Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HEKAYA ZA MLEVI : Kwa mganga hakuna bendera ya njano

44550 Gaston+Nunduma HEKAYA ZA MLEVI : Kwa mganga hakuna bendera ya njano

Mon, 4 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nilimwambia muuza bidhaa za dukani. “Nipatie sumu ya mbu”. Akanijibu “Wewe jiangalie na hicho Kiswahili chako usije ukafungwa! Tangu lini mimi nikauza sumu? Sema ‘dawa ya mbu”. Nami nikamwuliza “Kwani nataka kumtibu au kumuua?” Akabaki mdomo wazi.

Sijui kwa nini lugha nyingine zinakua wakati Kiswahili kinazidi kudumaa. Hivi ninavyosema “muuza bidhaa za dukani” wengine wananiangalia kwa macho makubwa wakitaka niseme “muuza duka”. Kwani analiuza duka lake au analitumia kuuza bidhaa?

Kuna usemi maarufu unaosema “Ukipatwa na ugonjwa usiende kwa mganga, bali nenda Hospitali.” Sasa kabla sijaanza kubwabwaja nirudi kwenye falsafa ya Leonardo da Vinci. Ilisema “Kuna watu wanaoona, kuna watu wanaoona kwa kuonyeshwa, na kuna watu wasioona kabisa”.

Hapa hakuwahusisha watu wenye ulemavu wa macho, bali alizungumza kama ilivyosemwa kwenye Vitabu Vitakatifu: “Mna macho lakini hamuoni”. Jicho linaponasa taswira huipeleka kwenye ubongo kutafsiriwa, na ndipo mtu hukitambua kile anachokiangalia.

Sasa turudi kwenye usemi wa “usiende kwa mganga”. Waliousema hawakuona, na tuwaonyeshe kile tutakachokiona.

Mganga ni mtoa tiba au tabibu. Kuna waganga wa macho, ngozi, mwili na maradhi mengine. Hivyo unapopatwa na maradhi huna budi kutafuta tiba ya maradhi yako inayopatikana kwa mganga.

Tatizo ni lugha. Ukimshauri babu yako aende kwenye elimu ya “ngumbaru” anaweza akakutia bakora. Lakini ukimwambia “Adult Education” atachekelea na kujiunga mara moja. Na ukitaka ugomvi na jamaa yetu anayelinda geti mwite “korokoroni”. Hata “kijakazi” wa Kilungule anaweza kudai aitwe “House Maid” kama mwenzake anayehudumia kwa Mzungu.

Tabibu… Akh! Sorry… Dokta mmoja alihangaika kumtibu mwanangu sikio bila mafanikio. Dawa zote ziligonga mwamba. Kwa kuwa alikuwa jirani yangu, siku moja alinijia na kichupa chenye majimaji ya kijani, akaniagiza kumdondoshea mtoto ndani ya sikio.

Sikuamini nilichoona; tone moja tu na mwanangu akapona. Nilimfuata na kumuuliza siri ya ile dawa. Ingawa hakuyafurahia maswali yangu alinijibu kuwa inaitwa Cannabis. Ni dawa isiyopatikana madukani na inawabidi wao waitengeneze.

Siku niliyokuja kupata maana ya Cannabis niliduwaa.

Nikiwa bado sijamalizana na suala la kunyanyapaa lugha zetu na kutukuza wageni, rafiki yangu ticha mkoba alinikaribisha kucheza Msondo kwenye bustani za Taxido. Kabla sijasahau nilimtaka anifafanulie tofauti ya dokta na mganga kwa taaluma yake ya ualimu.

Kwa kweli sikuzitendea haki mbavu zangu aliponijibu kwa ufupi sana: “Kwa mganga hukuti bendera ya njano” Nilicheka hadi nikapatwa na maumivu.

Kwanza nilipata jibu kuwa lugha, iwe ya picha, maneno au maandishi ina uwezo wa kuumba mambo. Katika vilinge vya waganga wa kienyeji (kuna waganga wa kienyeji na waganga asilia) haikosekani lugha ya picha itakayokuambia kuwa mganga huyu ni kiboko ya wote.

Kwanza kabisa utakutana na bendera nyekundu au nyeusi kama utambulisho wake. Bendera hiyo itakuwa na maandishi ya kiarabu ambayo hata Mwarabu mwenyewe hawezi kusoma. Pia itakuwa na mchoro maarufu wa fuvu na mifupa ya binadamu iliyo kwenye mtindo wa “X”.

Ushagundua anakupanga vipi mpaka hapo?

Mabaharia wanaelewa mbilinge za maharamia huko kwenye bahari kuu. Wakati meli zote hupeperusha bendera za mataifa yao, meli za maharamia hubeba bendera moja tu; nyeusi au nyekundu yenye alama ya “danger”! Hii huwaaminisha wanaotekwa kuwa wamekutana na viumbe wasiotaka utani.

Sasa kwa nini bendera hii ikatumike kwa matabibu wa kienyeji?

Inasemekana yupo mmoja kutoka nchi jirani iliyo Magharibi kwetu alivuka Ziwa na kuingia kwenye mkoa maarufu sana kwa ushirikina. Akaweka kilinge katikati ya kijiji cha walozi na kutangaza vita dhidi yao. Alipopandisha bendera ya maharamia wakajua hatanii, walozi wakakimbia na kuwaacha wahanga wao wakipata ahueni. Kila mganga aliyeona muvi ile aliilaiki na kuifollow.

Hata zilipoingia muvi za Kinaijeria tuliona jinsi masangoma wa kibongo walivyokopi mavazi mekundu na meupe pamoja na michoro ya usoni. Walikopi hadi matangazo ya: “Tunatoa hela za majini, kujiunga na Freemason, kusahaulisha madeni, n.k.”

Kwa hiyo waganga waliosomea au wenye vyeti hutaka kuitwa “Madokta” ili wajitofautishe na hao wanaokufutia madeni bila kulipa (na ingekuwa kweli basi benki zote zingefilisika). “Dokta” anaweza kukutibu kama “mganga wa asili”, lakini kamwe si “kama mganga wa kienyeji”. Unajua kwa nini?

Mganga wa asili hutibu kwa kutumia dawa za miti. Huweza kutumia magome, matunda, majani au mizizi kutengeneza dawa. Dokta hutumia dawa hizohizo lakini zilizosindikwa na zingine kuchanganywa na kemikali. Lakini mganga wa kienyeji anacheza na hisia zako.

Kwa mganga wa kienyeji kila mgonjwa huwa amerogwa. Wa pwani huwa ametupiwa jini na wa bara huwa ametupiwa kinyamkera.

Kama picha la Kihindi lakini maisha yanaenda.



Columnist: mwananchi.co.tz