Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HEKAYA ZA MLEVI : Hata kipimo cha gundua feki nacho ni feki

55629 Gaston+Nunduma

Tue, 7 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Viumbe hai kibaiolojia tumegawanywa katika makundi ya wanyama na mimea. Wote tunafanana katika tabia za msingi kama mahitaji ya chakula na hewa. Lakini tunatofautiana kwa aina ya mahitaji hayo, wanyama huvuta hewa ya oksijeni wakati mimea huvuta hewa ya kaboni.

Wanyama wa leo nao hutofautiana kwa aina ya maisha wanayoishi. Kulingana na vitabu vya historia, wote waliishi kwa kufanana kabla ya binadamu kuanza kuvumbua. Mwanzo wote walilala mapangoni, walikula chakula ghafi, walitembea utupu na kadhalika. Binadamu alijitenga na wanyama wengine kufuatana na mageuzi (evolution) ya upande wake.

Alipoanza kuishi kwa ustaarabu alijijengea mazingira ya aina hiyo. Alipika chakula bora, akatengeneza nyenzo bora, kifupi aliishi maisha bora. Sasa badala ya mawe alichonga mikuki, majembe na mashoka. Alisindika na kuchemsha dawa zake badala ya kutafuna magome na mizizi ambayo ingeweza kumletea madhara mengine.

Kadiri karne zilivyokuwa zikienda binadamu huyu akaanza kufanya makosa ya kujitakia dhidi ya ustaarabu wake. Alipoitambulisha fedha kama kipimo cha mabadilishano alitazama faida za wakati huo tu bila kuangalia athari zake.

Hasara kubwa zaidi ya fedha ni kwamba imeachiwa kuendesha maisha ya aliyeitengeneza. Watu wakaacha kufanya kazi na wakahaha kutafuta fedha. Hata wanafunzi hawasomi kwa lengo la kupata na kuongeza maarifa, bali kufaulu ili kupata kazi itakayowaingizia fedha.

Simama barabarani usimamishe gari; hata kama ni ya Serikali na ilikuwa inamfuata Waziri itasimama kwa breki kama zote. Usidhani dereva ana huruma sana, bali badala ya kuona anapungiwa na mtu, yeye anaona akipungiwa na noti!

Hivi sasa ni vigumu sana kupata bidhaa au huduma zenye viwango halisi (a.k.a. OG). Kila kitu ni feki. Hata kama ungekuwa na kipimo cha kugundua feki, basi na chenyewe kingekuwa feki. Hujawahi kuona aliyeuziwa mali feki naye akalipwa hela feki?

Hatukatai kuna viwango tofauti vya ubora wa bidhaa zinazozalishwa viwandani. Wenzetu Wachina wameweka wazi kwa wateja wao; Kwa mfano ukitaka kununua bidhaa kwao watakupa bei za viwango vya juu, kati na vya chini (high, normal na low standards).

Mfanyabiashara kwa kutaka faida kubwa atanunua bidhaa za ubora wa chini na kuziuza kwetu kwa bei ya viwango vya juu. Hatari zaidi ni pale anapokopi na kutengeneza zake ambazo hazina ubora kabisa (no standards). Hizi sasa ndiyo feki orijino.

Kimsingi simu ya kuchezea watoto haiwezi kuwa sawa na ile ya matumizi ya kawaida. Lakini hapa hautaambiwa ila utashangaa kununua Nokia ya thamani ya dola mia nane huko Marekani kwa dola mia mbili hapa. Ikibuma usilalamike kuwa Mchina anatengeneza feki, feki ni sisi wenyewe.

Ipo lugha inayochefua sana madukani; ile ya “unataka panado za Kenya au Tanzania? Ingefaa kama TBS wanakubaliana na viwango vya chini iwalazimishe wafanyabiashara kuainisha tofauti za viwango kwenye kifungashio. Mbona watengeneza sigara wamelazimishwa tangazo la kuikanyagia?

Utamlipa fundi wa gari lako lakini yeye atakuwekea gasket feki, kituo cha mafuta kitakujazia feki, muuza simu atakupa feki, pampasi za watoto feki, Au asubuhi nenda zahanati ukapime malaria. Utaambiwa “una malaria 2000!” Rudi mchana kapimwe malaria, taifodi na UTI uambiwe “huna malaria ila UTI kilo nne”! Utaondokaje hivihivi bila kuacha hela ya vidonge? Unawaachaje?

Mbaya zaidi mfamasia alitengeneza dawa za kutuliza maumivu zinazofunga mishipa ya fahamu kuhisi maumivu. Mkulima ameweka mbolea ya kemikali ili mimea yake izae utotoni. Mfugaji atawadunga sindano ili wakue na wauzwe kabla hawajatokwa na ubwabwa wa shingo.

Mama lishe atapika ugali na kuutia hamira ili uumuke. Kwa kufanya hivyo atatoa sahani nyingi zitakazompatia fedha ya ziada. Ukimkwepa usidhani kuwa umesalimika kwa sababu utaukaanga mchicha uliokuzwa kwa mbolea ya sumu ukitumia mafuta ya kula yaliyosindikwa kwa sumu.

Ukweli ni kwamba hatuko salama hata kidogo. Katika hali hii hatuna jinsi ya kujilinda kwa gharama yoyote. Kule India mtu anayekula chakula chenye viungo vingi ndiye anayepunguza sumu mwilini, lakini kwetu usijaribu.

Mzee Makongoro aliimba wimbo uliotumika kama ufunguo wa kipindi cha “Afya Zetu” cha Redio Tanzania Dar es Salaam akiimba: “Kuleni kuku, mayai, mboga, samaki, maziwa…” Na kweli wakati huo hicho ndicho kilikuwa chakula bora. Lakini leo usithubutu, tena weka mbali na watoto!

Sasa tule nini?

Wakati mwingine mimi natamani tungerudi nyuma kabla ya ustaarabu. Sijawahi kusikia mnyama pori akiugua moyo, ini au figo. Hapa maradhi haya yalianza taratibu hasa kwa wazee waliokuwa dhaifu. Lakini leo mtoto anazaliwa na kisukari!

Niliposema kuwa sasa tukilinde wenyewe sikuwa na maana ya kutangaza mgomo kwa chakula. Tunaweza kuanza na kususia vyakula vilivyosindikwa kwenye makopo kama maharage, nyama ya kusaga na nyinginezo. Halafu tuachane na matunda yanayotoka nje ya mipaka.

Ni kwa sababu muda wa chakula kuwa hai ni mfupi sana. Wenyewe mnaona maharage yakilala bila kuchemshwa yanavyokuwa. Hivyo kwenye kopo inaongezwa kaboni ili kuilinda.

Tukimudu kufanya hivyo ndipo tutaweza kushughulika na wazalishaji wetu.



Columnist: mwananchi.co.tz