Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Elimu bila malipo ilivyosababisha wazazi, walezi kubweteka

Thu, 29 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

“Tumeshaambiwa elimu ni bure kwa hiyo suala la kuchangia halipo tena, hatupaswi kuchangia chochote labda kwa utashi wa mtu binafsi. Elimu ni bure,”

Hivi ndivyo mmoja wa wazazi wenye watoto wanaosoma katika Shule ya Sekondari Ukwava, Kata ya Ulaya wilayani Kilosa, Christina Emilian anavyozungumza akieleza anavyoelewa kuhusu elimu bila malipo.

Anaamini kila kitu ikiwamo sare za shule, madaftari, kalamu na chakula kwa ajili ya mwanaye atavipata shuleni.

Sio yeye tu wapo wazazi na walezi wengine waliozungumza na Mwananchi wilayani Kilosa kuhusu elimu hiyo wakisema bure inamaanisha hakuna haja ya kuchangia na hawapaswi kuguswa kwa chochote.

Katika kikao kati ya wazazi na uongozi wa Shule ya Sekondari ya Zombo wilayani humo, kilicholenga kuweka mikakati ya kuwasadia wanafunzi wa kidato cha tatu kufaulu mitihani ya kidato cha nne hapo mwakani, mzazi mmoja aligoma kushiriki katika michango kwa kuwa elimu ni bure.

Japo wazazi wenzake walimsihi wakimweleza umuhimu wa kuchangia chakula cha mchana kwa watoto wao, alikataa katakata.

“Mtoto wangu atakula nyumbani, sina uwezo huo,” anasema Elias Mganga.

Katika kikao hicho wazazi walikubaliana kuhakikisha watoto wao wanapata chakula cha mchana kwa kuchangishana, isipokuwa mzazi huyo tu.

Utafiti uliofanywa na shirika la HakiElimu (2017) kuhusu Matokeo ya Utekelezaji wa Sera ya Elimu bila malipo ulibaini kuwa uelewa wa wananchi kuhusu jambo hilo bado hauridhishi.

HakiElimu inasema ikiwa hali hiyo haitatatuliwa ubora wa elimu utashuka kila mwaka.

Uchunguzi wa Mwananchi wilayani Kilosa ulibaini wapo wazazi na walezi wanaoamini wanaweza kushirikiana na Serikali kutekeleza sera hiyo, lakini wengine wanaona mzigo wa kusomesha watoto wao umetuliwa, hawapaswi kushiriki kwa chochote.

Utata huo ndio uliomlazimu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako akiwa bungeni kusema kuwa michango haijakatazwa hasa kama mzazi ataamua kutoa kwa hiyari yake.

Kauli ya Profesa Ndalichako ilijikita kwenye Waraka Namba 3 wa mwaka 2016 ambao umeainisha majukumu ya wadau mbalimbali wakiwamo wazazi ambao wana wajibu wa kuchangia sehemu ndogo ya michango kwenye shule za msingi.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Zombo, Masahau Magaga, anasema jukumu lake ni kuwashauri wazazi kuwekeza kwa watoto wao ili kuongeza ufaulu.

“Mfano ni kwenye chakula, kama watoto watakaa na njaa tangu asubuhi hadi saa tisa usitegemee ufaulu mzuri kwa mhusika,” anasema Nagwagwa.

Waraka huo wa elimu bila malipo unaruhusu wazazi kuchangishana kwa kukubaliana.

Hali halisi

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mazinyungu, pia ya wilayani Kilosa Ngamba Manegese, anasema tatizo lililopo katika jamii ni kuelewa kitu gani wanapaswa kushirikiiana na Serikali katika kuboresha elimu.

Anasema kwenye shule yake waliposikia elimu bila malipo baadhi ya wazazi walitaka kwenda kubeba chakula walichokuwa wamechangishana kwa ajili ya watoto wao kupata mlo wa mchana wakiwa shuleni.

Pia, anasema wapo wanafunzi waliofika kuanza kidato cha kwanza wakiwa hawana sare za shule kwa kudhani watazikuta shuleni.

Anasema alilazimika kuzuia baadhi ya wazazi na walezi kuchukua chakula walichokuwa wamechangia kwa ajili ya watoto wao ili kiendelee kutumika.

“Wanashindwa kutambua nini wajibu wao, hawajui kwamba wanapaswa kushirikiana na Serikali kuwezesha elimu bila malipo,” anasema.

Mwenyekiti wa bodi ya Shule ya Sekondari ya Ukwiva, Rubanga Mapesi anasema wanajamii wengi walipokea elimu bure wakiamini hakuna chochote wanachopaswa kuchangia.

“Ni vigumu kuwashawishi wachangie mambo muhimu yanayojitokeza shuleni. Wanachojua ni elimu bure basi! Hata chakula tu imeshindikana hivyo watoto hawali,” anasema.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Ukwiva, Efatha Makele anasema wazazi wamegoma kuchangia elimu katika shule yake. “Hawataki hata kusikia nadhani kuwaelimisha kutawasaidia kutambua kwamba ili kutekeleza mkakati wa elimu bure hawapaswi kukaa mbali na Serikali”.

Ofisa Elimu wa Wilaya ya Kilosa, Paula Nkane anasema uelewa mdogo wa jamii kuhusu elimu bila malipo ndio unaosababisha changamoto.

“Hii sio elimu bure ni elimu bila malipo kwa hiyo kazi kubwa iliyopo ni kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili kulitambua hilo,” anasema.

Kiuhalisia mzazi anapaswa kuhakikisha mtoto wake anakuwa na vifaa vya kujifunzia, ameshiba na amevaa sare.

Hata hivyo, anasema kwa sababu wilaya hiyo ipo kwenye mkakati mkubwa wa kuongeza ufaulu, jitihada zimeelekezwa katika kuhakikisha jamii inapata uelewa wa kutosha kuhusu elimu bila malipo.

Wazazi wazungumza

Baadhi ya wazazi waliozungumza na Mwananchi wanaamini mzigo wa elimu wameutua baada ya kuletewa elimu bila malipo.

Hata hivyo, wapo ambao wanaona suala la kushiriki katika elimu bila malipo ni wajibu wao.

“Siwezi kuchangia wakati nimeshaambiwa elimu ni bure, mtoto wangu atasoma bure kama chakula atakula akirudi nyumbani,” anasema Caros Lucas mkazi wa Kilosa.

Mzazi anayeunga mkono uchangiaji kwenye sera ya elimu bure, Idrissa Jacob anasema walichopunguziwa ni mzigo mzito wa kulipa ada na baadhi ya vifaa vya kujifunzia kama vitabu na michango ambayo ilionekana ni mzigo.



Columnist: mwananchi.co.tz