Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HEKAYA ZA MLEVI: Kuti la mazoea lisizoeleke tena

32910 Gaston+Nunduma Tanzania Web Photo

Sat, 22 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ipo hadithi ambayo karibu kila msafiri aliyepita Kiwira mkoani Mbeya katikati ya miaka ya 80 aliisikia. Ilikuwa kama kibonzo lakini mashuhuda walituapia kuwa ilikuwa ya ukweli. Hadithi hii ilitusaidia wengi kuchukua tahadhari katika safari na kama sikosei ilipunguza pia ajali.

Mbeya ni moja ya mikoa muhimu sana kwa uzalishaji wa chakula. Wakati ule ulikuwa ni miongoni mwa “The Big 4”, yaani mikoa minne iliyoongoza. Ukiachilia mbali chakula, Mbeya ni Mikoa uliojaliwa vivutio vya kitalii na miujiza ya kihistoria. Kule kuna “vijungu” vya maji moto ndani ya maji baridi.

Hapa ninamaanisha kwamba kuna chemchem ya maji ya moto kiasi cha nyuzi za sentigredi mia na zaidi katikati ya mito. Huko ndiko nilikokula kwa mara ya kwanza kiazi kilichoivishwa katika mto wa maji baridi.

Kule Mbozi ndiko kwenye alama za nyayo na michoro inayosemekana kuwapo kwa zaidi ya miaka 3000. Tena ndiko kimondo kilipoamua kuangukia kutoka mbinguni na kuweka makazi ya kudumu. Wilayani Kyela kulikuwa na visima vya asili ambavyo ukitupia sarafu na kupiga kelele, maji yake yaliruka kulingana na ukubwa wa sauti yako.

Kwa sababu hiyo Mkoa huu ulikuwa na pilika nyingi sana za usafiri na usafirishaji uliinganisha na Mikoa mingine. Tulisafiri kwa reli ya Tazara, mabasi ya TRC, Scandinavia, Zainab’s, Scaba Scuba, Kuku ni Mali na mengi mengine. Safari yetu ilianzia Dar na kuishia Tukuyu, hivyo ilikuwa ni lazima tupite Kiwira, katikati ya Mbeya Mjini na Tukuyu baada ya kupambana na milima kwa mwendo mrefu.

Mabasi maarufu kwa kule yalikuwa Leyland na Scania LBT 81. Scania zilijimudu sana milimani kwa sababu zilikuwa na mifumo ya haidroliki, lakini zilitweta mno miteremkoni. Mateminolojia yanasema zilikuwa ‘zinabalansi upepo’. Kinyume chake, Leyland zilizopuyanga bila mifumo hiyo zilipata shida milimani; basi lililalamika kama paka wa usiku. Kama ungeteremka na kutembea sambamba nalo ungeliacha nyuma. Lakini mabondeni ilikuwa kama kumsukuma mlevi.

Kiteremko cha Kiwira kilikuwa kirefu kikifuatiwa na kona kali iliyoenda kushoto. Baada ya mwendo wa kiasi barabara ilikata kulia, kisha kulia tena na kumalizia kushoto. Kwa ufafanuzi ni kwamba ilibidi barabara ikwepe bonde kubwa sana na ndipo iendelee mbele.

Kama ni mara yako ya kwanza kupitisha gari hapo ilikupasa uwe makini maradufu. Ukiwa unaelekea Tukuyu huwezi kuliona lile bonde zaidi ya barabara iliyonyoka baada ya bonde. Magari mengi yaliyoshuka kwa kasi yalifeli kukata ile kona, yakapaa kuingia bondeni. Kwa sababu hiyo mahala hapo paliitwa “Uwanja wa Ndege”.

Hapo sasa ndipo ile hadithi maarufu ya Kiwira ilipotukia.

Dereva mmoja maarufu wa mabasi aliacha kazi kwenye kampuni moja na kuhamia kwa mahasimu wao. Akapewa Leyland Victory jipya na kutengeneza hofu kwa wasafirishaji wengine wa abiria. Inasemekana vikao vya siri vilifanyika kuhusu njia za kumzuia asiharibu biashara zao.

Huyu bwana alitoka Dar kwa mbwembwe akiwaonesha ‘machejo’ hadi Kiwira, ambako ndiko zilipokuwapo ofisi zao. Hakutaka kuingia kwani alipania kumaliza ruti yake kwanza. Basi alikanyaga mafuta hadi utingo akashtuka. Lakini alipojaribu kumkumbusha habari ya Uwanja wa Ndege, dereva alicheka tu.

Ngoma iliteremka na spidi zote hadi ilipoikaribia ile jehanamu. Kwa mikogo bwana mkubwa alijitikisa kwenye siti na kuanza utaratibu wa kubadili gia na kupunguza mwendo. Hammadi! Kila alichogusa hakikumwitikia! Klachi hamna, gia hamna, breki hamna na hata taa hamna!

Dereva alipigwa ganzi mwili mzima. Alifumba macho na kupiga dua kimyakimya. Wakati wote abiria walitulia kwani walifahamu uzoefu wa dereva wao.

Lakini kwa mshangao alipojaribu tena kila kitu kikaamka. Gari ilishika breki ya ghafla na kupiga chafya nzito sentimeta chache kabla haijatumbukia.

Kwa jinsi alivyopigwa na wenge, dereva aligeuza gari na kuanza kurudi alikotoka. Hapo ndipo abiria walipoanza kelele za kutaka kujua kinachoendelea, lakini bingwa aliuchubua hadi walipofika ofisini Kiwira. Alikabidhi swichi ya gari na kuwataka watafute dereva mwingine! Tukiwa tunaelekea mwisho wa mwaka, ni lazima tukumbushane yale yanayojiri kila unapofika wakati kama huu. Tumekwishaanza sherehe zinazomalizia mwaka, hatuna budi kujitathmini matendo yetu ya kila mwaka hadi hapa tulipo. Ipo imani potofu kuwa kila jambo ni lazima lijirudie, badala ya watu kung’amua kuwa wao ndio wanaoyarudia mambo.

La kwanza ni ajali. Kwa sababu mwisho wa mwaka wasafiri ni wengi basi wasafirishaji pia huongezeka. Ni kipindi ambacho watu huwa radhi kukesha kazini ili kuongeza kipato. Wengine watakwepa kupeleka vyombo vyao kukaguliwa au kurekebishwa kwa kuogopa kuikosa ‘bingo’.

Sasa tunaishi kisasa zaidi. Kama tutafuata utaratibu uliowekwa ajali za miaka ya 80 zitaepukika kirahisi. Tupaze sauti tuonapo waendesha vyombo vya usafiri wanakengeuka. Tusijekuwa kama abiria waliomwamini dereva mzoefu hadi akataka kuwatupia kwenye “Uwanja wa Ndege”.

Lakini pia huku mtaani tuchukuliane kibinadamu zaidi. Inawezekana tulikwazana katika nyakati za kutafuta riziki, au hata katika harakati za kujiokoa. Kijiji kinapolipukiwa na bomu hakuna anayekumbuka kumtafutia babu mkongojo na miwani yake. Kila kunguru anakuwa bize kuepusha ubawa wake kwanza.



Columnist: mwananchi.co.tz