Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Gamba, Samadu, Kaiza magwiji walioondoka na sauti zao

28113 Pic+gamba TanzaniaWeb

Wed, 21 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Sauti zao hazitasikika tena zikipasua anga kwenye vyombo vya habari vya ndani na hata vya kimataifa kama tulivyowazoea. Ni magwiji watatu ambao wameondoka na sauti zao wakipishana kwa siku chache katika safari yao ya mwisho.

Wako kimya milele kwenye nyumba zao za kudumu zilizohifadhi miili yao kwenye Wilaya za Bunda, Muleba na Missenyi katika mikoa ya Mara na Kagera. Kila mmoja ametimiza wajibu wake kadri ya karama aliyopewa na Mungu.

enga ushawishi kwa wasikilizaji na kuibua matamanio kwa vijana kupenda utangazaji na wapo walioingia kwenye fani hiyo kwa ushawishi wao.

Sio rahisi kuziba pengo waliloliacha kwenye sekta ya habari lakini ni rahisi kujifunza kwao. Sio watangazaji wote waliofanikiwa kuvuka mipaka na kutumikia vyombo vya habari vya kimataifa. Kwa vyovyote vile walikuwa na sifa ya ziada.

Bila shaka mafanikio ya Isack Gamba, Samadu Hassan na Florian Kaiza katika utangazaji hapa nyumbani na kimataifa yametokana na msaada wa watu mbalimbali, taaaisisi, nguvu na juhudi binafsi.

Samadu Hassan

Tutamkosa Samadu Hassan na sauti yake iliyorindima kwenye taarifa za habari za kimataifa kwenye kituo cha Star tv na vipindi vingine huku akionyesha umahiri wake katika anga za kimataifa na kujipambanua kwa mtindo uliowavutia watazamaji na wasikilizaji. Amezikwa katika Kijiji cha Mafumbo Wilaya ya Muleba mkoani Kagera. Ni miongoni mwa watangazaji wachache nchini ambao licha ya ukongwe wao waliendelea kuwa na mvuto.

Usomaji na uandaaji wake wa makala fupi za kuvutia hasa katika anga za kimataifa ulikuwa ni wa kipekee.

Liliwahi kuandaliwa pambano na wasomaji wa mtandao wa JamiiForum kati yake na wakongwe wengine kwenye vituo vingine vya runinga. Maoni ya baadhi ya wasomaji yalimweka Samadu Hassan katika daraja la juu la watangazaji wenye mtindo wa kipekee na umakini katika matamshi.

Isack Gamba

Mapokezi makubwa ya mwili wa Izack Gamba kuanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es salaam (JNIA) hadi nyumbani kwao Bunda ukitokea Ujerumani alikokuwa akifanya kazi katika Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani (DW) na baadae kufariki dunia, ni wazi ameacha mema mengi ya kukumbukwa.

Ni mtangazaji aliyetajwa na mkongwe mwingine Charles Hilary kuwa pamoja na uwezo wake pia alikuwa na ubunifu uliosaidia kubadilisha kipindi cha michezo cha Redio One na kuleta msisimko zaidi.

Charles anasema pamoja na mambo mengine kubwa zaidi alilojifunza kwa mtangazaji huyo kijana ni usikivu na kwamba hata alipoona amepata nafasi ya kwenda nje ya nchi kwenye kituo cha kimataifa hakushangaa kwani alitarajia hilo. Aliamini taifa limepata mwakilishi mzuri kimataifa kwenye utangazaji kimataifa.

Hata Salum Mwalimu aliyewahi kuwa mtangazaji wa Channel ten sasa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Zanzibar anasema ndoto yake isingetimia kama sio Gamba kuruhusu sauti yake kusikika hewani kwa mara ya kwanza hatua iliyomfungulia njia ya kuonyesha uwezo wake katika utangazaji.

Florian Kaiza

Kwa upande wa Florian Kaiz (69) mtangazaji wa zamani wa DW na Redio Tanzania kifo chake kiliongeza ukubwa wa pengo katika kipindi ambacho maombolezo ya Gamba na Samadu yalikuwa yanaendelea.

Mazishi ya Kaiza yalifanyika katika Kijiji cha Buhanga, Kata ya Bwanjai Wilaya ya Missenyi, Kagera. Kipaji chake katika utangazaji kilianza kuchomoza tangu utotoni na wazazi wake wakampa nafasi ya kukikuza.

Kwa mujibu wa Padri Anthony Rugundiza wa Jimbo Katoliki Bukoba aliyeongoza ibada ya mazishi ya alisema Kaiza alianza kuitamani kazi ya utangazaji akiwa kijana mdogo. “Alikuwa akijificha nyuma ya boksi na kuigiza akisoma taarifa ya habari huku wenzake wakisikiliza”.

Anasema siri hiyo alielezwa na Kaiza mwenyewe mara kadhaa walipokutana nchini Ujerumani na kusema alikuwa miongoni mwa Watanzania wachache aliowatambulisha kwa wafanyakazi wenzake wa DW.

Akiongoza ibada ya mazishi ya mtangazaji huyo, Padri Rugundiza alisema Kaiza ni mfano wa vijana ambao vipaji vyao vililindwa na kukuzwa hadi kufikia hatua ya kutambulika Kimataifa na kutoa wito kwa wazazi na walezi kutambua vipaji vya watoto wao.

Safari ya kuzungukia vituo tofauti vya redio duniani kama Redio China na Sauti ya Ujerumani akiwa ametokea Redio Tanzania pengine isingewezekana kama wazazi wake wasingekuwa na mchango katika makuzi ya kipaji chake.

Alisisitiza matumizi sahihi ya muda na maandalizi mazuri kabla ya kuingia kazini ni vitu vinavyochangia mafanikio ya mtu kwani vinginevyo Kaiza asingeweza kufikia hatua hiyo kama asingekuwa na maandalizi ya kutosha kila anapoingia kwenye kazi ya utangazaji.

Hakuna anayeweza kuandika kwa usahihi kuonyesha milima na mabonde waliyopita magiwji hao hadi ngazi za Kimataifa kwenye utangazaji. Ni bahati mbaya wako kimya kabla ya kuandika kitabu kutueleza hayo tusiyojua juu yao.



Columnist: mwananchi.co.tz