Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HEKAYA ZA MLEVI : Mwisho wa mawindo mbwa hana thamani

48150 Gaston+Nunduma

Sat, 23 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katika kundi la wanyama wafugwao, hakuna anayependa starehe kuliko paka. Anamzidi hata binadamu kwani yeye hapendi kabisa kufanya kazi, bali kulala kwenye sofa na kutazama TV. Akiona picha ya samaki basi atateremka kutoka sofani na kuhamia jikoni akaonje mapishi ya siku hiyo.

Alipokuwa akitafuta mfadhili wa kudumu alikutana na swala, akalishwa kama mtoto. Kwa bahati mbaya mjomba simba alimkamata na kumla mfadhili wake. Akahamia kwa simba aliyemlisha mawindo yake. Lakini siku moja simba alijikoroga, akamdhuru mtoto wa tembo.

Tembo na mahasira yake alimkamata simba na kumpachika kwenye panda ya mti. Paka akaona kumbe tembo ndiye kiboko ya wote maana amemuadabisha hata yule aliyeogopwa kama mfalme wa wanyama. Kuanzia hapo akawa akiandamana na tembo.

Ukweli alikuwa na bahati sana, kwani kila alipoomba ufadhili alikubaliwa. Wakati uswahiba wa paka na tembo umepamba moto kuna jambo likatukia. Siku moja baada ya kushiba walilala chini ya mti. Lakini ghafla ukasikika mlipuko uliofuatiwa na kilio cha tembo.

Paka akamshuhudia bosi wake akimiminikwa na damu nyuma ya sikio. Akamwona mwindaji akitokeza kwenye vichaka huku gobore lake likifuka moshi. Alimtazama mwindaji akikata nyama ya tembo na kuijaza kwenye magunia, kisha akajitwisha moja.

Pamoja na huzuni aliyokuwa nayo, paka alimkimbilia mwindaji na kuongozana naye hadi nyumbani kwake. Aliamini kwa asilimia zote kuwa huyu sasa ndiye mwisho wa reli.

Lakini kabla hawajaufikia mlango lilitokea jimama kwa spidi ya kimondo, likauchukua ule mzigo na kusepa nao jikoni. Paka aliachia mdomo wazi: kumbe hata huyu ana kiboko yake! Akaunga tela nyuma ya jimama. Hiyo ndiyo sababu ya paka kupenda meko.

Hakukosea. Jikoni ndiko alikoweza kula bila kufanya kazi. Mwenzie mbwa anakula kwa jasho baada ya kuuza roho usiku kucha. Lakini yeye hata akitaka kubadilisha menyu anamkamata panya aliyeingia humo kisha anakunja nne kwenye sofa.

Asichokijua paka ni kwamba kila mwamba ana mwamba wake. Siku akiibuka mwamba wa jimama (ambaye ni talaka), hataliona hata hilo jiko. Mwindaji atakuwa akitoka na kibiriti chake tu.

Hakuna Taifa lililokosa tunu au raslimali. Kila Taifa kama sehemu ya dunia lina madini, gesi, bahari, misitu, jangwa (nalo ni raslimali). samaki au wanyama. Hivyo kama Taifa, linawajibika kugeuza raslimali zake kuwa kipato ama kutokana na ajira au utalii.

Mwafrika anaangalia mambo katika upeo mdogo sana. Anapoona mbuyu hakumbuki kuwa ulianza kama mchicha.

Leo hii anasoma habari na vitabu vya akina Christopher Columbus, Marco Polo, Napoleon, Julius Caesar na kadhalika kwa sababu wenzetu walimudu kutunza historia za mashujaa wao. Lakini pia kwa sababu walishaweka malengo ya kutawala, walikuwa wakizing’oa historia za wenzao na kupandikiza za kwao.

Kama mvuto wa kuwa shujaa mtu atajikoki kufuata nyayo za mashujaa hao. Mimi pia nawaita mashujaa kwa kuwa wengi wao walithubutu kuingia kwenye safari ndefu na za hatari. Lakini sikubali kuwa ati Speke alikuwa mtu wa mwanzoni kugundua Ziwa Victoria.

Mbona Wasukuma, Wajaluo na Waganda walilitumia ziwa hilo kutokea enzi na enzi katika maisha yao kabla ya kufika kwake? Walifua, wakaoga, kumwagilia mazao na kuvua samaki. Kama hawakulijua mbona walilita Nyanza, Nam Lolwe na Nalubaale?

Wala sikubaliani na Columbus kuwa ndiye wa kwanza kuvumbua Marekani. Historia inawataja Wahindi Wekundu kuishi hapo kabla yeye hajazaliwa.

Wajanja walishtukia mapema ishu hizi. Ukiwatajia Wachina “Coumbus” watakuuliza huo ni ugonjwa gani. Wao wana mashujaa wao akiwemo Mwenyekiti Mao. Na ukikomaa wanakuwa wadogo na kukubaliana nawe kama vile Wahindi walivyokataa Mahatma Gandhi kuitwa mhaini.

Sasa unajua tofauti ya shujaa na jasusi?

Shujaa ni yule anayethubutu kuhatarisha au hata kuutoa uhai wake akipambana na tawala dhalimu kuwalinda au kuwakomboa watu wake. Wapo mashujaa wengi waliofungwa magerezani na wengine kunyongwa hadharani kwa sababu kama hizo.

Lakini kwa kuwa madhalimu wanamlaani shujaa huyo kwa vitendo vyake watambadilishia jina. Yeyote anayepinga mamlaka kwa udhalimu wake aweza kuitwa gaidi, jasusi au mhaini na mamlaka hizo. Nyerere, Mandela, Kenyata na wengi wengine walipita kwenye nafasi hizo.

Tanzania ina historia ndefu iliyotukuka. Ni wazi michango ya mashujaa ilisaidia sana uwepo wake wa amani na utulivu hadi leo hii.

Lingekuwa jambo la maana iwapo kizazi hiki kingeendelea kupata historia za harakati zao kwa ukamilifu. Hivi sasa ni wanazuoni wachache sana wanaoweza kuwaelezea Mkwawa, Isike, Mirambo n.k. waliosimamia tunu za Taifa zisifisadiwe na wavamizi.

Naamini Elimu hii ikisisitizwa itakuwa njia nzuri ya kuimarisha uzalendo utakaofuta kabisa ufisadi.



Columnist: mwananchi.co.tz