Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Fahamu namna ya kuanzisha kampuni ya bima

Thu, 20 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Biashara ya bima ni moja kati ya miradi muhimu inayolipa licha ya changamoto zake. Kuna Watanzania wengi wanahitaji huduma hizi na upo uhitaji na umuhimu mkubwa wa kuanzisha kampuni nyingi zaidi za bima.

Sheria ya Bima ya mwaka 2009 inaitambua Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (Tira) kuwa ndio pekee inayosimamia utaratibu na utekelezaji wa masuala ya bima nchini.

Kazi kubwa ya mamlaka hii ni kutoa leseni na kusimamia utekelezaji wa kanuni na utaratibu katika kampuni zote zilizopo nchini kwa kuzingatia misingi iliyowekwa.

Kwa mtu yeyote anayetaka kufanya biashara ya huduma za bima ni lazima apeleke maombi kwa kamishna. Maombi hayo yataandikwa katika fomu maalum na ikiwa muombaji ana maelezo ya ziada anaweza kuambatanisha katika fomu hiyo.

Kifungu cha 24 cha sheria hiyo kimeweka utaratibu wa kutoa kibali ama leseni ya biashara ambao unasema ni lazima kamishina wa bima azingatie mambo kadhaa kabla muombaji hajaanza kuhudumia wateja.

Kati ya masharti yaliyowekwa ni lazima muombaji awe ni kampuni iliyosajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Kampuni na makao yake makuu na ofisi kuu za kampuni hiyo yawe Tanzania.

Muombaji anatakiwa kuwa mwanachama wa chama cha watoa huduma ya bima. Watendaji wake wakuu na watendaji wa ofisi lazima wawe ni Watanzania.

Muombaji pia ni lazima awe na mtaji unaotakiwa na alipe ada ya usajili kama itakavyotangazwa na waziri mwenye dhamana. Kwa mujibu wa Tira, vitu vingine vinavyohitajika kuipatia leseni kampuni ya bima ni kujaza kulipia ada husika fomu ya maombi.

Pia utapaswa kuwasilisha katiba ya kampuni, ada ya usajili, nakala ya cheti cha usajili wa kampuni na nyaraka zinazoonyesha umiliki wa mtaji wa kampuni. Umiliki wa wazawa kwenye kampuni haupaswi kupungua theluthi moja ya mtaji wa kampuni husika.

Wasifu wa mtendaji mkuu pamoja na wajumbe wa bodi ya kampuni wanapaswa wasipungue watano. Ni lazima uwasilishe wasifu wa maofisa wakuu wa kampuni. Wasifu huo wa watendaji na wakurugenzi unapaswa uambatane na kiapo juu ya ufilisi ya mashitaka ya jinai.

Ni muhimu kuzingatia kuwa kampuni inapaswa kuwa na namba ya mlipa kodi, leseni ya biashara na maelezo ya kina ya riba za fedha katika kampuni nyingine za bima, madalali na mawakala ilionao.

Usisahau kuhusu wakaguzi wa hesabu, benki, washauri wa kisheria, mchanganuo wa biashara wa kati ya miaka mitatu hadi mitano.

Nyaraka nyingine zitakazohitajika ni maelezo ya kampuni na shughuli zake, akaunti ya kodi na taarifa ya fedha. Utahitaji kuwa na sanduku la posta, anwani ya ofisi, nakala ya vyeti vya wamiliki wa hisa, mpangilio na mfumo wa huduma za kampuni.

Wasilisha pia nakala ya hati za kusafiria za wakurugenzi wa kampuni na uthibitisho wa huduma za bima kutoka kampuni ya bima.

Kuanzisha na kusajili kampuni ya bima na kutoa huduma bora za bima inawezekana. Chukua hatua ili ulete utofauti katika biashara ya bima Tanzania.

Sekta ya bima ni miongoni mwa maeneo ambayo wazawa wengi hawajayachangamkia. Huu ni wakati muafaka wa kufanya hivyo ili kuongeza ushiriki kwenye uchumi. Wakati Serikali inatekeleza sera ya ujenzi wa uchum wa viwanda, ni muhimu kukumbuka kuwa biashara na miradi mingi inahitaji bima. Wafanyakazi wa kampuni zilizopo na zitakazoanzishwa wanahitaji huduma hii pia jambo linalotoa mwanya kwa wenye nia ya kuongeza chanzo cha mapato kuchangamkia fursa.

Kitu muhimu, kama ilivyo maeneo mengine, ni kuzingatia sheria na kanuni zilizopo.

Columnist: mwananchi.co.tz