Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Fahamu umuhimu wa makundi adimu ya damu

Makundi Ya Damu Pc Data.png Fahamu umuhimu wa makundi adimu ya damu

Sat, 11 Dec 2021 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Umewahi kuchangia damu salama ili kuokoa maisha ya wenye uhitaji? Jukumu hili ni la kila mmoja wetu ambaye atakuwa na sifa ya kufanya hivyo, kwani damu haipatikani sehemu nyingine yoyote zaidi ya kutoka kwa binadamu.

Kutokana na umuhimu wake, Mpango wa Taifa wa Damu Salama umeanzisha mkakati wa kuwapata wenye makundi adimu ya damu, ili kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa damu katika makundi hayo.

Makundi hayo adimu ya damu ni yale yenye razazi (-) ambayo yana uwezo wa kuyachangia makundi yote, mfano kundi la damu la O-(O negative).

Kuna makundi makuu manne ya damu ambayo ni A, B, AB, O na kila kundi lina aina yake ya razazi ambazo ni (+) na (-).

Akizungumza katika mafunzo ya siku moja kwa wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari kuelekea kampeni ya ukusanyaji damu kuanzia Desemba 13 hadi 17, Mkuu wa Idara ya Ukusanyaji Damu katika mpango huo, Dk. Avelina Mgasa anasema wameanzisha mkakati huo ili kuwatambua, kuhifadhi na kuwatunza wachangiaji wenye makundi adimu ya damu.

“Kuna makundi mengine ni nadra kupatikana kwa watu. Kundi hilo lina uwezo wa kuyachangia makundi yote, mfano kundi la O negative, lakini yeye anachangiwa na mwenye kundi lake pekee,” anasema Dk Mgasa.

Advertisement Watu wenye kundi A+ wanaweza kuongeza damu kwa wenye kundi A+ na AB na kupokea damu kutoka kundi A+, A-, O+ na O-, kundi B+ wanaongeza damu kwa kundi B+, AB+ na kupokea damu kutoka kundi B+, B-, O+ na O-.

Pia watu wenye kundi O+ wanaongeza kwa wenye kundi O+, A+, B+ na AB-, huku wakipokea kutoka kundi O+ na O-. Kundi AB+ anaongeza damu kwa kundi lake pekee na kuwapa wote wa makundi mengine.

Kwa mwenye makundi adimu A- anaongezwa damu na kundi A+, A-, AB+ na AB- na kupokea kutoka kundi A- na O-, kundi B- anaongeza kwa makundi B+, AB+ na AB-, huku lenyewe likipokea damu kutoka kundi B- na O-.

Nalo kundi la AB- linaongeza damu kwa AB+ na AB- na kupokea kutoka kundi AB-, A-, B- na O- wakati kundi O- lina uwezo wa kusaidia wagonjwa wote wenye kuhitaji damu, lakini yeye watu wote hawawezi kumsaidia pindi anapokuwa na uhitaji isipokuwa mwenye damu inayooana na yake pekee.

“Kwa kuwa ni watu wachache wenye kuwa na aina ya kundi hili la damu, si Tanzania tu bali duniani kote, hivyo kundi hili la damu ni nadra kupatikana kwa urahisi, ndiyo maana tukaita kundi adimu la damu,” anasema.

Dk Mgasa anasema kutokana na hali hiyo, watatengeneza rejista maalumu yenye taarifa ya watu wote wenye makundi yote adimu ya damu pamoja na kuandaa ratiba maalumu ya uchangiaji wa damu kwa makundi hayo, ili kufanikisha upatikanaji wa damu hizo kwa wakati.

“Tutawabadilisha wachangiaji damu wanafamilia kuwa wachangiaji wa damu wa hiari, hivyo tutawaunga kwenye makundi ya whatsapp kwa ngazi au mikoa hadi kanda, ili kusaidia kunapokuwa na uhitaji,” anasema.

Anasema mwaka 2019/2020 idadi ya wachangia damu kwa kundi A- walikuwa 1,565 sawa na asilimia 0.5, kundi B- (1,192) sawa na asilimia 0.4, kundi AB- (267) asilimia 0.1, huku kundi O- walikuwa (3,643) sawa na asilimia 1.2.

Naye Ofisa Tathmini na Ufuatiliaji, Dk Wilhelmus Mauka anasema kwa mwaka 2021/2022 wameweka malengo ya kukusanya damu chupa 375,000 ambayo ni sawa na asilimia 75 ya mahitaji ya damu nchini.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linataka angalau watu 1,000 wachangie damu chupa 10, lakini kwa hapa nchini hivi sasa watu 1,000 wanachangia chupa sita za damu.

Hata hivyo, alisema kuna ongezeko la ukusanyaji wa damu kila mwaka, kwani katika mwaka wa fedha 2020/2021 walikusanya chupa za damu 331,279 ukilinganisha na chupa za damu 12,597 zilizokusanywa mwaka 2005 wakati mpango huo ulipoanzishwa.

“Kumekuwa na ongezeko la makusanyo ya chupa za damu kuanzia mwaka 2016, hasa baada ya mpango kuanza kufanya kazi ya ukusanyaji damu kwa kushirikiana na timu za halmashauri zote nchini,” anasema Dk Mauka.

Sasa kuna timu 286 kutoka timu 7 mwaka 2015 na zinachangia zaidi ya asilimia 60 ya damu zinazokusanywa na timu za halmashauri.

Anasema katika kukabiliana na changamoto ya ucheleweshaji wa majibu, kuongeza ufanisi wa utendaj kazi wa mpango, kanda zote saba zimewekewa mfumo ambao unatambua damu salama.

Sifa za uchangiaji damu

Ofisa Viwango na Ubora Kanda ya Mashariki, Samwel Mduma anasema wenye sifa ya kuchangia damu ni wale wenye umri usiopungua miaka 18 na usiozidi miaka 65, uzito usipungue kilo 50 na wingi wa damu uwe zaidi ya 12.5g/dl.

Anasema pia asiwe na magonjwa kama shinikizo la damu au kisukari, asiwe katika tiba yoyote na kwa mwanamke asiwe mjamzito au anayenyonyesha.

“Mwanamume anaweza kuchangia damu kila baada ya miezi mitatu na mwanamke anachangia kila baada ya miezi minne,” anasema.

Changamoto

Thomas Mhongole, Mkuu wa Idara ya Tehama anasema wananchi bado hawajapata elimu ya uchangiaji damu wa hiari na umuhimu wake.

Anasema kwa miaka mingi wanafunzi ndio walikuwa wachangiaji wakubwa wa damu, lakini kwa sasa wengi wanamaliza masomo ya sekondari wakiwa na umri chini ya miaka 18.

“Changamoto nyingine ni wananchi wengi wanasubiri wapate mgonjwa ndipo wachangie damu, hali inayosababisha kuwapo kwa uhaba wa damu,” anasema.

Mhongole anasema suala lingine ni usumbufu kwa wachangiaji damu pindi wanapokuwa na wagonjwa, kwani wanalazimika kuchangia tena hata kama wao ni wachangiaji wa hiari.

Pamoja na hayo, kuna changamoto kubwa ya uuzwaji wa damu hospitalini, hali inayorudisha nyuma juhudi za uchangiaji damu wa hiari.

Pia anasema jamii inatakiwa kuwa na mwamko wa uchangiaji damu, kwani ipo baadhi ya mikoa kama Mwanza, Dar es Salaam, Dodoma na Kigoma imekuwa ikifanya vizuri katika uchangiaji wa damu, huku mikoa ya nyanda za juu kusini ikiwa haifanyi vizuri.

Columnist: www.mwananchi.co.tz