Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

HEKAYA ZA MLEVI: Bora mnyama mwenye utu au mtu mwenye unyama?

26463 MNYAMA TanzaniaWeb

Sun, 11 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mama asiye na maadili alisikika akimtukana bintiye mdogo, “We ng’ombe ntakudunda! Niangalie hivyohivyo mijicho kwadu kama guluguja. Misikio mirefu kama sungura lakini husikii kama ngedere. Mbwa we!”

Mlevi mmoja akauliza, “Eti mama’ke mbwa, huyo mbwa kakufanyaje?”

Akaununua ugomvi. Alizatikwa maneno yote machafu uliyowahi kuyasikia. Mama alimfananisha bintiye na ng’ombe, guluguja, sungura, ngedere na mbwa, lakini yeye alipoitwa mamake mbwa likawa zengwe.

Binadamu na mbwa wote ni wanyama. Sijui chanzo cha jina mbwa lakini binadamu lilitokana na ubin wake na Adamu, baba yetu aliyeumbwa siku za mwanzo. Yeye alipewa uwezo wa kubatiza viumbe vyote kwa jinsi alivyoona inafaa.

Inasemekana hapo mwanzo viumbe hai wote walisikilizana kwa lugha ileile. Lakini baada ya hawa kwenda huku na wengine kule, walianza kutofautiana lugha, maumbile na hata tabia. Wengine walikwenda kuishi jangwani, wengine maporini na wengine pwani. Huwezi kumfananisha binadamu anayewinda na kula nyama na yule anayeshindia tende,

Huo ni mfano tu, lakini kila sehemu kuna mchanganyiko wa mambo na baadaye tabia. Tukapata tofauti ya binadamu wenye ubinadamu na wasio na ubinadamu.

Baadhi ya sifa za ubinadamu ni kujali. Hapa nina maana ya kujijali binafsi na kuwajali wengine. Baadaye ubinadamu ukarithiwa na utu. Bin Adam aliweza kujikidhi lakini asiwe na utu. “Binadamu yule ana utu”.

Kule Japan watu wanadhani utu una mahusiano na aina ya damu ya mtu. Mwenye damu ya kundi A ni mtulivu, anachukua mambo kwa uzito, na ni wenye kujali sana. yule wenye kundi la B ni mkarimu, lakini mwenye hasira, anayeweza kudanganywa kirahisi.

Kwa kutegemea dhana hiyo, watu huona damu kuwa muhimu kazini, kwenye mahusiano na hata wakiwa shuleni. Wanaotaka kuoana hupima kwanza makundi yao ya damu ili kuona iwapo wataendana. Kifupi kwao makundi ya damu ni kama nyota kule Uarabuni. Huko watu huamini kuwa mtu mwenye nyota ya Simba hawezi kuishi na mwenye nyota ya Mshale.

Ingawaje binadamu yu katika kundi la wanyama kwa sifa ya uzazi na unyonyeshaji, lakini utu humuondoa katika kundi hilo la wanyama. Ukitaka kumuudhi mtu mwite “mnyama” au “mbwa”. Ni afadhali unapomwambia “we shetani mkubwa” anakuvumilia.

Mpaka leo zipo sehemu kama Amazon ambazo ukienda kufungua duka la nguo ujue imekula kwako. Hawaoni sababu ya kuvaa nguo na hawana matumizi ya fedha. Wakiamka kazi yao kubwa ni kuwinda, kuvua samaki na kuvuna matunda ya porini.

Kwa kuwa sifa ya utu inahusisha kujisitiri, viumbe hawa wamekosa kabisa sifa ya utu. Wamekuwa wanyama kama walivyo wanyama pori wengine.

Lakini kitu kikubwa kinachoshangaza ni kwamba wanyama kama mbwa na wengine wote wanatunza uasilia maradufu ukilinganisha na watu. Wanazaa na kulea watoto katika njia zao, wanafundisha na kufundishika na wanaishi kwa kutumia milango yote ya hisia waliyoumbiwa.

Wanyama hawa hufanya tendo la ndoa kwa lengo moja tu; kuzaana. Wanakula na kunywa pale tu wanapohitaji, na pia hutumia dawa za asili kutoka kwenye mimea pale tu wanapoumwa.

Kinyume chake mtu hunywa dawa za kuongeza wowowo. Atakunywa zingine za kuzuia ujauzito, kisha watakwenda kula na kunywa pombe nyama na kufanya ngono kibiashara. Hatimaye atakunywa dawa zingine za kutoa ujauzito ulionasa bila kutarajia.

Pale anapokula ziada anaongeza sumu mwilini. Kwa mfano akishakula mchana anawaalika wadau kukutana pale kwenye kitimoto. Wanagonga kilo kumi wakishushia na unywaji usiokata kiu. Matokeo yake wanaongeza protini na mafuta yasiyohitajika miilini, ndipo msosi unapogeuka kuwa sumu.

Binadamu anaposhindwa kumuua mtoto wake akingali tumboni, anakwenda kumtupa chooni au jalalani. Kitendo hiki kinamtoa kabisa kwenye utu. Hata tunaposema kuwa “kafanya unyama” ni wazi kuwa tunawasingizia kwa sababu hakuna mbwa aliyewahi kujaribu ukatili wa namna hii.

Binadamu ndiye mnyama pekee anayefanya ngono kinyume cha maumbile. Tena ni yeye anayewafundisha wanyama wengine kufanya nao kitendo hiki.

Wengi tumesoma habari za wanaumbe kuwafanyia wasichana wadogo ukatili wa kijinsia, pia tumesoma za mabinti kutupa au kutelekeza watoto, lakini hatujasoma kuhusu mbwa aliyemwokoa msichana wa miaka mitatu huko Poland.

Mtoto Julia alitoweka nyumbani usiku kwenye mji mdogo wa Pierzwin. Zaidi ya watu mia mbili walitoka kumsaka wakifuata alama. Msako ulipoingia vichakani ulisikia sauti ya mbwa akibweka kwa dalili ya kuomba msaada.

Wakaifuata sauti na kumkuta mbwa wa jirani akiwa amemkumbatia mtoto kumkinga na baridi iliyopiga kwa kiasi cha nyuzi hasi 5 sentigredi. Hakuna aliyeamini.

Ingewezekana mbwa kumrudisha mtoto nyumbani. Lakini kumbuka kuwa hali ya baridi ilikuwa ni nyuzi hasi tano, yaani ilishuka kutoka sifuri. Hivyo kwa kuogopa mtoto kudhurika, mbwa alimkumbatia kumpa joto na kuomba msaada.

Je, siku utakayomtupa mtoto jalalani halafu mbwa wako akamwokoa na kukurudishia utajiita wewe mtu na yeye mbwa? Kwanza nadhani hakuna mbwa atakayefanya upumbavu wa kukurudishia. Atampeleka Ustawi wa Jamii ili kumwokoa na mnyama wa aina yako.

Columnist: mwananchi.co.tz