Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Fedha chache tulizonazo zitumike vizuri kujenga nchi

13232 Pic+fedha TanzaniaWeb

Thu, 23 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katika miaka ya hivi karibuni Zanzibar imefanikiwa kupiga hatua nzuri na ya kufurahisha ya kurahisisha usafiri wa barabara kutoka eneo moja la visiwani kwenda jingine.

Barabara kuu nyingi za Zanzibar ambazo zilikuwa nyembamba sana na kuwepo shida kwa gari mbili kupishana, zimepanuliwa na njia nyingi za vijijini ambazo zilikuwa hazipitiki sasa zimetengezwa.

Kwa hali ilivyo hivi sasa sio lazima kama ilivyokuwa zamani kwa mtu anayetoka eneo moja la kijiji kwanza kwenda mjini ndio aanze upya safari ya njia ya kumpeleka sehemu nyengine.

Miaka michache iliyopita ilikuwa sio rahisi hata kidogo kwa mtu kufunga safari ya kutoka kaskazini kwenda kusini na kurudi siku hiyohiyo. Siku hizi habari hizo ni sehemu ya ugumu wa usafiri uliokuwepo visiwani miaka ya nyuma.

Kwa kweli Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inastahiki pongezi kwa hatua iliyochukua ya kuimarisha miundombinu ya barabara.

Hata hivyo, yapo mambo mengi ambayo yanafaa kuangaliwa kwa umakini mkubwa na kupatiwa suluhisho la kudumu.

Kwanza ni juu ya umadhubuti wa baadhi ya hizi barabara ziliojengwa hivi karibuni. Zipo barabara ambazo muda mfupi baada ya ujenzi kukamilika na kutumika huwa katika hali isiyoridhisha kama vile zilijengwa kwa ajili ya matumizi ya dharura.

Hii inapelekea kutumia fedha nyingi kuzifanyia matengenezo ya mara kwa mara kila baada ya muda mfupi, hasa baada ya kumalizika msimu wa mvua.

Zipo sehemu huwa zinatuama maji kwa muda mrefu na kuwa na madimbwi kama vile wakati wa ujenzi yaliwekwa maeneo maalumu kwa kufugia samaki au kuwarahisishia bata kutafuta maeneo ya kuogelea.

Vilevile wakati mwingine utawaona watoto wadogo wanajitumbukiza katika haya madimbwi na kuhatarisha afya zao.

Ujenzi wa barabara

Hapa panajitokeza masuala mengi juu ya matayarisho ya ramani za ujenzi na ukaguzi wa umadhubuti wa hizo barabara wakati kazi ya ujenzi ilipokuwa inaendelea.

Zipo barabara zenye kona na vilima vidogo ambavyo kwa hali ilivyo ni hatarishi na huenda ikawa ndio sababu ya kuongezeka kwa ajali za barabarani ziliopelekea watu kupoteza maisha yao na wengine kuwa na vilema.

Hali hii ingeweza kuepukwa kama pangetumika utaalamu wa kuyafanya maeneo hayo kuwa katika hali bora zaidi.

Malalamiko ya wananchi

Hivi sasa upanuzi wa barabara nyengine kuu, kama ile ya kwenda Kaskazini Unguja unaendelea. Lakini, pamekuwepo na malalamiko ya wananchi juu ya namna ujenzi huo unavyoendelea.

Kwa mfano katika matayarisho ya ujenzi Chuini na Mfenesini vijiko vimekuwa vikiharibu mabomba ya maji safi na salama na kupelekea watu wa maeneo haya kukabiliwa na shida ya maji.

Hapa ungetarajia kwanza kuchukuliwa hatua za kuhamisha hayo mabomba au kuweka mengine ambayo wakati barabara inajengwa hapatakuwepo na usumbufu wa watu wa sehemu hizo kupata maji safi na salama.

Hivi sasa wengi wa watu wa maeneo haya wanategemea zaidi maji ya mito, mabwawa na ya visima ambayo usalama wake una mashaka makubwa.

Hatari iliopo ni kwamba maradhi ya miripuko, kama kipindupindu na malaria, hasa wakati wa misimu ya mvua imekuwa kama vile ni mambo ya kawaida visiwani katika siku za karibuni. Miripuko hii ya maradhi imepelekea watu wengi kupoteza maisha yao.

Ni vizuri kila inapotaka kupanuliwa barabara masuala ya upatikanaji maji safi na salama na kuhakikisha huduma ya umeme hupatikana bila ya usumbufu, kupewa umuhimu mkubwa.

Hii itawapa wananchi wa maeneo hayo kufurahia kuona upanuzi wa barabara badala ya kuona uamuzi huo umewaletea usumbufu mkubwa na hata kuona bora hio barabara nyembamba iliopo hapo ingebakia ilivyokuwa awali. Mara nyengine huwa ninashangazwa na wakati ambapo ujenzi wa hizi barabara unapofanyika.

Nilitarajia kazi kama hii ingefanywa wakati wa kiangazi na kuchukuliwa tahadhari ya kutofanyika wakati wa mvua ili kupunguza gharama za ujenzi na kurahisisha kazi ya ujenzi kuendelea bila ya matatizo na kwa gharama nafuu.

Wakati umefika wa kufanya utaratibu wa ujenzi wa barabara mpya ili kwanza kuwa na uhakika wa umadhubuti wake na kuondoa usumbufu ambao sio wa lazima kwa wana vijiji ambapo barabara hizo zinapita.

Vilevile pawepo na mawasiliano na mashirikiano mazuri na watu wa Idara ya Maji na Shirika la Umeme Zanzibar.

Haingii akilini hata kidogo kuona muda mfupi tu baada ya ujenzi wa barabara mpya kukamilika na kuanza kutumika ndio wanafika watu wa Idara ya maji kuichimba barabara ili kupitisha mabomba ya maji.

Jambo jingine linalofaa kuzingatiwa kwa umakini ni aina gani ya magari hutumia hizo barabara mpya, hasa zinazokwenda vijijini.

Siku hizi Zanzibar yapo magari makubwa na mazito ambayo hubeba vifaa vizito, saruji, mchanga na mawe.

Mara nyingi utayaona magari hayo makubwa yanatumia barabara ambazo kutokana na namna zilivyojengwa haziwezi hata kidogo kuhimili uzito huo.

Ujenzi wa barabara, tokea unapoanza kazi ya upimaji na utengenezaji wa ramani hadi ujenzi unapokamilika hugharimu mabilioni ya shilingi ambazo hupatika kwa shida, mara nyingi kwa njia ya mkopo.

Ni vizuri kutilia maanani thamani ya fedha nyingi zinazotumika mpaka ujenzi wa barabara kukamilika.

Zanzibar haina utajiri wa kuwa na fedha za kuchezea kwa ujenzi wa barabara na utengenezaji wa mundombinu mengine.

Yapo maeneo mengi, kama ya elimu na afya ambayo yana mapungufu mengi ya vifaa vya kusomesha na dawa muhimu kutokana na uhaba wa fedha.

Kwa hivyo, ni vyema hizo pesa kidogo ziliopo lazima zitumike vizuri ili maendeleo ya ujenzi wa barabara yaende sambamba na maendeleo ya elimu, sekta ya afya na maeneo mengine.

Columnist: mwananchi.co.tz