweli aliyetimiza ndoto zake lakini akaambulia kuchomwa mpaka jivu lake. Yeye alikuwa mkwapuzi wa pochi za mkononi. Wakati mmoja alipokuwa gerezani alifungwa na mwizi wa magari. Alianza kumwonea wivu mwenzie baada ya kugundua kuwa alikuwa na mjengo na familia safi kabisa.

Kidogo kidogo akaanza kuota kuiba magari. Akawaza jinsi atakavyokuwa na raha akimiliki nyumba ya kisasa, mke mzuri na watoto wenye afya bora. Si akataka kuitimiza!

La msingi ni kutimiza ndoto zenye tija kwako, jamii yako, Taifa lako na dunia yako. Ukizitimiza utaacha wosia kwa wengine kufuata ndoto zako.



Columnist: mwananchi.co.tz